Wakati Rais Dk. John Magufuli akihimiza kubana matumizi ya idara na taasisi za serikali, hali ni tofauti kwa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Shilingi bilioni 1.1 zimetumika kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 kuhudumia vikao vya bodi hiyo. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, bodi imekaa vikao 20 tofauti na utaratibu unaoagiza vikao viwe vinne kwa mwaka na viwili kwa dharura, ambavyo mara kadhaa huwa vya kuandaa bajeti na ukaguzi wa fedha.

Wakati hayo yakiendelea, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kuwapo kutoelewana miongoni mwa wajumbe wa bodi. Kutoelewana huko kunatokana na ufujaji unaofanywa na bodi inayoongozwa na Profesa Abiud Kaswamila.

Kuna taarifa za uhakika kuwa mwenyekiti amekuwa akitofautiana na baadhi ya wajumbe kuhusu matumizi mabaya ya fedha kupitia wingi na urefu wa vikao vya bodi.

Mwaka jana pekee, katika kipindi cha Juni hadi Novemba bodi hiyo ilikuwa imekwishakaa vikao zaidi ya vitano.

Muktadha wa kuitisha kikao cha dharura cha bodi (Extra-ordinary board meeting) unatokana na endapo kunatakiwa majibu ya hoja za ukaguzi au bajeti. Mara nyingi vipengele hivyo viwili huwekwa katika ratiba ya vikao vya bodi vya kawaida.

Imebainika kuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida, bodi imekuwa ikitumia siku nyingi kwa kila kikao kimoja. Mfano, bodi hiyo ilikaa kwa siku 10 kuanzia Novemba 4-13, mwaka jana; ilhali kwa kawaida vikao hivyo hutakiwa kuwa vya siku mbili hadi nne – kulingana na uzito wake.

Katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali (CAG), inaonyesha kuwa Bodi ya NCAA ilifanya vikao 20 na semina 6 kwa mwaka wa fedha 2017/18 na kutumia Sh bilioni 1.1.

CAG anasema sambamba na fedha hizo, kuna hoja ya mahudhurio ya timu ya menejimenti kwenye vikao vya bodi ya wakurugenzi katika kutimiza majukumu yao ya kuisimamia menejimenti.

CAG amependekeza Menejimenti ya Mamlaka ya Ngorongoro ipunguze gharama za kuendesha vikao kwa kuwa na vikao visivyozidi vinne kwa mwaka na wale maofisa wa ngazi za juu tu ndio wahudhurie.

Katika hatua nyingine, imebainika kuwa Mwenyekiti Kaswamila ametaka awe na ofisi ya kudumu katika makao makuu ya NCAA hifadhini; jambo ambalo linapingwa kwa kuwa yeye kwa nafasi yake hana kazi za kufanya kila siku.

“Anataka afanye kazi za menejimenti, amehakikisha baadhi ya watumishi hata walio katika ngazi ya wakurugenzi wanaondolewa kwa sababu ambazo hazina mashiko. Kuna mpango wa kuwarejesha baadhi ya wakurugenzi na mameneja walioondolewa NCAA kwa ufisadi na rushwa,” anasema mmoja wa watumishi wa NCAA.

JAMHURI limemtafuta Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Kaswamila, ambaye amejibu kupitia ujumbe mfupi wa maandishi wa simu ya mkononi. Amekataa kutoa ufafanuzi wa masuala yanayoisibu bodi yake, badala yake ametaka menejimenti ndiyo izungumze.

“Asante…Naomba uwasiliane na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro ambaye ni msemaji wa mamlaka…tafadhali atakutolea ufafanuzi wote,” amesema Profesa Kaswamila.

Katika hatua nyingine, tathmini ya CAG imebaini kuwa kuna tofauti ya taarifa za watalii kati ya Idara ya Utalii na Idara ya Fedha kutoka NCAA.

“Nilibaini kuwa Idara ya Utalii ilirekodi jumla ya watalii 1,040,618 na 787,032 kama jumla ya watalii wa nje na wa ndani mtawalia, wakati Idara ya Fedha ilirekodi watalii wa nje na wa ndani 1,016,607 na 791,140, mtawalia.

