Maono humfanya dhaifu awe imara

 

Maono hubebwa katika vitu vitatu muhimu. Mosi, uwezo wa kuona mbele. Pili, uwezo wa  kuona kwa undani. Tatu, uwezo wa kuona nyuma.

Uwezo wa kuona mbele ni sawa na kuona kwa kutumia darubini. Darubini ni chombo  kinachofanya vitu vilivyo mbali vionekane karibu.

Kila mtu na uwezo wa kuona mbali, lakini ni wachache tu wameamua kuutumia uwezo huo. Wengi wanapenda  kujua mambo watakayoyafanya sekunde kadhaa zijazo, dakika zijazo, siku au wiki zinazofuata. Ni  wachache wanaweza kuwa na maono ya miaka mitano, miaka 10, miaka 20 au miaka 100.

Uwezo wa kuona kwa undani unakusaidia kuona vitu kwa kina kabisa. Wakati wengine wanaona vitu vya kawaida, wengine wanaona vitu vikubwa. Kwa mfano, kuna mtu akiona mti, anaona kitanda, meza, viti na kadhalika.

Siku moja mtu alipita katika njia iliyo msituni. Baada ya kutembea kitambo kidogo akakutana na nyoka. Akachukua fimbo na kumuua. Siku  nyingine wakapita watu wawili mahali pale wakakuta nyoka amejilaza njiani wakakimbia na kuhama njia ile, wakapita kwingine.

Baada ya wiki moja kupita, jamaa mmoja akapita katika eneo lile akakutana na kitoto cha nyoka, akakichukua na kuanza kukifuga. Baada ya miaka kadhaa akatengeneza sehemu ya kufugia nyoka wengi. Watalii wakaanza kuzuru maeneo yale. Yule mtu akaanza  kupata pesa nyingi. Huyu aliona fursa ambayo wengine hawakuiona. Alikuwa mtu mwenye maono.

Maono pia huambatana na uwezo wa kuona nyuma. Dereva anayeendesha gari huwa na vioo vya pembeni na kioo kinachomsaidia kuona nyuma. Anaona nyuma ili asigongane na magari mengine yaliyoko nyuma. Ingawa anakwenda mbele, lakini nyuma yake kuna magari yanayoweza kumsababishia ajali. Lazima ayatazame pia. Ukiwa na maono  unahitaji kujifunza kutokana na makosa ya nyuma ili usirudie kuyafanya. Wakati uliopita upo ili kukusaidia kujifunza kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa. “Jana ni wakati uliopita na hatuwezi kuubadilisha,” anasema Eckhart Tolle.

Kuna mtu aliyewahi kusema: “Mtu asiye na maono ni mtu asiye na kesho na mtu asiye na kesho siku zote atarudi kwenye nyakati zilizopita.” Ukikutana na mtu anayesifu nyakati zake nzuri za nyuma ni ishara kwamba mtu huyo hana maono. Utasikia akisimulia mwaka fulani nilikuwa nafanya hivi na vile, sijui mwaka 2016 nilikuwa napata ‘pesa ndefu’, maisha yalikuwa mazuri, watu wa namna hiyo ni watu wasio na maono. Watu hawa wanakosa maono kwa sababu hawajachukua muda kutafakari kuhusu maisha yao ya baadaye.

Tukisikiliza pia midahalo ya kitaifa tunaweza kujua kama nchi yetu ina maono au la, kutokana na yale yanayozungumzwa yakionyesha wakati gani.  Kwenye maisha utavutwa na wakati ujao au uliopita. Ukiona unavutwa sana na wakati uliopita, jua kwamba hauna maono. Pasipo na maono watu huangamia.

Kuna mtu aliwakuta mafundi waashi watatu wakijenga. Kila fundi akipandisha ukuta wake. Alipofika kwa fundi wa kwanza akamuuliza: “Unafanya nini?”

Akajibu: “Ninapanga matofali.” Akamfuata wa pili akamuuliza vilevile; akajibu: “Hauoni ninachokifanya? Ninajenga ukuta.” Wa tatu alipoulizwa akajibu: “Najenga kanisa kwa utukufu wa Mungu.” Wote watatu walitoa majibu, lakini ni majibu yaliyo na uzito tofauti.

Wa kwanza anaona kupanga matofali, atapanga matofali mwishowe atakata tamaa na kuacha. Wa pili atajenga ukuta, mwishowe atajiuliza ukuta huu unakwenda wapi?

Ataacha pia. Wa tatu kwa sababu anaona mwisho ni rahisi kujenga na kumaliza. Watu wenye maono huona mwisho katika hatua za mwanzo.

Maisha ya wengi wetu ni ya kupanga matofali. Unaamka, unasali, unaoga, unakwenda kazini, ukitoka kazini unarudi nyumbani, unalala. Kila siku ratiba ni hiyo hiyo. Mwishowe tunaanza kusema maisha ni magumu. Hakuna anayewaza maisha ya baadaye.

Maono yana sifa zifuatazo: Mosi, maono yatakuchanganya kwa sababu hutabiri mambo yajayo, siku zote utaona ‘changanyikeni’, uhalisia hauonekani. Waisraeli walipewa maono ya nchi ya maziwa na asali wakati wakiwa jangwani kwenye ukame.

Pili, maono yatakutoa katika eneo la faraja. Maono yatakubadilisha, yatakutoa katika uzembe, maono yatamfanya mtu dhaifu awe imara, yatamfanya  anayefuja fedha

kuwa mwekezaji. Maono yatakwambia hapa ulipo si mahali pako. Maono yatalipa changamoto eneo lako la faraja.

Please follow and like us:
Pin Share