Mradi mkubwa wa maji unaojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) umeingia lawamani baada ya kampuni inayojenga kuanza kumwaga vifusi vya udongo ndani ya Ziwa Victoria.

Hali hiyo inayodaiwa kusababisha uchafuzi wa mazingira, inalenga kujenga barabara ya udongo ziwani ambayo itarahisisha ufungwaji wa mitambo ya kusambaza maji ya kunywa kwa wananchi.

Taarifa zinabainisha hadi sasa zaidi ya urefu wa mita 400 ndani ya ziwa hilo kubwa kuliko yote barani Afrika zimekwisha kufukiwa na udongo kutoka ukingoni.

Mitambo ya mradi huo inatakiwa kusimikwa majini umbali wa mita 500 kutoka ukingo wa ziwa hilo.

Wataalamu wanaelekeza mitambo hiyo kufungwa chini ndani ya maji kwa kutumia mashine maalumu bila kumwaga udongo juu ya maji kama inavyofanyika sasa.

JAMHURI limebaini umwagwaji wa vifusi hivyo ziwani unasababisha maji kugeuka rangi na kuwa meusi huku mapovu yakitanda juu yake.

Mhandisi Mshauri anayesimamia ujenzi wa kampuni hiyo katika mradi huo,  Baraka Alphayo, ameliambia JAMHURI kwa njia ya simu: “Mradi ulilenga kutumia mashine kusimika mitambo ya kusambaza maji, badala  ya kujenga barabara ya udongo majini. Lakini tukaona ingetumia muda mrefu kuja hiyo mitambo na mradi ungechelewa kuanza.

“Ingetuletea matatizo na hatutaki matatizo. Tukaona tutumie njia hiyo ya kujenga barabara, ingawa ina gharama kubwa  kuliko hizo mashine.”

Mbali na EIB, mradi huo unaojengwa ndani ya Kijiji cha Kalago, Wilaya ya  Busega, Mkoa wa Simiyu unafadhiliwa pia na Agence Francaise de Development (AfD).

Mradi huo unajengwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya zaidi ya Euro milioni 4.8.

Ulipangwa kukamilika mwezi ujao lakini kwa sasa umesogezwa hadi Agosti ndipo utahitimishwa baada ya mkandarasi kuomba kuongezewa muda.

Constantino Kadege, mkazi wa Mji wa Lamadi, Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu analaani umwagwaji huo wa vifusi vya udongo ndani ya Ziwa Victoria.

“Sheria zinakanyagwa,” Kadege amesema huku akiomba mamlaka za juu kuzuia uchafuzi huo wa mazingira.

Amesema tangu ujenzi wa barabara hiyo ya udongo ndani ya Ziwa Victoria, maji ya mwambao wa ziwa hilo yamechafuliwa.

Kwa mujibu wa Kadege, ingawa wanahitaji kupata maji ya kunywa lakini si kwa uchafuzi huo wa mazingira unaofanyika.

“Tuna wasiwasi. Huenda tukapata madhara kiafya kwa kunywa haya maji machafu. Serikali ipo wapi?” anahoji Kadege.

JAMHURI limeshuhudia malori yakisomba na kumwaga vifusi hivyo vya udongo  ziwani humo.

Baada ya vifusi kumwagwa, katapila la ujenzi linaloendeshwa na raia wa Kitanzania, husambaza na kushindilia barabara hiyo.

Barabara hiyo ina upana wa zaidi ya miguu 12 ya mtu mzima, ndani ya ziwa hilo ambalo pia ni chanzo cha Mto Nile.

Sheria isemavyo

Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji nchini namba 11 ya mwaka 2009, sehemu ya 103 inasema kuchafua maji ni kosa la jinai.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, adhabu yake ni faini isiyopungua Sh. milioni moja na isiyozidi Sh milioni 10 au kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004, sehemu ya 55 ya ulinzi na  usimamizi wa mito, mwambao wa mito, maziwa na fukwe, pamoja na mambo mengine, inazuia kuharibu fukwe za bahari au ziwa.

