Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani

Benki ya NMB imekabidhi msaada wa viti 100 na meza 100 vyenye thamani ya Sh. Mil. 15, kwa matumizi ya wanafunzi wa Shule za Sekondari Kidawendui na Jibondo, zilizoko Mafia mkoani Pwani, vifaa vilivyopokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Zephania Sumaye, kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa benki hiyo, Benedicto Baragomwa.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika viwanja vya Shule ya Kidawendui (zamani ikiitwa Ndagoni Sekondari), ambako DC Zephania aliipongeza NMB na kuitaja kama moja ya silaha za Serikali katika vita ya kupambana na maadui watatu waliotajwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambao ni Ujinga, Maradhi na Umaskini.

Akizungumza katika hafla hiyo, DC Zephania alisema NMB imeisaidia pakubwa Serikali, katika vita dhidi ya maadui hao, kupitia Program ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika Sekta za Elimu na Afya, ilikojikita kutatua changamoto mbalimbali za kimiundombinu, vifaa vya kujifunzia, vya kufundishia pamoja na vifaa tiba katika shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali.

“Wakati wa uhai wake, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwataja maadui watatu wa maendeleo ya Watanzania kuwa ni Ujinga, Maradhi na Umaskini, na sasa hivi NMB imekuwa mdau, mbia sahihi na silaha yetu kuu katika kutusaidia kupambana na maadui hao.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye (kushoto) na Mkaguzi Mkiu wa ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa (kulia) wakikagua madawati na viti vilivyotolewa na Benki ya NMB kwa Shule ya Sekondari ya Kidawendui na Jibondo zilizoko wilayani Mafia mkoani Pwani wakati wa hafla ya makabidhiano . Jumla ya vitu hivyo vina thamani ya shilingi milioni 15

“Kupitia sera ya Uwajibikaji kwa Jamii, NMB inatumia sehemu ya faida yao kila mwaka kusaidia jitihada za Serikali kupambana na maadui hao kupitia misaada yao hii katika elimu na afya, kwani kuboresha mazingira ya walimu kusomesha kirahisi na kutatua kero za kujifunzia miongoni mwa wanafunzi, nako ni kupambana na ujinga.

“Kwenye afya nako NMB imejikita kusaidia maboresho ya miundombinu ya zahanati zetu, Vituo vya Afya na Hospitali, ambako imesaidia kuanzia ujenzi na hata vifaa tiba. Hii nayo pia ni kusaidia kupambana na adui maradhi. Serikali tunatambua na kuthamini mchango wenu na tunaomba muendelee na sapoti hizo,” alifafanua Zephania.

Alizitaka taasisi mbalimbali nchini kufuata nyayo za NMB katika kusaidia utatuzi wa changamoto za kijamii, huku akiwataka wanafunzi na walimu wa Shule za Kidawendui na Jibondo kutunza viti na meza hizo, ambayo ni mbinu sahihi ya kuvutia taasisi zaidi kujitoa kusaidia kutatua kero nyingi zilizopo, ambazo dawa ya kuzimaliza ni pamoja na utunzaji wa misaada inayowafikia.

Akimtangulia DC Zephania, Baragomwa alisema elimu na afya ni sekta za kipaumbele kwa benki yake, ambayo imebadili Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na kuwa Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), lengo likiwa ni kupanua wigo wa kuihudumia jamii katika nyanja hizo pamoja na utunzaji wa mazingira.

“Hizo ni sekta za kipaumbele kwetu, kwani ndio mhimili wa maendeleo ya Taifa lolote duniani. Tunatambua juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia upatikanaji wa elimu bora mijini na vijijini, nasi hatuna budi kuipongeza kwa hilo na tukiwa wadau muhimu, tunao wajibu wa kuunga mkono juhudi za kusaidia jamii ambayo imeifanya NMB kuwa benki kubwa kuliko zote nchini.

“Tulipopata maombi ya kuchangia maendeleo na ustawi wa elimu wilayani Mafia tulifarijika na mara moja tukachagua kuja kushirikiana nanyi na leo tuko hapa kukabidhi meza 50 na viti 50 kwa Sekondari ya Kidawendui vyenye thamani ya Sh. Mil. 7.5, na pia meza 50 na viti 50 kwa Shule ya Sekondari Jibondo vyenye thamani sawa na hiyo. Hii inamaanisha kwa ujumla msaada kwa shule hizi una thamani ya Sh. Milioni 15,” alisema Baragomwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mafia (DED), Kassim Ndumbo, alikiri kuwa changamoto katika sekta ya elimu ni nyingi na kwamba Serikali pekee haiwezi kuzimaliza bila nguvu za wadau kama NMB, na kuongeza shule za sekondari katika wilaya yake zina uhitaji wa viti na meza 4,332, vilivyopo ni 3,464, huku shule za msingi zikiwa na upungufu wa madawati 1,000 kwani uhitaji ni madawati 6,000 na yaliyopo ni 5,000 tu.

Kabla ya hafla hiyo, msafara wa NMB ulitembelea Ofisi za DC na DED, ambako Baragomwa alimtambulisha Meneja mpya wa NMB Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Dismas Prosper, ambapo DC Zephania aliitaka NMB kushirikiana na serikali yake kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilizopo Mafia. Dismas alimshukuru DC na kumtaka kuitegemea benki yake katika mipango ya kimaendeleo iliyonayo.

By Jamhuri