Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amezindua nembo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika November 27 mwaka huu na kuwakabidhi wakuu wa mikoa muongozo wa uchaguzi huo.

Akizungumza wakati wa Uzinduzi huo leo Agosti 15,2024 Jijini Dodoma, Waziri huyo wa TAMISEMI amesema Serikali itahakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uwazi na haki.

Uzinduzi huo unaweka msisitizo kuhusu maandalizi ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na uandikishaji wa wapiga kura na taratibu nyingine muhimu zinazohusiana na uchaguzi ambapo Waziri Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa uchaguzi katika kukuza demokrasia na ushiriki wa wananchi katika utawala wa mitaa na kupata viongozi bora .

Waziri Mchengekwa ameeleza utaratibu wa zoezi hilo kwa kufafanua kuwa, “Kuchukua fomu za kugombea 01 Novemba, 2024,Kuanza kwa kampeni 20 – 26 Novemba, 2024, Siku ya Uchaguzi 27 Novemba, 2024,” Amefafanua Waziri huyo mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa na kueleza kuwa;

Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 ibara 4(1-3) (Matangazo ya Serikali Na. 571, 572, 573 na 574) ya mwaka 2024, ninautangazia umma wa Watanzania na vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuwa tarehe 27 Novemba, 2024 itakuwa ni siku ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara, “amesisitiza.


Waziri Mchengerwa amesema lengo ni kuzifanya Serikali za Mitaa kuongozwa kidemokrasia na kwamba vongozi wanaochaguliwa katika ngazi hizi ni wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, wenyeviti wa mitaa, wajumbe wa kamati za mitaa na wenyeviti wa vitongoji ambapo Uchaguzi wa mwisho wa Serikali za Mitaa ulifanyika mwezi Novemba mwaka 2019.

” Uchaguzi huu unaongozwa na Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya vijiji, Vitongoji na mitaa katika Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji, Matangazo ya Serikali Na. 571, 572 573 na 574 ya Mwaka 2024,kwa mujibu wa Kanuni hizi,Mtu yeyote anayekusudia kugombea nafasi za uongozi, atatakiwa kuchukua fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi husika siku zisizopungua ishirini na sita kabla ya siku ya uchaguzi kwa kadri itakavyoelekezwa na Msimamizi wa Uchaguzi,”amesema.

Ili kuweka usawa, amesema kutakuwa na Kamati ya Rufani katika kila Wilaya ambayo itasikiliza pingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea katika Wilaya husika ambapo Wajumbe wa Kamati ya Rufani watateuliwa siku saba kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea. (m) Ukomo wa kuwa Madarakani:

Amefafanua kuwa,”Nafasi zote zinazogombewa zilikuwa na uongozi kwa kipindi cha miaka mitano,kwa mujibu wa Kanuni hizi, viongozi hao watakoma kushika nafasi za uongozi siku saba kabla ya siku ya kuchukua fomu za kugombea uongozi chini ya Kanuni hizi, “amesema.

Kuhusu Kampeni za Uchaguzi amefafanua kuwa,kulingana na Kanuni kampeni za uchaguzi zitafanyika siku saba kabla ya siku ya uchaguzi na kwamba kanuni hizo zinaelekeza, kila Chama cha Siasa kinachoshiriki uchaguzi kuwasilisha ratiba yake ya mikutano ya kampeni ya uchaguzi kwa Msimamizi wa Uchaguzi si chini ya siku saba kabla ya kuanza kwa kampeni.

“Upigaji wa kura utaanza saa mbili kamili asubuhi na kumalizika saa kumi kamili jioni,ninawatakia uchaguzi mwema, amani na utulivu katika kipindi chote cha uandikishaji, uteuzi wa wagombea, kampeni, upigaji kura, wakati wa kutangaza na kupokea matokeo ya uchaguzi, “amesema.

Please follow and like us:
Pin Share