Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameagiza kukamatwa kwa watu waliovunja makazi ya watu zaidi 30 nyakati za usiku eneo la Majoe Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam

RC Chalamila amesema hayo leo Desemba 22,2023 alipotembelea eneo hilo na kujionea nyumba zilizo bomolewa na watu ambao hawafahamiki kwa kuwa uhalifu huo umekua ukifanyika nyakati za usiku.

Albert Chalamila baada ya kuwasikiliza waathirika wa mgogoro huo alimuagiza OCD na TAKUKURU kumkamata Mwenyekiti wa Mtaa wa Majoe ili aweze kuhojiwa ni watu gani wamefanya uhalifu huo ” haiwezekani watu wanakuja kubomoa nyumba usiku alafu hawajulikani na mwenyekiti yupo hili halikubaliki” amesema RC Chalamila.

Vilevile RC Chalamila amemtaka OCD kuwasaka na kuwakamata wote waliojihusisha na tukio hilo, apeleleze kwa kina ajue ni akina nani, hatua itakayofuata ni atakuja tena na vyombo vyake pamoja na timu ya wataalam wanasheria na wataalam wa Ardhi ili kupata ufumbuzi wa mzizi wa mgogoro huo.

Aidha RC Chalamila ameagiza eneo hilo kuanzia sasa lilindwe ili Isitokee uharibifu au ubomoaji mwingine wa aina yeyote, ambapo amesistiza kitendo kilichofanyika halivumiliki pia kina chafua taswira ya Jeshi la polisi, kinamchafua Rais na Chama cha Mapinduzi kwa ujumla.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema alifika katika eneo hilo na kujionea nyumba zilizo bomolewa ambazo ni zaidi ya 30 na wamiliki wa nyumba hizo hadi sasa wamekua wakihangaika kutokana na kukosa makazi.

RC Chalamila amesema hatua aliyoichukua ni ya awali ili apate pa kuanzia na ijulikane wazi hatengui wala kuingilia hukumu ya mahakama.

By Jamhuri