Nyerere alitabiri madhara ya uuzaji ardhi

Oktoba 14, mwaka huu Watanzania tuliadhimisha miaka 14 ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ifuatayo ni makala iliyoandaliwa na MWANDISHI WETU kwa msaada wa blogu ya Udadisi, ikielezea mtazamo wa kiongozi huyo kuhusu uzaji ardhi.

“Katika nchi kama yetu, ambamo Waafrika ni masikini na wageni ni matajari, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi yake katika miaka themanini au mia moja ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni na wenyeji watakuwa watwana. Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri na wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.” JKN 1958 (Uhuru na Umoja)

Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyasema haya mwaka wa 1958 wakati wa vuguvugu la kupigania uhuru katika makala yake iitwayo Mali ya Taifa.

Inaelezwa kwamba Mwalimu Nyerere aliamua kuandika maneno hayo kutokana na jaribio la Waingereza kuingiza nchini na mfumo wa umiliki wa ardhi usiokuwa na ukomo (freehold). Suala hilo lilipendekezwa na Tume ya Malkia wa Uingereza ya mwaka 1953-1955 iliyolitekeleza katika nchi tatu zilizokuwa chini ya utawala wa Mwingereza, ambazo ni Kenya, Tanganyika na Uganda.

Mtazamo wa tume hiyo ni kwamba mfumo huo ulikuwa bora zaidi ikilinganishwa na mfumo wa umilki wa ardhi wa pamoja chini ya misingi ya mila na desturi za makabila mbalimbali. Pendekezo hilo lililenga zaidi kuingiza mfumo wa soko huria katika kuratibu suala zima la mfumo wa milki ya ardhi.

Kwa mtazamo wa Mwalimu, kuruhusu mfumo wa aina hiyo siyo tu kungeleta matabaka ya wenye ardhi na watwana, lakini pia kwa mazingira ya nchi yetu ungekuwa chanzo cha machafuko ya kijamii. Pendekezo hilo lilikubalika kwa majirani zetu Kenya na likawa ndiyo chanzo kikubwa kwa walalahai na walalaheri wa huko kujilimbikizia maeneo makubwa ya ardhi kiasi cha baadhi yao kumiliki ardhi yenye ukubwa unaolingana na eneo la nchi ya Rwanda!

Hapa nchini baada ya kupata upinzani kutoka kwa viongozi wa kisiasa wa wakati huo wakiongozwa na Mwalimu Nyerere, wazo lilizikwa rasmi miaka ya mwanzoni ya uhuru. Kimsingi Mwalimu Nyerere aliichukulia ardhi kama zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wote na si kundi la wachache.

 

Baada ya kupata uhuru, sheria ya Kikoloni ilifanyiwa marekebisho madogo, lakini msingi wa sheria ulibakia pale pale. Kutokana na dosari katika sheria hiyo, wazalishaji wadogo, wakulima, wafugaji na makundi mengineyo yaliathirika, hasa lilipokuja suala la uhakika wa miliki.

Pamoja na kwamba Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ilikuwa na nia nzuri ya kuwakwamua Watanzania kutoka katika lindi la umaskini kupitia Sheria ya Ardhi ya Kikoloni ya Mwaka 1923, wengi walijikuta wakipoteza haki zao.

Uanzishwaji wa mashamba ya lililokuwa Shirika la Kilimo na Chakula (NAFCO), Ranchi za Taifa (NARCO) na upanukaji wa maeneo ya hifadhi ni mifano michache inayoonesha jinsi haki za watu juu ya ardhi zilivyopokwa. Ardhi ilipokwa kutoka mikononi mwa wananchi ama umma na kuwekwa mikononi mwa dola, siyo katika wakati wa Mwalimu Nyerere tu bali kutoka enzi za ukoloni.

Kimsingi, utaifishaji na mengineyo yaliyofuatia yalikuwa ni sehemu tu ya kile tulichokirithi kutoka kwa wakoloni.

Je, aliyoyasema Mwalimu Nyerere mwaka 1958 katika kipindi chetu yamepoteza maana ama yanasadifu yanayotokea sasa? Baada ya kukaa na sheria hiyo ya Kikoloni kwa takriban miongo saba (1923-1999), Serikali kwa kufuata mapendekezo ya Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Migogoro ya Ardhi ya Mwaka 1991, iliamua kutunga sheria mpya za Ardhi mwaka 1999.

Sheria ya Ardhi Namba 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 za mwaka 1999, pamoja na mazuri yaliyokuwamo bado msingi wake mkuu unabaki kuwa sheria ya Kikoloni kwa maana ya kulimbikiza nguvu nyingi mikononi mwa dola. Ardhi inatajwa kuwa mali ya umma, lakini kivitendo ni mali ya Serikali zaidi kuliko kuwa ya umma. Sheria hizi zilifanyiwa marekebisho mwaka 2004, ambayo kinyume cha Mwalimu, yanatambua ardhi tupu ambayo haijaendelezwa kuwa ina thamani na yanaruhusu ardhi kuuzwa kama bidhaa nyingine yoyote sokoni.

Katika makala yake ya 1958, Mwalimu ameendelea kutanabahisha, “Wakati watu wengi watakapokubali njia ambayo itawawezesha wachache kumiliki ardhi ambayo kwa kweli ni zawadi ya Mungu kwa watu wote, watakuwa wanaukubali utumwa kwa hiari yao wenyewe.”

