Jeshi la Polisi linamtafuta mtu aliyefahamika kwa jina moja la Masoud kwa tuhuma za kumkata sehemu za siri pamoja na chuchu za matiti zote kwa aliyekuwa mpenzi wake aliyedumu naye miezi miwili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP Ramadhani Ng’anzi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Oktoba 9,mwaka huu, majira ya saa
16:45 Jioni, huko maeneo ya hifadhi ya Msitu wa Sayaka uliopo Kata ya Itumbili, Wilaya ya Magu.

Kamanda amesema kuwa katika uchunguzi wa awali mwanamke huyo (jina lake linahifadhiwa) alifanyiwa ukatili huo kwa imani za kishirikina ambapo mtuhumiwa alimuadaa kuwa anaenda kumuonyesha shamba la dengu lililopo katika msitu wa hifadhi ya Sayaka na walipofika alimkaba shingoni na kupoteza fahamu na kutekeleza unyama huo.

Amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya kila jitihada kuhakikisha linamtia nguvuni mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa katika vyombo vya dola. Mhanga wa tukio hilo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Bugando na hali yake inaendelea vizuri.

Wakati huo huo,Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea na operesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu na wahalifu kwenye maeneo ya nchi kavu na majini kwa nia ya kuendeleza kudhibiti hali ya utulivu ndani ya Mkoa.

Kamanda Ng’anzi amesema kuwa katika operesheni za nchi kavu, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata simu 118 na watuhumiwa 8 waliokuwa wanajihusisha na ukwapuaji/uporaji wa simu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza.

“Mafanikio haya ni kutokana na ushirikiano wa wananchi uliowezesha kumkamata mtuhumiwa aliyekuwa anapokea na kununua simu za wizi toka kwa watuhumiwa wa wizi wa simu hizo,” amesema.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama limefanikiwa kukamata injini 4 za boti, nyavu haramu na watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria na kwa upande wa barabarani makosa mbalimbali yameendelea kudhibitiwa na mengine yamekamatwa na kutozwa faini kiasi cha Tshs 360,167,500 ambazo zimeingizwa kwenye mfuko wa serikali.

Hata hivyo,mapambano dhidi ya dawa za kulevya bado yanaendelea ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 8 wa makosa mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kukabiliana na mkono wa sheria.

By Jamhuri