NMB yamwaga neema shule tano Temeke

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar

BENKI ya NMB imekabidhi msaada wa vifaa mbali mbali vyenye thamani ya milioni 39 kwa shule tano za Temeke huku iksisitiza dhamira yake ya kuendelea kusaidia mipango ya maendeleo ya sekta ya elimu nchini kote.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na mabati 600, madawati 100 na meza 50 yatakayonufaisha Shule ya Msingi Chem Chem, Shule ya Msingi Azimio, Shule ya Msingi Mtoni, Shule ya Msingi Magurumbasi na Shule ya Sekondari Kibasila.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika Sekondari ya Kibasila, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard amesema jitihada za benki hiyo zinalenga kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha maendeleo ya sekta ya elimu.

Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard (wa tatu kulia), akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa, sehemu ya msaada mabati 600 kwa ajili ya shule tatu za msingi zilizopo wilaya ya Temeke, pia NMB imekabidhi madawati 100 kwa shule moja ya msingi, pamoja na viti 50 na meza 50 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kibasila.

“Serikali imefanya kazi kubwa ya kuweka miundombinu ya sekta ya elimu. Shule nyingi mpya zimejengwa na Serikali ya awamu ya sita. Kama benki, tunaona ni muhimu kuunga mkono juhudi za kuinua sekta hii ndomaana tumejikita kutoa vifaa vya shule nchi nzima,” amesema.

Ameongeza, “Kama benki, tunatoa asilimia moja ya faida yetu kila mwaka kusaidia sekta ambazo tuimezipa kipaumbele katika mkakati wetu wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ambao unalenga sekta kama vile afya, elimu na dharura. Kama sehemu ya mpango wetu wa CSR, leo tunakabidhi bidhaa zenye thamani ya 39m/- na tunaamini hii itasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia katika shule zitakazonufaika,”

Awali, Mbunge wa Jimbo la Temeke, Dorothy Kilave amesema msaada huo umekuja wakati muafaka hasa wakati huu ambapo wilaye yake imeeanza kutekeleza kampeni yake ya ‘Boresha vya Kale’ ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kukarabati shule kongwe wilayani humo.

“Serikali imeanza kujenga shule mpya kote nchini ila siai mama wilaya, tumeona ni wakati muafaka wa kuboresha shule kongwe ili zisibaki nyuma zikiwa katika hali mbaya ndiyo maana tukaja na kampeni hii. Tunaishukuru Benki ya NMB kwa kuunga mkono juhudi zetu na tunaamini msaada wao utafanikisha kampeni yetu.” amesema.

Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard (katikati), akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa, sehemu ya msaada wa madawati 100 kwa ajili ya Shule ya Msingi, Chemchem ya Mbagala, pia NMB imekabidhi mabati 600 kwa shule tatu za msingi, pamoja na viti 50 na meza 50 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kibasila, zilizopo wilayani Temeke. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Temeke Hassan Rugwa ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kuunga mkono wilaya hiyo na kuongeza kuwa benki hiyo imekuwa mstari wa mbele na bidhaa nyingi zinalenga watu wa ngazi ya chini.

“Kuna kambuni nying katika sekta ya kibenki na fedha lakini Benki ya NMB ni ya kipekee. Hivi karibuni, benki ilitangaza bidhaa yake ya mkopo wa elimu ambayo itanufaisha watoto kutoka familia masikini. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru NMB kwa kuendelea kutuunga mkono,” amesema.