Ofisa wa Jeshi ajitosa kutetea wapagazi

MOSHI

NA CHARLES NDAGULLA

Kilio cha masilahi duni kwa wapagazi katika Mlima Kilimanjaro kimeendelea kusikika kwa makundi mbalimbali yanayopanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.
Safari hii Kanali Machera Machera wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ameungana na wapagazi hao kupaza sauti za kutaka masilahi yao yaangaliwe kwa karibu.
Kanali Machera aliongoza kikosi cha watu 40 wakijumuisha askari wa JWTZ, wanahabari na maofisa kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupeleka bendara ya taifa katika kilele cha Uhuru ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika.
Akizungumza kwenye Lango Kuu la Marangu baada ya kukamilisha safari ya siku sita za kupanda mlima huo, Kanali Machera anasema kazi inayofanywa na wapagazi na waongozaji wageni ni ngumu na ni ya hatari sana kwa maisha yao.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kazi inayofanywa na watu hawa ni ngumu na inahatarisha maisha yao. Ukiwa kwenye kituo cha Gilmans unawaona wanapanda na kushuka kwenda kusaidia wageni wanaopata matatizo lakini masilahi yao kwa kweli ni duni sana,” anasema.
Kanali Machera ametoa wito kwa serikali kuzisimamia kwa ukamilifu sheria zinazolinda masilahi ya waongozaji wageni, wapagazi pamoja na wapishi, ikiwamo pia kuanzishiwa bima ya afya itakayowawezesha kutibiwa pindi wanapopatwa na matatizo ya kiafya.
Anabainisha kuwa pamoja na makundi haya kuwa na umuhimu mkubwa kwenye sekta ya utalii, hasa kwenye hifadhi hiyo ya taifa, bado wanafanya kazi katika mazingira magumu wakipata malipo duni, mavazi yasiyoendana na hali halisi ya mlimani na lishe duni.
Ukiondoa jukumu kubwa la waongozaji wageni la kuhakikisha mgeni anafika kilele cha Uhuru, wapagazi ama wagumu kama wanavyoitwa, wana kazi kubwa ya kubeba mizigo ya wageni kwenda na kurudi kwa siku sita ama zaidi, ikiwamo pia kubeba vyakula, majiko ya gesi na maji kwa ajili ya mahitaji ya wageni.
Hata hivyo, pamoja na serikali kuweka viwango vya mishahara ya kila kundi kupitia Tangazo la Serikali (GN) Namba 228 la mwaka 2008 linalotaka watu hao walipwe malipo mazuri, utekelezaji wake umekuwa ni wa kusuasua huku kukiwa hakuna jitihada zozote za serikali kuhakikisha utekelezaji wa tangazo hilo zaidi ya matamko ya mawaziri wenye dhamana na wizara hiyo.
Tangazo hilo limeweka kiwango cha dola 20 za Marekani kwa siku kwa waongoza wageni (Tour  Guide), dola 15 kwa wapishi na dola 10 kwa siku kwa wapagazi (porters), maarufu kwa jina la wagumu. 
Hata hivyo, chama cha waongozaji watalii Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru (KILI/MERU), kimelalamika kuwa tangu tangazo hilo la serikali kutolewa zaidi ya kampuni 700 za uwakala wa utalii zimekuwa hazilipi viwango hivyo na badala yake wanatoa malipo duni kwa watu hao.
Oktoba mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, aliongoza timu ya wapanda mlima kupanda Mlima Kilimanjaro katika kampeni yake iliyopewa jina la HK Kili Challenge na kuguswa na kazi ngumu zinazofanywa na wagumu ambao hawakusita kuwasilisha kilio chao kwake.
Dk. Kigwangalla alikiri wazi kuwa kwa mtu ambaye hajawahi kupanda mlima huo hawezi kujua umuhimu wa makundi hayo ambayo ndiyo roho ya utalii katika mlima huo, kwani bila makundi hayo matatu ni ndoto kwa makampuni ya utalii kufanya biashara hiyo kwa ufanisi.
“Lazima tukubali, bila guides, porters na wapishi, hauwezi kuupanda huu mlima. Ni watu muhimu sana, lakini kwa mtu ambaye hajapanda huu mlima hawezi akajua umuhimu wao, mimi nimepanda nimeona umuhimu wao,” anasema.
 
MWISHO.