Hivi karibuni Rais John Magufuli kwa uwezo aliopewa na Katiba ya nchi aliwasikiliza wafungwa waliomo gerezani Butimba, Mwanza na kubaini kwamba wapo walioonewa na kuwekwa gerezani kwa njia za ukatili tu kama kukomolewa. Akaamuru waondolewe.

Hiyo ni hali ya utu ya kuwajali watu aliyonayo rais wetu. Wananchi wanaliona hilo kama njia bora ya kuwajali watu wake, wanapaswa wamshukuru na kumpenda rais wao. Mtu kakomolewa kwa kuwekwa gerezani, lakini kiongozi wake mkuu anamfuata kulekule na kumsikiliza kisha kumpa haki yake ambayo hakuweza kuipata hata kwenye vyombo vya sheria!

Pamoja na kulipongeza hilo, naomba nimweleze Rais Magufuli kwamba hali hiyo haiko magerezani tu. Wapo wengine walionyimwa haki kwa namna ile ile hata kama watu hao hawakupelekwa gerezani. Wametendewa kinyume kabisa cha haki. Wanatesekea uraiani tu wakiwa kama walio kwenye kifungo cha nyumbani.

Wapo watu waliosimamishwa kazi na wengine kuondolewa kwenye utumishi na kubaki hawana utumishi wowote kwa umma. Huo ni uonevu wa moja kwa moja.

Hata kama hawa wako nje ya gereza, nafsi zao zinawauma sana bila kutofautiana na wale walio gerezani kwa kusingiziwa. Mtu anapoona anaachishwa nafasi yake ya utumishi wa umma bila kuonyeshwa kasoro yake, inauma sawa na mtu aliyepigwa risasi ya moto.

Kinachosababisha hali hiyo itokee ni kitu kipana. Kuna kuoneana wivu kwamba fulani kajinufaisha na nafasi yake kwa hiyo yanaundwa majungu kumharibia.

Naamini kwa uwezo alionao Rais Magufuli, anaweza pia kuliangalia hilo katika kulinusuru taifa na tabia hiyo chafu ya ‘bora tukose wote.’ Atakuwa amewaondolea watumishi wa umma tabu inayozitesa nafsi zao kama alivyofanya kwa wale walionewa na kuswekwa gerezani bila makosa.

Hatuwezi kujenga taifa lenye nguvu kwa njia za kufanyiana hila, vinyongo, husuda, wivu na kukomoana; huku tukiwa tumetanguliza hisia tu. Hayo yote yanaliyumbisha taifa na kulisababishia mambo ambayo siyo endelevu, na hata kama yakiwa endelevu, basi yanaelekea kwenye maangamizi.

Nampongeza Rais Magufuli kwa kuliona tatizo hilo la kuwaweka watu gerezani kwa kuwasingizia kama mojawapo ya njia ya kuwakomoa. Na mimi naona rais asingeishia hapo, kwa maana ya kuwaweka huru watu hao kama kuwarudishia haki zao, bali ingetafutwa vilevile tiba na kinga ya tatizo hilo.

Katika kulifanya tatizo lisijirudierudie wangetafutwa watu wanaosababisha tatizo hilo ili wakawajibishwe kwa kulingana na uhalifu waliofanya. Kumweka mtu kifungoni kwa kumuonea tu si jambo dogo. Yeyote anayekuwa amehusika inabidi afuatiliwe kwa umakini ili aeleze ni kwa nini alifanya hivyo.

Baada ya hao wa magerezani ndipo waangaliwe watu wanaoonewa kwa kusitishiwa nafasi zao za utumishi. Kama nilivyosema, taifa haliwezi kujengwa kwa mtindo huo likawa endelevu na lililonyooka. Ni lazima litayumbayumba.

Kote duniani kunaonyesha kwamba haki ikitoweka mambo yanapindapinda na kuwa tenge kama ilivyotokea Marekani na Afrika Kusini.

Kwa hiyo, kama ambavyo rais wetu anajinasibu mara kwa mara kwamba yeye ni mtu wa haki, ningemshauri aonyeshe moyo huo kwenye maeneo yote ya utawala wake. Haki ikitanda kila sehemu, kwa kila mtu kuona katendewa haki, maendeleo ni jambo ambalo halitafutwi tena kwa tochi ila kujionyesha lenyewe peupe.

Kwa hiyo wote ambao wametendewa sivyo –  wameonewa wakiwa katika utumishi wa umma wanapaswa waangaliwe na ikibidi warudishiwe haki zao kama walivyoangaliwa walio magerezani. Rais kama ni kusimamia haki anapaswa aisimamie bila kujali huyu kakaa vipi wala yule kakaa vipi. Ni haki kwa wote, kama ambavyo maendeleo yanatakiwa yawe kwa wananchi wote.

Yamekuwapo manung’uniko miongoni mwa wananchi kuhusu kufanyiwa fitina na kuwasababisha kuwa nje ya utumishi wa umma. Ni jambo ambalo ningemuomba Rais Magufuli ahakikishe watu hao wanatendewa haki.

Kama ambavyo rais anahamasisha watu kufanya kazi kwa kujituma wakiwa wametanguliza uzalendo, katika hali ya kuoneana kwa vinyongo, wivu, chuki binafsi na kadhalika, inakuwa vigumu mtu kuonyesha moyo wa uzalendo akiwa anakabiliwa na mzigo huo wa kuonewa.

Tunaweza kuona kuwa yote hayo yana lengo la kutaka kukwamishana, zaidi kumkwamisha rais ambaye amekusudia kulipeleka mbele taifa.

Namuomba rais kulitupia jicho jambo hilo kwa wepesi. Wahaya wana usemi kwamba: “Atakwenda akwokeza omulubabi.”  Maana yake ni kwamba asiyekupenda anakubabua kwa jani la mgomba; yaani anawasha moto na kuchukua jani la mgomba kuelekeza ulipokaa wewe halafu anajifanya kutimiza mambo yake mengine, kumbe moto wote unakuja kwako. Usipoijua mbinu hiyo utashitukia umeungua.

Rais Magufuli asikubali watu wasiomtakia mema wamuunguze kwa jani la mgomba.

prudencekarugendo@yahoo.com

 0784 989 512 / 0654 031 701

5670 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!