NINA NDOTO (19)

Uaminifu unalipa

 

Uaminifu ni tabia ya mtu  kuaminika. Kama watu hawakuamini si rahisi kutimiza ndoto yako. Uaminifu unalipa. Watu wakikuamini ni mojawapo ya hatua kubwa ya kuzifikia ndoto zako.

Uaminifu hujengwa, lazima kuna mambo unatakiwa kuyafanya ili watu waweze kukuamini. Kuwa mwaminifu kwenye kazi unayoifanya, na kuwa mwaminifu kwenye majukumu yako ya kila siku.

Uaminifu  huwafanya watu wafanye kazi na watu wengine. Uaminifu ndiyo huwafanya watu wapandishwe vyeo na hata mishahara kwenye kazi zao. Hakuna asiyependa kusikia mtu fulani ni mwaminifu.

Ikitokea mtu fulani akasema wewe si mwaminifu tayari utakuwa umejijengea sifa mbaya.

Utajuaje kama wewe ni mwaminifu? Kwanza kabisa fikiria watu wanasema nini juu yakomuda ambao haupo. “Chapa yako ni kile watu wanachosema kuhusu wewe wakati haupo,” anasema Jeff Bezos mwanzilishi wa kampuni ya Amazon. Jiulize leo umejenga chapa gani ya uaminifu katika mambo unayoyafanya.

Uaminifu pia huja pale mtu anapofanya zaidi ya matarajio, yaani anapokuwa amezalisha zaidi. Ukiwa kazini fanya zaidi ya inavyotarajiwa, toa matokeo zaidi. Ukiwa umejiajiri, toa huduma zaidi ya ile ambayo wateja wako au watumiaji wa huduma yako wanatarajia.

Hadithi ya talanta ina funzo kubwa sana kwetu kwa uaminifu. Kuna aliyepewa talanta tano, mwingine akapewa mbili na mwingine akapewa moja. Yule wa talanta moja alizalisha nyingine tano, yule wa mbili alizalisha nyingine mbili, na yule wa talanta moja hakuzalisha chochote kama faida isipokuwa talanta aliyopewa na bwana wake.

Kwa sababu watumwa wawili walizalisha talanta zaidi bwana wao aliwapongeza akiwaita “Watumwa wema na waaminifu.” Yule mwingine asiyezalisha chochote aliitwa mbaya na mlegevu. Ukitaka kuaminiwa zalisha zaidi, zalisha kwa viwango.

Tupo katika nyakati ambazo watu wamekwisha waweka watu wa kazi fulani kwamba si waaminifu. Unaweza kubadili kurasa na kuwa mtu mwenye kuaminika na kuwawabadili walivyofikiri juu yako.

Unapozungumza na watu sema ukweli. Unapokuwa mtu wa kusema uongo hakuna atakayekuamini. Ukweli utakuweka huru. Kuna aliyewahi kusema, “Uaminifu unaanza na ukweli na kuisha na ukweli.” Usiseme uongo kujiokoa kwani uongo unaposemwa ukweli huwa upo karibu. Hawakukosea waliosema, njia ya muongo ni fupi.

Nakubaliana na Stephen  Covey aliyewahi kusema, “Uaminifu ni gundi ya maisha. Ni kiungo muhimu kwenye mawasiliano. Ni msingi unaobeba uhusiano wote.”

Kutimiza ahadi, huongeza uaminifu pia, unapotoa ahadi itimize kwa muda husika.

“Tunza ahadi zako na kuwa thabiti. Kuwa mtu ambaye wengine wanaweza kumuamini,” anatukumbusha Roy T. Bennett.

Uaminifu utakusaidia mno kukuza biashara yako. Wauzie watu bidhaa bila kusema uongo kama unamtumia mtu bidhaa mtumie kwa wakati, ahadi ni deni. Naunga mkono hoja ya Zig Ziglar, mhamasishaji na mwandishi wa vitabu aliyesema, “Kama watu wakikupenda watakusikiliza, lakini kama wakikuamini, watafanya biashara na wewe.” Yusufu alikuwa kijana aliyefanya kazi zake kwa uaminifu mkubwa. Uaminifu ulimsaidia kufikia ndoto zake. Kuna wakati mke wa bwana wake (mke wa Potifa mkuu wa majeshi) alimshawishi ili alale naye kwani kijana huyo alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kupendeza.

Yusufu alikataa kulala na mke wa bwana wake. Yule mwanamke akamtengenezea kisa ambacho kilimfanya aonekane alitaka kumbaka. Tunasoma, “Alisubiri wakati ambapo watumishi wake wengine hawakuwepo. Alijua kwamba Yusufu angeingia ndani ili afanye kazi yake. Alipoingia tu, akajaribu kumshawishi. Akashika vazi lake, kwa mara nyingine akamsihi akisema: ‘lala nami!’ Yusufu alitenda haraka. Akamnyang’anya vazi toka mkononi mwake na kuvuta lakini mke wa Potifa akaling’ang’ania. Yusufu akaliacha vazi mikononi mwake akakimbia.” (Mwanzo 39: 11, 12).

Haikuishia hapo, bwana wake alivyosikia habari hiyo mbaya kuhusu Yusufu akaamuru afungwe gerezani.

Maisha yake yakawa kama yamefikia ukomo. Alipofika gerezani akawasaidia watu wawili kutafsiri ndoto zao. Ndoto hizo baadaye zilikuja kuwa kweli. Mmoja wa wale waliotafsiriwa ndoto alimwambia Farao kuhusu Yusufu baada ya Farao kuwa na ndoto ambazo zilikosa mtu wa kuzitafsiri. Hatimaye Yusufu alitafsiri ndoto hizo.

Baada ya kufanya jambo hilo Farao alipendezwa naye na kumfanya kuwa waziri mkuu katika serikali yake. Uaminifu ulimlipa Yusufu.