Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Benki ya NMB mwishoni mwa wiki ilikabidhi madawati, viti na meza zenye thamani ya shilingi milioni 41.2 kwa shule sita zilizopo wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya benki hiyo wa muda mrefu ya kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu.

Shule zilizonufaika na msaada huo ni pamoja na Shule ya Msingi Juhudi iliyopokea meza 100 na madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10, Shule ya Msingi Juhudi Jeshini iliyopokea madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10, Shule ya Msingi Amani iliyopokea madawati 60 yenye thamani ya shilingi milioni 6.

Pia shule ya Msingi Jaica iliyopo Mzambarauni ambayo ilipokea madawati 42 yenye thamani ya shilingi milioni 4.2, Shule ya Msingi Zavalla iliyopokea meza 25 na viti 25 vyenye thamani ya shilingi milioni 6 na Shule ya Msingi Umoja iliyopokea madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Juhudi, Seka Urio Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam alisema kitendo hicho kinaendana na mkakati wa benki hiyo wa kuchangia maendeleo hasa kwa jaamii ambapo benki hiyo inafanya kazi zake.

“Sisi kama benki ya NMB tumejitolea kweli kuunga mkono mipango mbalimbali ya maendeleo nchini kote. Ili kuthibitisha tena dhamira yetu, tumetenga shilingi bilioni 6.2 mwaka huu ambazo zitatumika kuchangia maendeleo ya jamii yaani CSR kote nchini katika sekta zetu za kipaumbele ikiwa ni pamoja na elimu, afya na dharura,” alisema.

Urio alibainisha kuwa madawati yaliyotolewa na benki hiyo yanalenga kuweka mazingira mazuri ya kujisomea kwa wanafunzi wa shule tano za wilaya ya Ilala.

“Leo, tunakabidhi madawati, viti na meza zenye thamani shilingi milioni 41.2 ili kupunguza upungufu wa madawati na kuhakikisha wanafunzi wanajifunza katika mazingira mazuri na rafiki. Ninaomba shule zinazonufaika zitumie vitu vilivyotolewa kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema.

Awali,Neema Msolo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Juhudi katika hotuba yake iliyosomwa wakati wa makabidhiano hayo alibainisha kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kwani shule yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu mkubwa wa madawati.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema mchango wa benki hiyo unadhihirisha uhusiano mzuri na wenye afya kati ya serikali na sekta binafsi.

Mpongolo alisema serikali yake inatambua kuwa elimu ni chachu ya maendeleo ndiyo maana imekuwa ikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu na kuipongeza benki hiyo kwa kuendelea kusaidia kuchangia mipango mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na Serikali huku akiongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dk Samia Suluhu Hassan amejipanga kuendelea kufanya kazi kwa karibu sana na sekta binafsi.

“Ili kikuza sekta ya elimu, Serikali tayari imeweka miundombinu wezeshi ya majengo, inatia moyo kuona wadau wa maendeleo kama baenki ya NMB wamajitokeza kuunga mkono juhudi zetu kwa kuchangia madawati,” amesema Mpongolo.

 Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, (kulia waliokaa), akizungumza na mmoja wa wanafunzi walionufaika na msaada wa meza, viti, na madawati vilivyotolewa na Benki ya NMB kwa shule 5 za Manisapaa ya Ilala jijini Dar es Salaam Aprili 15, 2023, vikiwa na thamani ya shilingi milioni 41.2. Kutoka kushoto ni Meneja wa NMB Tawi la Gongolamboto, Demetrius Kugesha, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Seka Urio. (Na Mpiga Picha Wetu).
Please follow and like us:
Pin Share