Wiki iliyopita Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alipendekeza kufanyika mabadiliko ya sheria ili kuruhusu watuhumiwa wa makosa yote, yakiwamo ya mauaji na uhujumu uchumi kupewa dhamana.

Lengo la pendekezo hilo ni kupunguza msongamano kwenye magereza nchini. Jaji Mkuu alitoa ushauri huo alipotembelea Gereza la Butimba katika Jiji la Mwanza. Amesema Mahakama imekuwa na mapendekezo kwamba kama ilivyo kwa Kenya, makosa yote mahakama iachiwe haki ya kusimamia dhamana, yaani sheria isifunge dhamana. 

Amesema Kenya hata kesi za mauaji mahakama inatoa dhamana, na kwamba jambo hilo linawezekana hata hapa nchini. Mbali na hilo, Jaji Mkuu amesema hata masharti ya dhamana yanapaswa kulegezwa.  Amesema kwa mfano,  sasa hivi wananchi wengi wanamiliki vitambulisho vya taifa, na anahoji, kwa nini visitumike kama dhamana bila kutamka mwananchi aonyeshe mali?

Amesema pendekezo jingine ni kuhakikisha masuala ya kijamii hasa yale yanayohusu mikataba, yashughulikiwe kwa kufuata makubaliano ya mikataba husika badala ya kuwakamata watu na kuwaweka mahabusu. Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, siku hizi kumekuwa na mtindo kwamba masuala ya kijamii kwa mfano mikataba au masuala yanayomhusu mkandarasi (contractor) kushindwa kukamilisha kazi yake, utasikia “kamata weka ndani.” Amesema hali hiyo inachangia msongamano kwenye magereza.

Amesisitiza kuacha masuala ya jinai yaendeshwe kijinai na masuala ya mikataba yaende kimikataba. Sisi JAMHURI tumemsikia Jaji Mkuu kama ambavyo tumekwisha kumsikia Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Augustine Mahiga, ambaye anaamini uwiano (ratio) wa watu waliomo magerezani ni mkubwa kuliko uwezo wake, kwamba kila palipo na mfungwa mmoja kuna mahabusu wanne.

Kwa kuzingatia haya yote, tunaamini kwamba serikali na wadau wote muhimu wa tasnia ya utoaji haki nchini wataendesha mjadala mpana zaidi miongoni mwao ili hatimaye taifa lifaidike zaidi kutokana na mitazamo hiyo iliyokwisha kuwekwa bayana na Jaji Mkuu pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa kitaifa nchini waliowahi kuwamo serikalini, katika sekta binafsi na mashirika ya kimataifa.

Jambo moja muhimu kwa JAMHURI ni kwamba, tunakubaliana na wote wanaoamini kuwa mabadiliko ya hapa na pale yanahitajika katika mfumo wa utoaji haki na usimamizi wa sheria kwa ujumla ili si tu haki itendeke, bali ionekane inatendeka wakati wote.

9726 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!