Kuna wakati Watanzania kadhaa walikuwa wakinung’unikia vyombo vya habari vya kimataifa kwa kuona Tanzania haitajwitajwi kwenye vyombo hivyo. Wapo walioona kutotajwa huko ni jambo baya, lakini wapo walioamini hiyo ni dalili njema.

Walioamini hiyo ni dalili njema, waliamini hivyo kwa sababu wanaamini, na kwa kweli ndivyo ilivyo, kuwa ukitangazwa kwenye vyombo hivyo maana yake kuna mambo mabaya ambayo kwao ni habari.

Habari za Afrika ni zile zinazohusu maradhi, vita, migongano, umaskini, mauaji kama ya albino na vurugu ya aina nyingine ya mambo mabaya mabaya.

Kwa hiyo, kutotajwatajwa kwa Tanzania kwenye vyombo hivyo maana yake hatuna ‘mambo mbaya’ ambayo ingekuwa sababu ya sisi kuandikwa na kutangazwa!

Haikushangaza kuona baadhi yetu wakitamani Tanzania ijulikane, si kwa uzuri wake wa vivutio vya utalii na mambo mengine mazuri, bali kwa lolote linaloweza ‘kutupaisha’.

Zamani tulivuma kwa sababu ya msimamo wetu hasa katika kupinga aina zote za dhuluma na ubaguzi. Msimamo wa Tanzania ulivuma ndani na nje ya Afrika, hata kuyatetemesha mataifa makubwa.

Kwenye awamu hii, mvumo wa Tanzania umerejea kwenye vyombo vya habari vya kimataifa. Majarida makubwa kama Wall Street Journal na The Economist, hayakosi kuwa na habari zinazoihusu Tanzania. Kama ilivyotarajiwa, habari nyingi si za kusifu juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo, bali kutazama dosari kadhaa na kuamua kuzitumia kama rejea yao.

Haya yanayosemwa na kuandikwa na vyombo vya habari vya Magharibi kwa kushirikiana na mawakala wao wa ndani na nje ya Tanzania, yanatokea kwa sababu kuna mambo yanafanyika.

Tunasemwa kuhusu suala la demokrasia. Tunasemwa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari; na kwa jumla tunasemwa kwa mambo kadha wa kadha ambayo kwa mtazamo wa kimagharibi hayafai.

Rais Magufuli na wasaidizi wake si malaika. Yawezekana kukawapo kasoro kwa sababu ni binadamu. Hata hivyo, dosari hizo zisitufanye tukafumba macho na kushindwa kuyaona na kuyatambua mengi mazuri yanayofanywa na Serikali katika kuhakikisha tunakuwa na Tanzania mpya.

Kuna imani kuwa ukiona nchi inasifiwa na nchi za Magharibi, basi hapo kuna tatizo. Kusifiwa na hao maana yake ni lazima uwe unatekeleza matakwa yao. Hata kiongozi wa Afrika akiwa anaua watu, alimradi akiwa kibaraka wa Magharibi hawezi kusemwa.

Lakini nchi ikiwa na kiongozi anayewatumikia wananchi wake kama alivyokuwa Muammar Gaddafi, hata kama angekuwa na mema ya aina gani, vyombo vya Magharibi vitatumika kuwaaminisha walimwengu kuwa hafai.

Mataifa ya Magharibi hayajawahi kuwa na uungwana wa kusifu mazuri ya nchi changa. Yanapomsifu kiongozi wa nchi kama Tanzania, sisi wananchi tunapaswa kushituka. Tunapaswa kushituka kwa sababu hadi asifiwe maana yake kuna mambo amewafurahisha. Huwezi kuwafurahisha Wazungu kwa kuwatumikia vema wananchi wako. Kiongozi wa Afrika atasifiwa na Wazungu kwa sababu anatekeleza matakwa yao. Mara zote ukisikia Wazungu wakimsifu kiongozi wa Afrika ujue kuna kitu wanapata kutoka kwake.

Tulisikia namna walivyosifu sera na sheria za uwekezaji kwenye madini. Walitupamba kwa maneno matamu ya kila aina. Tukapewa mialiko na tukapigiwa mfano kwingineko duniani kama taifa lililofanya vizuri kwenye sekta ya madini.

Lakini katikati ya hilo lindi la sifa, wakawapo Watanzania na walimwengu wengine waungwana. Wakatuhadharisha kwa kutuambia kuwa tunaibiwa kwani tunachokipata ni kidogo mno kuliko kile kinachopelekwa kwao.