Malalamiko

Salu Maduhu, Emmanuel John na Elizabeth Kayombo, wanataka kuzuiwa kwa ujenzi huo.

“Rais John Magufuli atume watu wake waje wachunguze hii hali. Sina hakika kama wafadhili wa mradi huu wanakubaliana na ujenzi wa namna hii. Naomba Takukuru na waandishi wa habari tusaidieni,” anasema Dotto Kija.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kalago unakojengwa mradi huo, Mpuya Lucas,  hakubaliani na umwagwaji wa vifusi hivyo ziwani.

Amesema anavyojua udongo wowote unakuwa na bakteria wanaosababisha  magonjwa, hivyo ameomba mamlaka zizuie ‘uchafuzi’ huo wa mazingira na maji.

“Udongo wanachimba Kijiji cha Mwasamba, Kata ya Lutubiga. Hata hapa kijijini walianza kuchimba tukawazuia,” amesema Mwenyekiti Lucas.

Gazeti hili limeelezwa kuwa mmoja wa wawekezaji wilayani Busega (jina tunalo), amepewa onyo kutokufuatilia ujenzi huo wa barabara ndani ya Ziwa Victoria.

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Lamadi (Chadema), Bija Laurent, amesema  inashangaza kuona uchafuzi huo wa mazingira unafanyika mbele ya vyombo vya dola.

“Maji tunayahitaji – sawa, lakini yasiwe ya kuumiza tena afya za wananchi wetu. Hii hapana,” amesema Bija aliyehamia CCM wiki iliyopita katika mahojiano na JAMHURI mjini Lamadi.

“Mfadhili wa Kizungu hawezi kukupa fedha za mradi kama huu bila kuonyesha  utatunza vipi mazingira wakati wa ujenzi wake.

“Takukuru wachunguze uhalali wa ujenzi wa barabara hii ya tope ndani ya  Ziwa Victoria,” amesisitiza mwanasiasa huyo.

Madhara

Daktari wa magonjwa ya binadamu, Dk. Dishon Chacha wa jijini Mwanza anasema maji yanapochafuliwa na udongo kuna uwezekano wa kusababisha  madhara kiafya kwa binadamu.

“Kwenye udongo kuna bakteria. Madhara mojawapo mtu anapokunywa maji kama hayo ni kupata minyoo na ugonjwa wa homa ya matumbo (Typhoid). Typhoid inaua,” amesisitiza Dk. Chacha huku akitolea wito jamii kupima afya mara kwa mara.

Typhoid husababishwa na bakteria aitwaye, Salmonella typhi na Salmonella paratyphi, kulingana na taarifa za kidaktari.

Meneja Miradi wa Mamlaka ya Majisafi na taka jijini Mwanza (Mwauwasa) inayosimamia mradi huo, Celestine Mahubi, amekiri kuwapo ujenzi huo wa barabara ya udongo ndani ya Ziwa Victoria ili kupata sehemu ya kusimika mitambo.

“Hakuna teknolojia nyingine inayoweza kutumika kusimika mitambo tofauti na kujenga barabara hii ya molamu. Barabara hizi zinatumika duniani kote, hata Uholanzi wanatumia mfumo huu,” amesema Mahubi.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, alipoulizwa iwapo ujenzi wa barabara hiyo ya udongo ndani ya eneo lake la utawala, una baraka za serikali,  amesema ndiyo.

“Una baraka kutoka NEMC. Hii ni baada ya kukosekana teknolojia ya kuweka mabomba chini ndani ya maji.

“Mradi upo chini ya uangalizi wa Rais (John Magufuli). Ukikamilika  utahudumia kaya 22,000 Lamadi, si Busega yote,” DC Tano amesema.

Ofisa wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria, Jamal Baruti, ameliambia gazeti hili kuwa ujenzi wa barabara hiyo ya udongo ndani ya Ziwa Victoria anaufahamu.

“Ujenzi huu naufahamu vizuri sana,” amesema Baruti kwa kifupi.

Hata hivyo hakuwa tayari kuendelea kuzungumzia malalamiko ya wananchi juu ya ujenzi huo.

Please follow and like us:
Pin Share