Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amefungua mafunzo ya usafirishaji kwa wahudumu wa mabasi ya masafa marefu na Mijini kanda ya Kati yaliyoandaliwa na chuo cha taifa cha usafirishaji (NIT)kwa lengo la kuboresha huduma hiyo kuendana na usasa.

Aidha mafunzo hayo ambayo yamejumuisha jumla ya watoa huduma 70 wa Kanda ya Kati yamefanyika huku kukiwa na uhitaji mkubwa wa mafunzo hayo kwani baadhi yao hawana lugha nzuri kwa abiria na kusababisha baadhi ya kampuni za usafirishaji kufilisika.

Akiongea kwenye ufunguzi wa Mafunzo hayo February 12,2024 jijini hapa, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma ametumia nafasi hiyo kuwata wahudumu hao wa mabasi kujua thamani na umuhimu wa kazi yao .

Amesema kuwepo kwa mafunzo hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia waliowezesha kuwepo kwa Mradi huu wa East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project(EASTRIP) unaofadhiliwa na Benki
ya Dunia ambao ni mkopo wa Serikali.

“Napongeza hatua ya Uongozi wa NIT wanataaluma na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuhakikisha kuwa mafunzo haya yanafanyika katika Mkoa wetu wa Dodoma kwa kanda hii ya Kati mngeweza kuamua yakafanyika mikoa mingine ya kanda hii, kwetu sisi ni heshima kubwa, “amesema

Amesema Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kimepewa jukumu kubwa la kuwaandaa wataalamu waliobobea katika nyanja tano za usafirishaji.

Senyamule amejikita kwenye usafiri wa barabarani na kueleza kuwa NIT imekuwa ikizalisha wataalamu mbalimbali wenye weledi mkubwa huku akishauri chuo hicho kuhakikisha kinatoa mafunzo haya mara kwa mara ili kuwa na wataalamu wenye vigezo vya huduma kwa jamii.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Usalama katika Usafirishaji na Uhandisi wa Mazingira wa NIT, Patrick Makule amesema Mafunzo hayo kuwepo ni mchakato wa muda Marefu na ni muhimu kwa watoa huduma kwani kumekuwepo na malalamiko kwa abiria.

“Tumeona kunauhitaji mkubwa wa kuhakikisha watoa huduma kwenye mabasi wanapatiwa Mafunzo ili wasafiri waweze kufurahia safari zao lakini pia kumaliza malalamiko yanayoendelea ,” amesema

Naye Afisa Mfawidhi Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA) Mkoa wa Dodoma Ezekiel Emanuel amesema Mafunzo hayo yataleta mapinduzi chanya kwenye sekta ya usafirishaji .

Amesema Mamlaka ya usafiri na usafirishaji Tanzania Latra wamekuwa na jukumu la kutatua migogoro wakipokea malalamiko kutoka kwa wapokea huduma ambao ni abiria.

” Watoa huduma kwenye mabasi ya Masafa Marefu wamekuwa wakitoa huduma iliyo chini ya kiwango na hiyo yote ni kutokana na kutokuwa na elimu sahihi ya huduma kwa mteja, hivyo niwaombe wamiliki wa magari ya usafirishaji wajitahidi kuwapeleka watoa huduma kupata Mafunzo ya huduma kwa wateja kwani kwakufanya hivyo itawasaidia kwenye biashara zao, ” amesema.

Naye Mkuu wa Kitivo cha mafunzo ya lojistiki na biashara Dkt Prosper Nyaki amesema
Kozi hii ya muda mfupi itawajengea washiriki uwezo na umahiri katika kuzitambua Sheria za LATRA na Kanuni zake ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma bora kwa mteja, mbinu za utoaji wa huduma ya kwanza na usalama wa abiria na mali zao.

“Mafunzo haya yatasaidia pia utunzaji wa mizigo na utambuzi wa bidhaa hatarishi kwa kuzingatia kanuni za usafirishaji, namna bora ya kushughulikia malalamiko ya mteja, usafi na utunzaji wa mazingira, mahusiano na mawasiliano, nidhamu na unadhifu wa mtoa huduma, pamoja na maarifa ya utoaji na umuhimu wa tiketi mtandao, “amefafanua

Amesema Mafunzo hayo ni endelevu na yatakua yakiendeshwa katika Kampasi ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji iliyopo Mabibo jijini Dar es Salaam kwa muda wa wiki mbili na gharama nafuu kwa kila mshiriki (kalenda ya mafunzo hayo pamoja na gharama inapatikana katika tovuti ya Chuo ambayo ni www.nit.ac.tz).

“Chuo kipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za mashirikiano na VETA ambapo kupitia mashirikiano hayo Chuo kitasogeza huduma zaidi kwa wadau kupitia kampasi za Vyuo vya VETA ambavyo vipo katika kanda zote za Tanzania, ” amesema na kuongeza;

“Kama tulivyobainisha katika tangazo la udahili, washiriki wote hawa wapatao 70 katika kanda hii ya Kati wamefadhiliwa na mradi ujulikanao kama East Africa Skills for Transformation and Regional
Integration Project (EASTRIP) unaoendeshwa na NIT,Mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unatekelezwa Tanzania, Kenya na Ethiopia ili kuwezesha muingiliano wa
kijamii katika nchi za ukanda wa Afrika, ” amesema.

Aidha amesema katika kufikia malengo ya Mradi, Chuo kina majukumu ya Kuandaa Mitaala inayokidhi matakwa ya soko la ajira, kuongeza ushirikiano na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi kwa kuwa na mikataba ya ushirikiano , Kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ,Kuzifikia Taasisi zingine ambazo ziko nje ya mradi na kutoa mafunzo ,Kuwajengea uwezo
watumishi katika nyanja mbalimbali ndani na nje ya nchi.