Amekuja Rais Magufuli. Kaamua kuvunjavunja mirija ya unyonyaji. Tayari ameonekana mbaya. Magazeti makubwa duniani yanamwandama.

Wakati fulani Rais Magufuli amepata kusema, “Ukisifiwa na adui ni lazima uchunguze umekosea wapi, lakini ukisemwa na adui ujue umemtwanga.” Sijui alikuwa akimaanisha maadui gani, lakini bila shaka kauli yake hii ni mtambuka. Yawezekana inawagusa hadi hao waliozoea kupora rasilimali za nchi yetu.

Rais Magufuli ameshika uongozi tukiwa katika hali mbaya. Maendeleo ya nchi yaliyozungumzwa na kuonekana ni ya mtu mmoja mmoja. Hayakuwa maendeleo ya nchi kwa manufaa ya wananchi wote.

Sawa, tulikuwa na zahanati, vituo vya afya na hospitali. Tusijadili suala la dawa na vifaa tiba. Tujadili jambo dogo tu, lakini muhimu – la namna wagonjwa walivyopokewa na kuhudumiwa. Hali ilikuwa mbaya mno. Kuugua kulionekana kosa la jinai! Mgonjwa au mjamzito alikumbana na kadhia ya matusi na lugha zisizo za staha. Tumeona Serikali ilivyojitahidi kukabiliana nalo. Upatikanaji dawa na vifaa tiba nalo ni eneo jingine ambalo Serikali inajitahidi kuliboresha japo bado kuna mkwamo unaosababishwa na tabia za mazoea za wizi na udanganyifu.

Ofisi za umma hazikuwa ofisi za umma tena, bali za watu binafsi waliokuwa na uwezo wa kutenda kadiri walivyotaka. Wananchi wa kawaida hawakuheshimiwa. Leo tunaona mabadiliko makubwa japo bado vijitabia vibaya vipo kwa baadhi ya watumishi.

Nchi haiwezi kusema inapiga hatua ya maendeleo kama kinachoangaliwa ni uwezo na hali nzuri ya watu au tabaka fulani. Tulishaona wanufaika wakuu walikuwa ni wanasiasa, viongozi wa umma, baadhi ya wafanyabiashara na watu wenye ushawishi katika jamii.

Miradi, au huduma zinazogusa jamii ndilo jambo la maana kwenye ustawi wa jamii yoyote. Hapa ndipo tunapoona kazi kubwa inayofanywa ya ujenzi wa reli ya kisasa, ufufuaji wa Shirika la Ndege, ujenzi wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Stigler Gouge, mradi wa bomba la mafuta, ujenzi wa meli katika maziwa makubwa nchini, ujenzi wa vivuko, ujenzi wa barabara, huduma za maji, usambazaji umeme vijijini na mambo mengine makubwa makubwa.

Tunaona udhibiti wa rasilimali za nchi tukilenga kuona zinawanufaisha wananchi wote. Sheria za madini zimebadilishwa ili wachimbaji wakubwa walipe kodi na ushuru mwingine, kwa lengo la kuleta tija kwenye uchumi wa nchi na wananchi.

Biashara ya madini ni ya matajiri wakubwa duniani. Si biashara ya maskini. Hao wameguswa. Wamewaka. Hawakutarajia kuona Afrika ya leo kuwapo kiongozi wa kusimama kupinga hadharani na kwa vitendo unyonyaji wao.

Wazungu wanajua walivyoiacha Tanganyika (Tanzania) ikiwa haina kitu, lakini leo inapiga hatua kubwa kwenye nyanja zote. Mzungu gani atafurahi kuona tukijenga barabara zetu wenyewe? Nani atafurahi kuona tukigoma kuwaomba na badala yake tukijenga reli kwa fedha zetu wenyewe? Nani watafurahi kuona tukiwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya viwanda? Mzungu gani atakayependa kuona tukiachana na mitumba kwa kujenga viwanda vyetu vya nguo?

Wazungu gani watampenda Magufuli kwa kuona akiifanya Tanzania kuwa nchi inayojitegemea? Nani watamshangilia huko Ulaya na Marekani kwa kuona anafanya mambo mengi ya kimaendeleo bila ridhaa yao? Bwana gani anaweza kufurahi kumwona mtumwa wake akiwa huru? Hayupo. Ukiyajua haya huwezi kustaajabu kusoma matusi dhidi ya Rais Magufuli kwenye magazeti na majarida ya nje.

Kuyasema haya si kwamba hatuna kasoro kwenye mwenendo wetu. Kasoro zipo, lakini si kwa kiwango ambacho mabepari wanataka kuuaminisha ulimwengu.

