Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, itakuwa na kibarua kizito mbele ya Algeria katika mchezo wake wa pili wa Kundi ‘F’ wa kusaka kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2023, Ivory Coast.

Stars inashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa na rekodi ya kushinda mechi moja miongoni mwa 11 ilizocheza dhidi ya Algeria tangu mwaka 1973, huku ikipata sare nne na kufungwa sita.

Ushindi pekee wa Tanzania ulipatikana mwaka 1995, ikishinda 2-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, huku sare ya mwisho ikiwa mwaka 2015 ya mabao 2-2; magoli ya Elius Magoli na nahodha Mbwana Samatta.

Stars inahitaji kushinda katika mchezo huo wa kwanza nyumbani ili kuweka matumaini yake vizuri ya kufuzu kwa fainali za mwakani kabla ya kwenda Uganda katika mechi yake ya tatu.

Katika mechi hii, safu ya ulinzi ya Stars chini ya kipa Aishi Manula na beki Bakari Mwamnyeto inapaswa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha hawatoi nafasi kwa washambuliaji hatari wa Algeria wakiongozwa na nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez.

Nahodha wa Stars, mshambuliaji wa Royal Antwerp FC, Samatta, atakuwa na jukumu la kuendeleza rekodi yake nzuri ya kuzifumania nyavu dhidi ya Algeria. 

Tanzania inasaka kufuzu kwa mara ya tatu kwa fainali za Afrika baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 nchini Nigeria na 2019 nchini Misri. 

By Jamhuri