Nini anatakiwa kukifanya ‘Mo’?

DAR ES SALAAM

Na Andrew Peter

Bilionea na Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Wakurungezi wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji, ameandika katika ukurasa wake wa ‘twiter’: “Tunasafisha kila sehemu ambayo inahitaji kuwekwa sawa ili turudi kwenye ubora wetu #nguvu moja.”

Kauli ya Mo inaendana na ile ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliyesema: “Ni wakati wa kufanya mabadiliko ya kikosi, tunasajili vizuri, tutabaki na wachezaji wazuri, kuna wengine umri umekwenda na viwango vimeshuka, lakini hatutawaacha vibaya. Tunawashukuru wachezaji.”

‘Try Again’ alikwenda mbali kwa kuwaasa viongozi wenzake kuwa makini na kauli zao katika kipindi hiki.

“Ni vizuri kushauri, lakini tutumie njia bora. Kwa nini tulipofanya vizuri nyuma hawakusema? Haipendezi. Wajumbe wa bodi wana nafasi ya kushauri, lakini wanatoka wanakwenda kuzungumza nje. Si jambo jema,” amesema. 

Ukizisikia kauli za viongozi hawa wa Simba, kutimuliwa kwa Kocha Pablo Martin na yanayoendelea nyuma ya pazia ni wazi msimu umemalizika vibaya kwa mabingwa hao mara nne wa Ligi Kuu Tanzania Bara; sasa klabu imeingia katika ligi ya malumbano na kutafuta mchawi.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa Simba ilianza kupoteza ubingwa na kushindwa kutimiza ndoto ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika siku bilionea Mo Dewji alipotangaza kujiondoa katika uongozi wa klabu.

Bila ya kujali kwamba Mo aliweka Sh bilioni 20 au hapana, lakini alikuwa kiungo muhimu katika mafanikio ya klabu kwa miaka minne iliyopita.

Uamuzi wa kujiondoa katika uongozi ulitoa fursa kwa Yanga kujipanga zaidi, pia kama ingekuwa Simba ipo katika masoko ya mitaji na hisa, hakuna shaka mauzo ya hisa zake yangeporomoka vibaya sana msimu huu.

Pamoja na upungufu wake, Mo Dewji alifanikiwa kutengeneza ushawishi kwa wachezaji kujituma zaidi uwanjani, jambo ambalo halikuonekana kwa Simba msimu huu.

Mo si tajiri wa kwanza kuondoka katika klabu na kuiacha timu ikiyumba kiuongozi na kushindwa kufanya vizuri uwanjani. Mifano ipo.

Mfano wa hivi karibuni ni Chelsea baada ya Roman Abramovich kuondoka kufuatia vikwazo vya kiuchumi alivyowekewa na Umoja wa Ulaya kutokana na mgogoro wa Russia, kumeifanya klabu hiyo kumaliza ligi vibaya na kupoteza ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku baadhi ya nyota wakitangaza kuondoka na timu kuwekwa chini ya uangalizi maalumu.

Hata mabingwa watarajiwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga, ilipatwa na pigo kubwa na kupoteza mataji baada ya kuondoka kwa Yusuf Manji, jambo lililowafanya vijana hao wa Jangwani kusubiri kwa miaka minne hadi msimu huu alipoingia GSM.

Pia miamba ya Italia, AC Milan, ilipoteza heshima yake katika soka la Italia na Ulaya kwa ujumla baada ya mmiliki wake, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo, Silvio Berlusconi, kuondoka kutokana na kashfa katika uongozi wake.

AC Milan imesubiri kwa misimu tisa hadi msimu huu kunyakua ubingwa wa kwanza wa Serie A, hiyo yote ni kutokana na msukosuko wa kuondoka ghafla kwa tajiri wao. 

Leicester City ikiwa chini ya bilionea wa Malaysia, Vichai Srivaddhanaprabha, ilitikisa soka la England na kufanikiwa kunyakua ubingwa, lakini tangu alipofariki dunia kwa ajali ya ndege nje ya uwanja, timu imepoteza ubora na kukikimbiwa na nyota kadhaa akiwamo Riyadh Mahrez na N’Golo Kanté.

Tafiti mbalimbali zimebaini sababu zinazofanya timu nyingi kuyumba baada ya kuondokewa na matajiri wake, ni mzigo mkubwa wa madeni, hasa mishahara ya wachezaji iliyokuwa inalipwa na kiongozi wa awali.

Pili, unapobadilisha mmiliki unabadilisha na malengo ya klabu, kwa sababu kila kiongozi anakuja na mbinu tofauti na mitazamo tofauti katika uendeshaji wa timu.

Mbinu alizotumia Mo Dewji akiwa mwenyekiti ni tofauti kabisa na anazotumia Abdallah ‘Try Again’, hasa katika suala la matumizi ya fedha na utawala.

Hivyo kama Dewji ‘Mo’ anataka kuisafisha Simba, sehemu ya kuanza nayo ni kuhakikisha ule mchakato wa kuifanya klabu hiyo kujiendesha kisasa unarudi upya kwa wanachama na kuondoa malalamiko.

0655 413 101