“Idara ya Utalii ilirekodi watalii wa nje 24,011 zaidi na wa ndani pungufu kwa 4,108 ikilinganishwa na Idara ya Fedha kati ya mwaka 2015/16 na 2017/18. Idadi ya watalii ilitakiwa kufanana kwa idara zote kwa kuwa ina athari ya moja kwa moja kwenye mapato yaliyorekodiwa,” anasema CAG katika taarifa yake.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1959 kwa lengo la kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za asili za eneo la uhifadhi, kukuza utalii ndani ya eneo la uhifadhi, kutoa na kuhamasisha utoaji wa vifaa muhimu kwa ajili ya kukuza utalii; na kulinda na kukuza masilahi ya Wamaasai wa Tanzania wanaojihusisha na ufugaji ndani ya eneo la uhifadhi.

Vibweka vya TBS

Ukaguzi wa CAG, Profesa Assad, katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) umebaini shirika hilo kukosa viwango katika maeneo kadhaa kiutendaji.

CAG anasema kumekuwa na ukokotoaji usio wa kawaida wa tozo za adhabu na ada ya utambulisho wa makundi ya bidhaa.

 Anasema TBS wametumia thamani za bidhaa tofauti na zile zilizothibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kutoza adhabu ya asilimia 15 kwenye mizigo ambayo haijakaguliwa kwa njia ya utaratibu wa uhakiki wa kukidhi vigezo kabla ya kusafirisha na asilimia 0.2 katika utambulisho wa makundi ya bidhaa.

“Vitendo hivi ni kinyume cha matakwa ya taratibu za ukaguzi wa bidhaa zilizofika kutoka nje,” anasema CAG.

 Kwa mujibu wa CAG, TBS wakati mwingine imekuwa ikitoza asilimia 15 ya adhabu katika mizigo ambayo haijakaguliwa kwa kutumia utaratibu wa uhakiki wa kukidhi vigezo kabla ya kusafirisha kwa bidhaa zinazodhibitiwa tu, badala ya mzigo wote.

Katika hilo, maelezo ya CAG yanaweka bayana kuwa hicho ni kitendo kilicho kinyume cha matakwa ya kifungu cha 5.1.5 (c) cha taratibu za ukaguzi wa bidhaa zilizofika kutoka nje.

Anasema kutokana na kutofautiana huko, shirika limekuwa likipoteza mapato kwa kutumia thamani ndogo zaidi ya zile ambazo zimethibitishwa na TRA.

“Pia, haki inashindwa kutendeka kwa baadhi ya waagizaji wa bidhaa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba misingi tofauti ya tozo imetumika kuadhibu waingizaji tofauti wa mizigo ambayo haijakaguliwa kabla ya kusafirishwa katika bandari ya upakiaji.

CAG amependekeza TBS itumie thamani ya bidhaa iliyothibitishwa na TRA ili kukidhi matakwa ya taratibu za ukaguzi wa bidhaa zilizofika kutoka nje.

Akiwa mkoani Njombe, Rais Magufuli alitaka mawaziri ikibidi ‘wavute bangi kwa siri’ ili kuongeza ukali katika kuwashughulikia watendaji waliobainika kufanya madudu kwenye vyombo vya umma wanavyoviongoza.

 Tanzania imekuwa ikiagiza zaidi vifaa vya usafiri, mitambo, vifaa vya ujenzi, mafuta, mbolea, malighafi za viwandani na bidhaa za vyakula. Sehemu kubwa ya bidhaa hizo ni kutoka China, India, Afrika Kusini, Kenya na Falme za Kirabu (U.A.E).

Madudu ya SUMATRA

CAG pia amebainisha madudu ndani ya Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) katika majukumu yake ya kutoa leseni.

Hapo CAG anasema kuna leseni zenye namba ya kipekee kwa kila chombo cha usafiri kinachohitaji leseni, lakini baada ya ukaguzi na kufanya marejeo ya leseni 165,230 alibaini leseni 20 zilitolewa kwa gari zaidi ya moja.

“Hii inaweza kutoa mianya ya uwezekano wa kufanyika udanganyifu ambao utasababisha serikali ikose mapato,” anasema CAG na kupendekeza SUMATRA irekebishe kasoro zilizojitokeza ili kuondoa uwezekano wa mamlaka kupoteza mapato.

Ukumbi wa Mlimani City

CAG amebaini pia kutosimamiwa kwa mapato kwa mujibu wa mkataba kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mpangishaji wa eneo lake maarufu kama Mlimani City.

Katika hilo amesema hakuna usimamiaji makini wa mapato ya matangazo, kumbi na maegesho kutoka kwa Kampuni ya Mlimani Holding Limited.