Hivi karibuni, Madaraka Nyerere, kwenye safu yake ya ‘Ujumbe Toka Muhunda’, aliandika maneno haya, “Tukubali pia kuwa watu kama Trump wanapata mwanya wa kudhihirisha hulka yao ya kibaguzi kwa sababu ni kweli kuwa Afrika inaandamwa na matatizo ya kila aina, mengine ya kujitakia, mengine yanayosababishwa na wengine.

Pamoja na utajiri mkubwa wa maliasili wa Bara la Afrika, utajiri huu unaishia mikononi mwa Waafrika wachache na kunufaisha zaidi nchi tajiri ambazo viongozi wake, kama Trump, tunawapa sauti ya kututukana. Usimamizi mbovu wa maliasili unaochochewa na ufisadi wa sehemu kubwa ya viongozi wa Afrika, unasababisha Waafrika kubaki fukara, na kuwa sababu mojawapo inayokuza wimbi la Waafrika wanaokimbia nchi zao kwenda Ulaya na Marekani kusaka nafuu ya maisha.

Inakadiriwa kuwa mwaka 2017 kati ya wahamiaji milioni 258 wa dunia nzima, idadi ya wahamiaji kutoka Afrika ilifikia milioni 36. Mwaka huo huo Marekani ilikuwa na wahamiaji milioni 50, ikiongoza ulimwenguni kama nchi inayokaliwa na wahamiaji wengi zaidi.

Tutaendelea kunyanyaswa, kutukanwa, na kudhalilishwa mpaka tutakapoweza kusimamia masuala yetu na kuhakikisha kuwa matatizo yanayowasukuma Waafrika kukimbia nchi zao na kuomba kuishi Ulaya na Marekani, yanapunguzwa au kumalizwa kabisa.

Wabaguzi kama Trump wapo na hawataisha, na wanaendelea kuzaliwa kila siku. Hilo hatuwezi kulibadilisha, lakini jambo ambalo tunaweza kulifanyia kazi ni kubadilishwa kwa fikra zetu.

Kwanza, kubadilisha mawazo ya kujihisi wanyonge, tunaoonewa, na kudhalilishwa wakati wote tukiamini kuwa hatuna uwezo wowote wa kuboresha hali yetu sisi wenyewe. Afrika siyo maskini. Bara Afrika ni tajiri kwa watu na rasilimali.

Mwaka 2012 nchi zinazoendelea zilipokea jumla ya dola trilioni 1.3 za Marekani za misaada kutoka nchi zilizoendelea. Hii thamani inajumuisha misaada, thamani ya miradi ya uwekezaji, na mapato mengine. Mwaka huo huo nchi zinazoendelea zilihamisha thamani ya bidhaa ya dola trilioni 3.3 za Marekani kupeleka nchi zilizoendelea.

Thamani ya utajiri uliohamishwa kutoka nchi zinazofananishwa na choo ilikuwa ni dola trilioni 3.3. Hatupaswi kujisikia wanyonge, tunapaswa kukubali kuwa sisi ni wajinga.

Ujinga huu unanifikisha kwenye suala la pili la kutafakari. Waafrika tunapaswa kuchukua hatua gani kuziba mianya ya huu utajiri unaohamishwa holela kwenda nje na kuwapa watu nafasi ya kututukana?

Naamini tunahitaji mtazamo mbadala kuondoa ule wa kusifia uwekezaji kama suala la kutuletea ajira, teknolojia na uzoefu. Uzoefu ndiyo, lakini siyo uzoefu tunaoambiwa; huu ni uzoefu wa kupewa dola trilioni 1.3 na kutoa dola trilioni 3.3. Tunachohitaji ni kujijengea uzoefu wa kuongeza utajiri tunaobaki nao mkononi.

Kujiongezea utajiri kuna maana ya kuwapunguzia utajiri wale ambao wananufaika na rasilimali iliyopo. Na hili linahitaji nchi za Afrika kuongeza ushirikiano miongoni mwao katika maeneo ya uchumi, miundombinu, mawasiliano na siasa, ili kuweza kuhimili mfumo uliopo unaokoleza umaskini na unyonge wetu wa kifikra. Umoja utaongeza sauti ya Waafrika kutetea maslahi yao na kuruhusu kasi kubwa zaidi ya maendeleo ambayo, miaka 60 baada ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika, bado haijafikia hatua ya kuridhisha.

Kwa anayoyafanya Rais Magufuli, tusitarajie kusikia akisifiwa na manabii wa ubepari ndani ya Tanzania na hasa hasa katika mataifa ya Magharibi.

By Jamhuri