Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Askari wa Jeshi la Polisi CPL Petro Nyabucha ambaye pia ni mganga wa Zahanati ya Polisi iliyopo kwenye eneo la kikosi cha kuzuia ghasia (FFU) eneo la Mahenge Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma amejiua kwa kujipiga risasi shingoni wakati akiwa chooni kwenye eneo la moja ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma akiwa analinda mitihani ya kumaliza elimu ya msingi(darasa la saba) inayotarajiwa kufanyika kitaifa Septemba 13, mwaka huu.

Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimeonekana kuleta taharuki kwa wakazi wa eneo linalozunguka ofisi za Mkuu wa Mkoa Ruvuma zimesema kuwa tukio hilo limetokea Septemba 8, mwaka huu, majira kati ya saa 1 na saa 1:30 asubuhi ambako inadaiwa CPL Nyambucha alikuwa na askari wenzake ambao walikuwa wamepangwa kulinda mitihani ya darasa la saba inayosubiri kusambazwa wilayani mkoani humo.

Baadhi ya mashuhuda ambao waliomba majina yao yahifadhiwe walisema kuwa askari huyo akiwa na askari mwenzake ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja inadaiwa ghafla aliondoka bila kuaga baadae askari mwenzake alianza kumtafuta kwa kuwauliza baadhi ya watu waliokuwa karibu na eneo la jengo ambalo wamehifadhia mitihani kisha baadae wakiendelea kumtafuta ambapo walimkuta chooni akiwa amekufa huku shingoni kukiwa na majeraha.

Wamesema kuwa inadaiwa kuwa CPL Petro Nyabucha ni hivi karibuni ametoka kwenye mafunzo ya udaktari na kwa hivi sasa ni mganga wa Zahanati ya Polisi iliyopo eneo la FFU Mahenge Manispaa ya Songea na bado alikuwa hajaoa na wamedai kuwa ni mzaliwa wa Ukerewe mkoani Mwanza.

Wamesema kuwa baadae taarifa zilitolewa kwa viongozi wa eneo hilo pamoja na viongo wa Jeshi la Polisi ambao walifika kwenye eneo la tukio kisha taratibu zilifanywa za kumtafuta daktari ambaye alifika na kudhibitisha CPL Petro Nyabucha alikuwa amefariki kwa kujifyatulia risasi shingoni kwa kutumia bunduki aliyokuwa amepewa kulindia mitihani na kwamba baadae mwili wa marehemu uliondolewa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa Songea(HOMSO) na kwamba taratibu za kuusafirisha mwwili kwenda Ukerewe mkoani Mwanza zinafanyika.

Hata hivyo jitihada za waandishi wa habari zilifanywa kwa kuutafuta uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma kwa lengo la kupata ufafanuzi zaidi wa tukio hilo ambapo walipofika ofisini kwa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya waliambiwa kuwa hayupo na ofisi amemkaimisha staff One ambaye alitajwa kwa jina moja la afande Husseini na alipopigiwa simu yake ya mkononi ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alisema kuwa afande Staff One Husseini yuko kwenye kikao mjini Tunduru na baada ya masaa 2:30 watakuwa wamefika Songea.

Waandishi wa Habari waliendelea kusubiri ofisini hapo kwa zaidi ya masaa 2:30 ndipo alilazimika kukutana na Staff Two aliye jitambulisha kwa jina la Fadhili Mdemu ambaye amesema kuwa yeye si msemaji na akalazimika kumpigia simu Afande Lamia Mganga ndiye aliyekuwa ameachiwa ofisi na Staff One ambaye alikuwa amekwenda Tunduru.

Baada ya askari huyo kuomba kutoa taarifa hizo akati huyo ameswma kuwa naye si msemaji wa tukio hilo na anayetakiwa kuzungumza ni Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma Afande Husseini .

Hata hivyo waandishi wa habari walifanya juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma Marco Chilya kwa kumpigia simu ambaye alikiri kuwepo kuwepo kwa tukio hilo na amesema kuwa hawezi kutoa taarifa kamili kwa kuwa hayupo mkoani Ruvuma.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya serikali ya Mkoa Songea (HOMSO) Dokta Yona Mwakabumbwe hakuweza kupatikana kwa njia ya simu na baadae taarifa zaidi zilisema kuwa ana kazi yupo kwenye chumba cha upasuaji licha ya kuwa lengo kubwa lilikuwa ni kutaka kupata taarifa zaidi za tukio hilo la askari kujifyatulia risasi shingoni mbaye inadaiwa mwili wake umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali hiyo.

By Jamhuri