“Kifungu namba 10.1 cha mkataba wa upangaji kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kampuni ya Mlimani Holding Ltd (MHL) kinakitaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam au wawakilishi wao kupitia vitabu vya Kampuni ya MHL kwa ajili ya kuthibitisha kiwango cha upangaji wanachotoza kwa wapangaji waliopo ndani ya majengo na huduma za maegesho zitolewazo.

“Kwa kipindi cha mwaka ulioishia Juni 30, 2018 imebainika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakitimizi majukumu yake ya kimkataba kwa kushindwa kupitia viwango vya tozo; hivyo kutegemea taarifa zitolewazo na Kampuni ya MHL,” anasema na kubainisha kuwa dola 10,869.90 na dola 8,204.73 za Marekani ziliwasilishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama kiwango cha gawio la mwaka kutokana na mgawanyo wa hisa katika mapato ya eneo la matangazo na maegesho ya magari.

“Hata hivyo, nimethibitisha kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakijafanya uhakiki wowote kujiridhisha na usahihi wa hesabu za mapato hayo.

 “Pia nilibaini kuwa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakina idadi kamili ya vikao na makongamano yaliyofanyika ndani ya ukumbi wa mikutano wa Mlimani City. Hivyo kutokuwa na uwezo wa kujua kiwango halisi cha mapato yaliyopatikana kutokana na kukodishwa kwa ukumbi huo.

“Kutokana na kushindwa kumsimamia mpangaji, ni dhahiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakiwezi kuthibitisha thamani halisi ya hisa zilizopo na kiwango cha gawio kinachostahili kulipwa,” ameeleza CAG na kupendekeza menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufuatilia suala hilo, ikiwamo ukaguzi wa vitabu ili kupata stahiki zake kwa usahihi kutoka kwenye mradi wa Mlimani City.

Madudu RAHCO

Kampuni Hodhi ya Kusimamia Rasilimali za Shirika la Reli (RAHCO), CAG anasema imefanya uwekezaji wa amana ya Sh bilioni 7.61 na Sh milioni 962 katika Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) na UTT Microfinance, na kwa pamoja uwekezaji huo ulitarajia kuzalisha riba ya Sh milioni 707.9 lakini kiasi hicho cha fedha hakikuweza kuthibitishwa kwenye vitabu vya RAHCO.

Anasema RAHCO haiwezi kurudishiwa kianzio wala riba kutoka UTT au TIB, na kwa msingi huo, vitabu vya RAHCO vitakuwa na nakisi ya kiasi hicho cha fedha za riba ambacho hakijarekodiwa kwenye vitabu vya akaunti na hali hiyo itaathiri ukwasi na shughuli za uendeshaji za RAHCO kutokana na kushindwa kurejesha kiasi kilichowekezwa.

Anapendekeza menejimenti ya RAHCO kufuatilia ili kurejesha fedha hizo zilizowekezwa, na serikali iingilie kati kunusuru hali hiyo.

Lakini kwa upande mwingine, RAHCO haikukusanya mapato ya kodi kutoka kampuni za mawasiliano ilizoingia nazo makubaliano ya kikazi.

“Juni 2010 RAHCO iliingia makubaliano na kampuni tatu za mawasiliano ya simu kwa ajili ya kuweka mitambo ya mawasiliano kando kando ya miundombinu ya reli.

“Mkataba ulioingiwa ulikuwa na thamani ya dola milioni 1.01 za Marekani. Hata hivyo, kiasi cha dola 540,800 ya kiwango hiki hakijapokewa kwa zaidi ya miaka minane sasa mpaka mwishoni mwa mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2018.

“Menejimenti bado haina uhakika kama kiwango hicho cha fedha kitalipwa ama la kutokana na upungufu katika utunzaji kumbukumbu,” anasema CAG.

 Kwa mujibu wa CAG, ni dhahiri kuwa kampuni hizi tatu za simu zinafaidi matumizi ya mali za RAHCO bila kutimiza majukumu yaliyomo kwenye masharti ya mkataba.

“Nina wasiwasi huenda mapato yatokanayo na kampuni hizi za simu yakawa yanalipwa kwenye akaunti ya mtu binafsi, kwani niligundua akaunti tatu ambazo zinamilikiwa na RAHCO, lakini hazikuingizwa kwenye vitabu vya uhasibu vya RAHCO.

“Napendekeza kuwa Menejimenti ya RAHCO ifanye ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha kuwa kiasi cha fedha kilichopaswa kulipwa kinapatikana kutoka kwa wakodishaji,” anasema CAG akionyesha uchochoro wa ufisadi RAHCO.

Please follow and like us:
Pin Share