Je, matokeo ya mabadiliko ya Sheria ya Ardhi ya mwaka 2004 ni nini? Tunaweza kusema utabiri wa Mwalimu Nyerere katika hilo umetimia? Je, kumeibuka kundi la Watanzania matajiri wajanja wachache ambao kazi yao ni kuwanunua waungwana tuliosalia tusiyo na hili wala lile tukisogezwa pembezoni zaidi?

Wakati wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Kiongozi wa nchi alishangaa kuona Watanzania wakiwa hawafaidi matunda ya mageuzi ya soko huria, hivyo aliamua kwenda nchini Peru kutafuta mwarobaini wa tatizo hilo, matokeo yake ndiyo marudio ya yale ambayo Tume ya Malkia ilipendekeza, lakini kwa mtazamo wa kuwa kila kipande amilikishwe mtu binafsi kwa kuwa masuala ya umiliki wa pamoja ni mambo ya Ujamaa uliokwishapitwa na wakati.

Pamoja na hayo, hiyo ndiyo njia rahisi ya kupata ardhi kwa Watanzania wajanja wachache ama wageni matajiri kwani badala ya kuongea na ukoo sasa wataongea na mtu binafsi!

Ukitembelea vijiji vya pembezoni mwa miji yetu utagundua kuwa wamiliki wa awali sasa wamebakia kuwa watwana katika ardhi zao kwa kuwa walishauza ili kukidhi haja na shida zao mbalimbali. Kwa kuwa Watanzania wengi tegemeo lao kubwa ni ardhi, machafuko ya kijamii ambayo Mwalimu Nyerere aliyahofia enzi zake, kwamba kama tusipokuwa makini yanaweza kutokea, leo yamekuwa ni wimbo wa kawaida katika vyombo vya habari!

Mashamba makubwa yaliyochukuliwa na Serikali kwa lengo zuri la kuifaidisha jamii nzima, siku hizi yamebinafsishwa na wakati mwingine mashamba yamebinafishwa hata pale ambapo wanavijiji waishio jirani nayo wana mahitaji ya ardhi.

Migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo hapa Tanzania ni ishara ya jamii kuchoshwa na mgawanyo wa rasilimali unaofaidisha kundi dogo la wateule, huku wana wa nchi wakitaabika kutafuta wapi pa kukamata! Wimbi la ujio wa wageni wanaotamani ardhi yetu nalo bila shaka katika miaka michache ijayo litaongeza petroli katika moto ambao kama hatutakuwa makini katika kipindi hiki utalipuka.

Tuliokuwepo sasa tumesahau kuwa kama alivyotuasa Mwalimu Nyerere, ardhi ni mali yetu, lakini hasa ni mali ya vizazi vijavyo, hivyo tumekabidhiwa kama dhamani kwa ajili ya kutuwezesha, lakini hasa kukiandalia mazingira mazuri kizazi kitakachofuata.                   Bila shaka huo ulikuwa ni msingi wa kuweka msisitizo katika jamii za Kitanzania kuwa msitari wa mbele, hasa kuanzia ngazi ya familia na kijiji katika kujumuika kwa pamoja kujiletea maendeleo endelevu.

Siku hizi tuna mikakati mbalimbali na hivi karibuni ulizinduliwa Mkakati wa Kilimo Kwanza. Je, Kilimo Kwanza ni kwa ajili ya kundi gani, kinamlenga nani? Je, kimetambua nafasi ya hilo kundi la wazalishaji wadogo, hasa akina mama ambao kimsingi ndiyo wanaolilisha taifa?

Ikumbukwe kwamba Mwalimu Nyerere alipata kusema kuhusu namna akina baba wa Kitanzania wanavyotumia muda wao. Nusu ya maisha yao wapo likizo, huku kazi za shamba zikifanywa na akina Mama! Je, nafasi ya akina mama imetambuliwa na Kilimo Kwanza? Au ndiyo mikakati ya kuwezesha Watanzania matajiri wajanja wachache kunyakua maeneo makubwa ya ardhi kwa kisingizio cha Kilimo Kwanza?

Katika Azimio la Kilimo Kwanza kuna pendekezo la kufanyia marekebisho Sheria ya Ardhi ya Vijiji kuwezesha upatikanaji wa ardhi uwe rahisi. Imeshindikana kuviwezesha vijiji viwe msingi wa Kilimo Kwanza kwa kutumia ardhi, au Kilimo Kwanza kinanoga pale mfanyabiashara bepari akitoka Dar es Salaam na kwenda kunyakua ardhi ya wana wa Mara, Simiyu, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na Geita?

Nihitimishe mahaka hii ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa mwalimu Nyerere kwa kusema kwamba masahibu wanayowakumba majirani zetu siyo majanga ya asili ila ni kazi ya akili za binadamu. Tukiachia hulka za kibinafsi zitawale uamuzi na mienendo yetu ya kimaisha hii amani tunayojivunia sasa itayeyuka kama barafu ya Mlima Kilimanjaro inavyoyeyuka. Tukumbuke kuwa panapofuka moshi moto hufuatia.

Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache ujao kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana na vizazi vya watwana havitakubali hilo, hivyo tutakuwa tumekiandalia kizazi kijacho vita na machafuko kwa tamaa ya kujilimbikizia kila kipande cha ardhi.

Hiyo ni changamoto kubwa kwa viongozi wetu wa Serikali kuhakikisha wanadhibiti tatizo hilo kwa dhati ya moyo kwa manufaa ya Watanzania wengi katika kizazi cha sasa na vijavyo.