Na John Walter, Babati

Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Vijiji vya Endamagay na Gidaboshka, uliopo katika Jimbo la Babati Vijijini.

Mradi huo wenye thamani ya Shilingi bilioni 1.099 unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi 3,766 wa vijiji hivyo na maeneo ya jirani.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Aweso alisema Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.

Alibainisha kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 30, 2026, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 87.

Katika ziara hiyo, Waziri Aweso aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Baran Sillo.

Kufuatia hatua iliyofikiwa na mradi huo, Mhe. Aweso alitoa maelekezo kwa Wizara ya Maji kuhakikisha ndani ya kipindi kifupi inapatikana Shilingi 508,300,000 kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizosalia, ili mradi ukamilike kwa wakati na wananchi waanze kunufaika na huduma ya maji safi na salama kama ilivyopangwa.