Wiki iliyopita serikali ilitoa taarifa kuhusu uamuzi wake wa kuanza  mchakato wa ununuzi wa vichwa 22 vya treni, mabehewa 1,430 ya mizigo na mabehewa 60 ya abiria, vitakavyotumika kwenye uendeshaji wa reli ya kisasa, maarufu kama SGR, ambayo ujenzi wake unaendelea chini ya Kampuni ya Yapi Merkez.

Kampuni hiyo (Yapi Merkez) inajenga reli hiyo ya SGR awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 56, na awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma  ikiwa imefikia asilimia 52.  Vipande vyote hivi vina urefu wa zaidi ya kilomita 722, na ujenzi wake unafanyika kwa fedha za ndani Sh trilioni 7.2.

Lakini mbali na kutoa taarifa hiyo, wiki hiyo ya jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alizindua safari ya kwanza ya majaribio ya treni ya wahandisi kwenye eneo la Soga, Kibaha – Pwani.

Mhandisi Kamwelwe amesema mpango wa sasa wa serikali ni kuwa na ‘seti’ tano za treni za SGR zitakazokuwa na mabehewa manane ya abiria, mpango ambao unalenga kuimarisha  sekta ya usafirishaji wa reli.

Katika uzinduzi huo wa majaribio, treni ilitembea kilomita 20 na kubaini kuwa reli kwa eneo ambalo limetumika kwa safari ya majaribio ni salama, hatua ambayo inakabirisha uamuzi mwingine wa kukamilisha ununuzi wa vichwa vya treni 22 na mabehewa yake 60 ya abiria na 1,430 ya mizigo.

JAMHURI tunapongeza hatua hiyo ya majaribio yaliyofanyika kwa mafanikio, tukiendelea kuamini kuwa usafiri wa reli utakuwa wa msaada mkubwa katika kuinua uchumi kwa kasi ya aina yake nchini. Kwa hiyo, tunashauri kila hatua inayofuata iendelee kutekelezwa kwa umakini mkubwa, kwa mujibu wa sheria za nchi na kubwa zaidi, kwa kutanguliza masilahi ya taifa hili na wananchi wake kwa ujumla.

Wakati wote wahusika katika mradi huu wakumbuke ule msemo wa wahenga kwamba, ‘penye nia pana njia’. Na kwa kweli, katika mradi huu, msemo huo umekwisha kujidhihirisha. Tunawatakia kila la heri wahusika wote kwa masilahi ya taifa.

By Jamhuri