Jeshi la Polisi limemfukuza kazi askari wake, PC Hamad Mud wa Kituo cha Polisi Sanya Juu, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, akitajwa kuwa kinara wa mtandao wa wizi wa magari.

Kwa uamuzi huo, Mud anasakwa ndani na nje ya nchi ili afikishwe mahakamani.

Amekuwa akihusishwa na wizi wa magari kutoka Kenya, Rwanda na Uganda. Anatajwa kuwa na uhusiano mkubwa na maofisa wa polisi mkoani Kilimanjaro.

Kabla ya kufukuzwa kazi, alifunguliwa mashitaka ya kijeshi ya utoro kazini, lakini amekuwa mafichoni Kenya ambako inaaminika kuwa na mtandao mkubwa wa wizi wa magari.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa (pichani), ametoa mwito kwa wananchi kusaidia kupatikana kwa Mud.

“Tunao watuhumiwa ambao tunawatafuta wanajihusisha na matukio ya wizi wa magari, katika vita ya kukabiliana na uhalifu sisi tunachoangalia mhalifu yuko wapi na wanaomsaidia ni kina nani.

“Anatafutwa kama watu wengine wanavyotafutwa, tunakaribisha wananchi wenye taarifa zinazomhusu waziwasilishe kwangu,” ameomba Kamanda huyo.

Kauli ya Kamanda Mutafungwa kwa waandishi wa habari, imehitimisha majigambo na vitisho vya askari huyo kwa mwandishi wa habari hizi, kwani kabla ya kufukuzwa kazi aliwahi kutishia kumkamata na kumfungulia mashitaka kwa kile alichodai anachafuliwa.

Mtuhumiwa huyo alitoroka kazini mwaka jana baada ya gari aina ya Benz namba T481 AGS linalodaiwa kuwa ni la wizi ambalo mpaka sasa lipo Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi, kukamatwa nyumbani kwake Rau katika Manispaa ya Moshi.

“Nimekueleza mimi siyo wale mnaowatapeli mjini, mimi ni ofisa na nafanya kazi zangu za Jeshi la Polisi, ninafuata taratibu za jeshi na siyo msemaji wa Jeshi la Polisi, hivyo umekosea, jipange upya.

“Tena unachotumwa ni cha uongo, kajaribu kwa aliyekamatwa na hilo gari labda unaweza pewa rushwa kama unavyotaka hapa…usicheze na mimi nitakupatia pesa za Takukuru,” ilisomeka sehemu ya ujumbe wa maandishi wa Mud wa Julai mosi, mwaka jana kwa mwandishi wa habari hizi.

Katika tukio kama hilo, mwezi uliopita Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, lilimfuta kazi askari wa Kituo Kikuu cha Polisi katika Mji Mdogo wa Himo, Koplo Federika Shirima, kwa tuhuma za kujihusisha na mtandao wa wizi wa magari.

Alikamatwa akiwa na magari matatu yanayoaminika kuwa ni ya wizi; ambayo yamesharejeshwa jijini Dar es Salaam.

Nyumbani kwa askari huyo alikamatwa raia anayetajwa kuwa na uhusiano wa karibu na askari huyo akiwa na vibao 70 vya namba za magari. Mtuhumiwa alipelekwa Dar es Salaam.

Kukamatwa kwa askari huyo na hatimaye kufutwa kazi ni matokeo ya mapambano ya polisi na watuhumiwa wa ujambazi Septemba, mwaka huu, ambako polisi waliwaua watuhumiwa watatu.

Katika mapambano hayo, polisi walikamata bastola 16, simu za upepo na risasi 70.

Gari aina ya RAV 4 lilikamatwa likiwa na namba bandia T 540 CUU likiwa mikononi mwa Mkuu wa Kituo hicho, ASP Zuhura.

Hata hivyo, ofisa huyo hadi sasa hajafutwa kazi zaidi ya kuvuliwa madaraka yake na kurejeshwa Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, kwa kile kilichoelezwa kuwa mamlaka yake ya nidhamu iko kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani.

Katika hatua nyingine, Polisi inachunguza askari wake 10 wa Kituo Kikuu cha Polisi Sanya Juu wanaotuhumiwa kupokea rushwa ya Sh milioni 5 na kuliachia gari aina ya Canter lililokuwa na magunia manane yenye bangi.

Shehena hiyo ilikuwa ikipelekwa Kenya kupitia West Kilimanjaro. Mtuhumiwa ni Ester Stamford Shayo, mkazi wa Tarakea, anayetajwa kuwa kinara wa kusafirisha mihadarati.

Kamanda Mutafungwa alisema Agosti, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Rombo, ilimtia hatiani mwanamke huyo na kumpiga faini Sh 1,000,000 kwa kosa la kukutwa na mihadarati.

3402 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!