Vladimir Putin ameionya Korea Kusini itakuwa ikifanya ‘kosa kubwa’ ikiwa itaipatia Ukraine silaha katika vita dhidi ya Urusi.

Maoni yake yanakuja baada ya Seoul kusema inazingatia uwezekano huo, kujibu makubaliano mapya ya Urusi na Korea Kaskazini kusaidiana iwapo kuna “uchokozi” dhidi ya nchi yoyote ile .

Moscow ‘ [itafanya] maamuzi ambayo hayawezi kufurahisha uongozi wa sasa wa Korea Kusini” ikiwa Seoul itaamua kusambaza silaha kwa Kyiv, Bw Putin aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi.

Kiongozi huyo wa Urusi alikuwa akizungumza nchini Vietnam, muda mfupi baada ya ziara ya kifahari huko Pyongyang ambapo alitia saini makubaliano ya ulinzi wa pande zote mbili na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.

Awali Seoul ilikuwa imelaani makubaliano hayo kama tishio kwa usalama wa taifa lake, na mshauri wa usalama wa taifa Chang Ho-jin alisema nchi yake inapanga “kutafakari upya suala la msaada wa silaha kwa Ukraine”.

Kufuatia matamshi hayo ya Bw Putin, ofisi ya rais wa Korea Kusini ilisema Ijumaa kwamba itazingatia “chaguo mbalimbali” katika kusambaza silaha kwa Ukraine na msimamo wake “utategemea jinsi Urusi inavyoshughulikia suala hili”.

Mamlaka pia zinatarajiwa kumwita balozi wa Urusi nchini Korea Kusini ili kulalamika , shirika la habari la Yonhap liliripoti likinukuu vyanzo vya kidiplomasia ambavyo havikutajwa.

Wakati Korea Kusini imetoa msaada wa kibinadamu na zana za kijeshi kwa Ukraine, hadi sasa imekataa kutoa silaha hatari kwa vile ina sera rasmi ya kutozipa nchi silaha vitani.

Baadhi ya watu nchini Ukraine wamekuwa wakitumai kuwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Moscow na Pyongyang ungeifanya Seoul kufikiria upya mtazamo wake. Wachambuzi walisema hapo awali kwamba Kyiv ingetumia ziara ya Bw Putin huko Pyongyang kuongeza shinikizo.