Tumewasikia viongozi wa dini

Mwishoni mwa wiki iliyopita Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) walizindua kitabu chao kinachoelezea namna ya taifa kuendesha uchumi wa soko jamii.

Maudhui ya kitabu hicho yamegusa mambo mengi. Kwa mfano, kuhusu mfumo wa uchumi wa soko jamii nchini, wameainisha dhamira ya mfumo huo wa soko jamii kwamba ni kuwa na taifa imara lenye ukuaji wa uchumi ambao ni endelevu na jumuishi, unaowezesha ushiriki wa watu wote na maendeleo kwa wote.

Kwamba, mfumo huo wa uchumi unaweza kuipeleka Tanzania katika mafanikio ya kiuchumi kwa kufuata miongozo ya kimaadili na mikakati  katika sekta mbalimbali.

Wamebainisha kuwa kuna tunu 11 za msingi zinazosaidia utekelezwaji wa mfumo wa uchumi wa soko jamii ambazo ni ufahamu na ujuzi wa mambo muhimu kuhusu shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko la ndani na ziada kuuzwa nje.

Tunu nyingine ni hekima, ambalo ni jambo muhimu katika siasa kufanikisha uwepo wa utawala bora. Nyingine ni  uwajibakaji, uzalendo, utu wa mtu, uadilifu na jumuiya ambayo inatoa fursa ya mshikamano, kufanya kazi kwa pamoja na kusaidiana ili kufikia mafanikio.

Tunu nyingine kati ya hizo 11 ni vijana, kwamba uwepo wa vijana kwenye jamii na nguvu kazi kubwa kwenye soko la ajira kuna tafsiri kubwa mbili; tafsiri ya fursa na changamoto kwa taifa. Lakini kuna suala la tathmini ya sera za maendeleo na shughuli zote za kiuchumi, kuna uwazi katika kufanya uamuzi na utekelezaji wake na jingine ni umoja na mshikamano.

Kwa ujumla katika kitabu hicho kuna mambo ya msingi ya kuzingatiwa na jamii yote ya Watanzania. Kwa kuwa viongozi hawa wa dini ni sehemu ya jamii, basi jamii kwa umoja wake ifanyie kazi uchambuzi wao huo kuhusu uchumi wa soko jamii kwa Tanzania.