BENKI ya NMB, imezindua rasmi Programu ya Muda wa Kati (Multicurrency Medium Term Note – MTN) yenye thamani ya Sh Trilioni moja, pamoja na kufungua Dirisha la Uwekezaji wa Toleo la Kwanza la Hati Fungani ya Jamii (NMB Jamii Bond).

Katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu alisema Serikali inajivunia bunifu za viwango vya NMB, huku Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama, akiitaja Hati Fungani hiyo kuwa ya kwanza kwa ukubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema benki yake inaanza kuiuza rasmi Jamii Bond kote nchini kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba 27 mwaka huu, na baada ya hapo itapatikana katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kwa wanunuzi watakaoikosa katika kipindi hicho.

“NMB Jamii Bond ni ya kipindi cha miaka mitatu, hadi Novemba 2026, ambako wawekezaji wake watapata riba ya asilimia 9.5 kwa mwaka na italipwa kwa vipindi vinne kwa mwaka. Kiasi cha chini ni Shilingi 500,000 na mnunuzi atapaswa kujaza fomu matawini na kwa Mawakala wa DSE waliopewa kibali na CMSA

“Wanunuzi wa Hati Fungani hii ni watu wote, binafsi, mashirika, makampuni, lengo ni kukusanya Sh. Bilioni 75, lakini CMSA imeturuhusu kufanya ongezeko (green shoe option) la Shilingi Bilioni 25, kwa hiyo tunaweza kwenda hadi Shilingi Bilioni 100.

“Tumeruhusiwa na CMSA kuuza Hati Fungani hii kwa shilingi za Kitanzania, lakini pia kwa Dola za Kimarekani, ambako tumepewa idhini ya mauzo ya Dola Milioni 10 na ongezeko la Dola milioni tano, hivyo kufanya mauzo ya Dola kuwa yanayoweza kufikia Milioni 15.

“Fedha zitakazopatikana zitatumika kutoa mikopo inayolenga matokeo chanya na endelevu katika jamii, ikiwemo kwa ajili ya miradi ya nishati mbadala, miradi ya kuzuia na udhibiti wa uchafuzi mazingira, usimamizi wa maji safi na maji taka na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Pia itakuwa ni kwa ajili ya mikopo ya kuwawezesha wanawake na usawa wa kijinsia, ya nyumba nafuu, usalama wa chakula, huduma za afya, elimu, vijana,” alibainisha Bi. Zaipuna huku akizishukuru taasisi zote zilizoshirikiana nao, zikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), CMSA, DSE, ABSA Tanzania ambayo ni Mshauri Mwenza.

Kwa upande wake, Mkama aliishukuru Ofisi ya Msajili Hazina kwa kuzijengea taasisi za fedha mazingira wezeshi katika kukuza uchumi, huku akisema kuwa mnamo Agosti 31 mwaka huu, CMSA ilitoa idhini kwa NMB kutoa Hati Fungani hiyo ambayo ni sehemu ya Programu ya Muda wa Kati yenye thamani ya Sh Trilioni 1.

“CMSA ni Taaassi ya Serikali yenye jukumu la kuhakikisha Hati Fungani zinazotolewa zinakidhi matakwa na vigezo vya kisheria, ambapo mnamo Agosti 31, tulitoa idhini kwa NMB kutoa Jamii Bond, ambayo fedha zitakazopatikana zitaelekezwa katika miradi mbalimbaili ya kijamii kwa ustawi wa umma.

“Leo Septemba 25 tunaiambia dunia kuwa NMB imekidhi matakwa ya kisheria kwa mujibu wa CMSA, Jumuiya za Kimataifa kiasi cha kupewa idhini ya kuiingiza sokoni Jamii Bond.

“Historia inaandikwa leo, NMB imekuja na bidhaa ya hadhi ya juu, hatujawahi kuwa na Hati Fungani ya thamani kubwa kiasi kisi hiki, hii ni rekodi, sio tu kwa Tanzania na Afrika mashariki, bali ni kubwa zaidi kuwahi kutolewa na taasisi yoyote iliyopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Naye Mchechu, aliwashukuru washirika wa mchakato huo, hususani wasimamizi BoT, CMSA na DSE kwa walichofanya kufanikisha jambo kubwa na la kihistoria kutokea katika Sekta ya Fedha nchini, ambacho ni kitu cha kujivunia na kujipongeza.

“Kazi nzuri inayofanywa na NMB, inaipa Ofisi ya Msajili heshima tukiwa ndio wasimamizi wa Sekta ya Fedha. Sisi kama Serikali tunafurahia sana uwekezaji wetu ulioko NMB, tunajivunia na ndio ‘model’ ambayo tutaitumia na kuiingiza katika Taasisi na Mashirika yetu, kwa sababu tumeiona faida yake.

“Ni jambo jema sana soko linapochagizwa na viongozi imara na wabunifu kama waliopo NMB, kwa kuwa viongozi waliolala wanalinyonya soko. Ukiwa na benki kubwa kama hii, bunifu zinazoona mbali ndio jambo la kujivunia, hakika mmethubutu kuthibitisha uimara kwa kuzindua ‘bond’ ya Trilioni 1.

“Menejimenti na Wafanyakazi, chini ya Bodi ya Wakurugenzi, mnazitendea haki nafasi zenu, hasa ukizingatia tuna mazingira sahihi, rafiki na ya kweli kukuza ustawi wa Sekta ya Fedha yaliyowekwa na uongozi wa Rais Samia Hassan Suluhu, ambaye amedhamiria kuleta mageuzi chanya katika sekta hii.