Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Mohamed Mchengerwa ameitaka Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kwenda kuondoa utendaji wa mazoea ili kuweka misingi ambayo itaifanya Tanzania kuwa namba moja Afrika na dunia katika sekta ya utalii.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hii leo jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Aidha, ameitaka Bodi ya TTB kukaa na Menejimenti ili kufanya mapitio ya Sheria ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii.

Waziri Mchengerwa ameitaka Bodi kwenda kutatua mara moja changamoto zilizopo na kusimamia mikakati ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ambapo amefafanua kuwa idadi ya vivutio vilivyopo nchini hailingani na mapato yanayopatikana.

Amesema bila utangazaji madhubuti unaokwenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa watalii, taifa haliwezi kunufaika na rasilimali za utalii zilizopo nchini hata kama uhifadhi wa rasilimali hizo utaimarishwa.

Amempongeza Rais kwa maono yake ya kuifungua na kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kupitia filamu ya The Royal Tour.

“Ni katika muktadha huo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliamua kutufungulia njia kwa kuanzisha Programu maalum ijulikanayo kwa jina la Tanzania: “The Royal Tour’’ inayolenga kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji. Hivyo, tunao wajibu wa kuhakikisha kuwa Programu hiyo inakuwa endelevu sambamba na kuanzisha mikakati mbalimbali itakayochochea ongezeko la watalii hapa nchini pamoja na mapato yatokanayo na Sekta ya Utalii”. amefafanua Mchengerwa

Kwa upande wa Bodi ya TANAPA, ametoa wito kwa Bodi ya kuendelea kusimamia mfumo wa kijeshi ili kuweza kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Jeshi la Uhifadhi hususani katika eneo zima la uhifadhi wa rasilimali za Wanyamapori na Misitu katika maeneo ya hifadhi zote.

Share this Ar