Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

BENKI ya NMB, imetangaza udhamini wa Sh. Milioni 30 wa Mashindano ya Gofu ya Mkuu wa Majeshi Tanzania (NMB CDF Trophy 2023), yanayotumika kuadhimisha miaka 59 ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ).

Huu ni msimu wa nane mfululizo kwa NMB kudhamini CDF Trophy, mashindano ya wazi yatakayofanyika Septemba 2 na 3 kwenye Viwanja vya Gofu Lugalo, ambapo mwaka huu yatatanguliwa na Mashindano ya Majeshi (Combat Fiddle), hapo Septemba Mosi, yakishirikisha timu za Majeshi ya Tanzania na Malawi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi ya mfano kwa Brigedia Jenerali Mstaafu, Michael Luwongo ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo (TPDF Lugalo Golf Club – inayoandaa mashindano hayo), Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa NMB, Aikansia Muro, alisema benki yake inajisikia fahari kwa aina ya mashirikiano mema yaliyopo baina yao na JWTZ yanayowasukuma kuendelea kudhamini.

“Tunaishukuru Lugalo Golf Club na JWTZ kwa ujumla, kwa ushirikiano mwema na endelevu baina yetu, ambao umetupa heshima ya kudhamini CDF Trophy kwa miaka nane sasa. Udhamini huu endelevu unaodhihirisha kuwa kuna mahusiano mazuri baina ya NMB na JWTZ, unachagizwa pia na dhamira yetu ya kutambua umuhimu wa michezo kwa jamii.

Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Aikansia Muro (wa pili kushoto), Meneja Mwandamizi wa Wateja Binafsi NMB, Priscus Kavishe (kushoto), wakikabidhi kwa pamoja mfano wa hundi ya Sh. Mil. 30 kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Michael Luwongo (katikati) kwa ajili ya udhamini wa Mashindano ya NMB CDF Trophy 2023 yatakayoanza Septemba 2 katika viwanja vya Gofu Lugalo. Wanaoshuhudia ni Nahodha Klabu ya Gofu Lugalo, Meja Japhet Masai (kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga.  (Na Mpiga Picha Wetu).

“Katika kufanikisha mashindano haya mwaka huu JWTZ inapoadhimisha miaka 59 hapo Septemba Mosi, NMB tumetoa Sh. Milioni 30 kufanikisha michuano hii ya mwaka huu.

“Huu ni muendelezo wa benki yetu kudhamini michezo nchini, ambako karibuni tu tumesaini makubaliano ya kuongeza ufanisi wa usajili wa Mashabiki na Wanachama wa klabu kongwe za soka za Yanga na Simba, huku tukiwa na kumbukumbu chanya za kuzidhamini Taifa Stars, Azam FC, Singida United, timu ya Taifa ya mpira wa magongo na Mashindano ya mashule,” alibainisha Aikansia.

Kwa upande wake, Brigedia Jenerali Mstaafu, Luwongo, aliishukuru NMB kwa kuyabeba mashindano hayo kila mwaka wanapokuwa katika Maadhimisho ya Kuanzishwa kwa JWTZ Septemba 1, 1964 na kwamba pamoja na shughuli mbalimbali za kijeshi zinazofanyika, wao kama klabu ya Gofu ya Jeshi hilo, wanaadhimisha kwa mashindano ya kumuenzi Mkuu wa Majeshi (CDF).

“Tunawashukuru na kuwapongeza NMB kwa ushiriki wao katika mashindano haya, ambayo yatakuwa ya wazi yakishirikisha timu za Jeshi la Tanzania, Malawi na timu za kiraia, yakitangukiwa na Combat Fiddle Ijumaa ya Septemba 1.

“Malawi ambao walishiriki pia mwaka jana, watakuja na timu za Jeshi lao, lakini pia Klabu ya Gofu ya Lilongwe (Lilongwe Golf Club) ambayo ni ya kiraia, msafara wao utajumuisha takribani washiriki 20, huku tayari washiriki wa ndani wapatao 100 wakiwa wameshajisajili.

“NMB CDF Trophy ni shindano la kipekee kabisa, ambalo litakuwa na zawadi nzuri zilizoboreshwa zaidi kwa ajili ya washindi wa kategori zote za ‘Professional,’ Watoto (juniors), Divisheni za A, B na C, pamoja na wanawake na ‘seniors.’

“Tutaitumia NMB CDF Trophy kuiandaa timu ya Taifa ya Tanzania ya Gofu itakayoshiriki Mashindano ya Jumuiya ya Madola, huko San Diego, Marekani, ambako Afrika itakuwa nchi pekee kuiwakilisha Afrika,” alisema Brigedia Jenerali Mstaafu Luwongo.

Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kisiga, aliipongeza NMB kwa udhamini uliotukuka unaolenga kuhamasisha maendeleo na kukuza mchezo huo nchini, huku Nahodha wa Klabu ya Gofu Lugalo, Meja Japhet Masai, akijinasibu utayari wa kikosi chao na kwamba watautumia uenyeji wao kutwaa mataji ya mashindano hayo ya wazi yatakayosimamiwa na TGU.

Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Aikansia Muro (wa pili kushoto), akimkabidhi mfano wa hundi ya Sh. Mil. 30 Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Michael Luwongo (katikati) kwa ajili ya udhamini wa Mashindano ya NMB CDF Trophy 2023 yatakayoanza Septemba 2 katika viwanja vya Gofu Lugalo. Wanaoshuhudia ni Meneja Mwandamizi wa Wateja Binafsi wa NMB, Priscus Kavishe (kushoto), Nahodha Klabu ya Gofu Lugalo, Meja Japhet Masai (kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga.  (Na Mpiga Picha Wetu).