Padri Kitunda amenigusa, tujenge uzalendo

Najua baadhi ya wasomaji wangu wanapenda kila wakati tuandike siasa, uchumi na mambo mengine ya kijamii. Leo naomba mniruhusu nichepuke kidogo. Kuna kitu kimenigusa katika ibada niliyohudhuria Jumapili iliyopita katika Parokia yetu ya Roho Mtakatifu ya Kitunda. Paroko Msaidizi, Paul Njoka, alitutaka kanisani tufurahie siku ya Uhuru kwa kuimba nyimbo za uzalendo.

Sitanii, amefafanua kwa kina umuhimu wa nyimbo hizi kama msingi wa kuhifadhi historia na kuwafanya watoto wajivunie taifa lao la Tanzania. Moyo wangu ulijawa furaha sana. Mwongoza kwaya wa pili aliniburudisha kwa kiasi kikubwa, kwani alikuwa akiwaongoza hadi waumini. Ila si kwaya au waumini waliokuwa wamejiandaa vema.

Niliwaangalia usoni wakati tunaimba nyimbo hizi, ukiacha kukosea maneno ya nyimbo hizi muhimu kwa taifa letu, baadhi ya vijana waliamua kukaa kimya. Mdundo wa nyimbo hizi baadhi wanaziimba kama Wazungu, badala ya asili yake. Nikasema angalau katika kulinda na kukuza uzalendo leo kupitia safu hii niandike beti za nyimbo hizi kwa mzazi atakayepata fursa amfundishe mwanae.

Tulianza na Tazama Ramani…

1. Tazama ramani utaona nchi nzuri,

Yenye mito na mabonde mengi ya nafaka,

Nasema kwa kinywa halafu kwa kufikiri,

Nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania.

Majira yetu haya, yangekuwaje sasa,

Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X2

 

2. Chemchemi ya furaha amani nipe tumaini,

Kila mara niwe kwako nikiburudika,

Nakupenda sana hata nikakusitiri,

Nitalalamika kukuacha Tanzania.

Majira yetu haya, yangekuwaje sasa,

Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X2

 

3. Nchi yenye azimio lenye tumaini,

Ndiwe peke yako mwanga wa Watanzania,

Ninakuthamini hadharani na moyoni,

Unilinde nami nikulinde hata kufa.

Majira yetu haya, yangekuwaje sasa,

Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X2

Baadaye Paroko Msaidizi, Njoka, akawambia wanakwaya waendelee na nyimbo hizi za uzalendo. Wimbo wa Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa Moyo Wote, nao nikasikia watu wanauma maneno. Nikasema wimbo huu nao niwafikishie wasomaji wangu waukariri na kuwafundisha watoto wao, si wa parokia yangu tu, bali nchi nzima.

1.Tanzania Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote,

Nchi yangu Tanzania, Jina lako ni tamu sana,

Nilalapo nakuota wewe, Niamkapo ni heri mama wee.

Tanzania Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote.

 

2. Tanzania Tanzania, Ninapokwenda safarini, 

Kutazama maajabu, Biashara nayo makazi, 

Sitaweza kusahau mimi, Mambo mema ya kwetu kabisa. 

Tanzania Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote. 

 

3.Tanzania, Tanzania, Watu wako ni wema sana, 

Nchi nyingi za kuota, Nuru yako hakuna tena, 

Na wageni wa kukimbilia, Ngome yako imara kweli wee. 

Tanzania Tanzania, Heri yako kwa mataifa. 

 

4. Tanzania Tanzania, Karibu wasio na kwao, 

Wenye shida na taabu, Hukimbizwa na walo wezi, 

Tanzania yawakaribisha, Tuungane kiumbe chema wee. 

Tanzania Tanzania, Mola awe nawe daima. 

Kabla padri hajahitimisha ibada akatutaka waumini tuimbe wimbo wa taifa kujivunia siku hii adhimu ya Uhuru kwa Tanganyika kufikisha miaka 57 ya Uhuru uliopatikana Desemba 9, 1961, ila kwa bahati mbaya nao nikasikia baadhi ya watu wanauma midomo. Nikasema wimbo huu nao niuweke hapa.

1. Mungu ibariki Afrika, Wabariki viongozi wake,

Hekima umoja na amani, Hizi ni ngao zetu,

Afrika na watu wake,

Ibariki Afrika, Ibariki  Afrika,

Tubariki watoto wa Afrika.

 

2.  Mungu ibariki Tanzania, Dumisha uhuru na umoja

Wake kwa waume na watoto,

Mungu ibariki, Tanzania na watu wake,

Ibariki Tanzania, Ibariki Tanzania,

Tubariki watoto wa Tanzania.

Binafsi nasema Padri Njoka amenipa amani kweli Jumapili iliyopita. Amenikumbusha miaka ya 1970 wakati wa Vita ya Kagera na miaka ya 1980 nikiwa shuleni. Naomba wazazi tuwafundishe watoto nyimbo hizi. Sisi tuliopata fursa ya kuuona utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, nasema tuliifaidi historia kupitia somo la Siasa shuleni. Siku hizi nasikia linaitwa Uraia, ila sina uhakika kama linatimiza malengo. Heri ya miaka 57 ya Uhuru wa Tanganyika.