Na Mwandishi wetu Jeshi la Polisi-Dar es Salaam

Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi limepewa jukumu la kulinda maisha ya watu na mali zao ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu hilo ambalo limepata mafanikio makubwa siku hadi siku kutokana na ushirikiano wa vyombo vingine vya dola pamoja na wadau wengine wa ndani na nje na kwa kiasi kikubwa kutoka kwa wananchi wapenda amani, utulivu, mshikamano na watii wa sheria za nchi.

Akitoa taarifa hiyo msemaji wa Jeshi la Polisi nchini kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP David Misime amesema kuwa askari Polisi wanapotekeleza majukumu yao wameruhusiwa na sheria kubeba silaha ili waweze kulinda maisha ya watu na mali zao pamoja na kulinda maisha yao na mali za serikali ikiwepo ni pamoja na silaha aliyobeba askari.

SACP Misime ameongeza kuwa Kumejitokeza mtindo wa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakivunja sheria na wakati mwingine wanatenda uhalifu wa kujichukulia sheria mkononi pamoja na kuwashambulia askari wakiwa wamebeba silaha.

Sambamba na hilo Msemaji wa Jeshi hilo amesema kuwa Jeshi la Polisi nchini linawataka baadhi ya watu kuacha tabia hiyo mara moja kwani askari ni binadamu kama binadamu mwingine na sheria inamruhusu kutumia silaha hiyo kulinda uhai wake pamoja na uhai wa mtu mwingine na mali za watu pamoja na mali za Serikali.

Ametoa rai kwa baadhi ya watu wenye tabia hiyo waache mara moja tabia hiyo na wale ambao wamewahi kufanya hivyo wafahamu kuwa lazima watakamatwa na kufikishwa mahakamani kwani wametenda uhalifu.

By Jamhuri