Na Allan Vicent, JamhuriMedia, Tabora

Shirika la Reli nchini (TRC) limetakiwa kuhakikisha vipande viwili vya mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka DSM–Moro na Moro-Makutupora (Dodoma) vinakamilika haraka ili wananchi waanze kutumia treni hiyo.

Agizo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Ally Possi alipokuwa akihitimisha maonesho ya wadau wa usafiri wa reli kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya usalama wa reli yaliyofanyika kitaifa katika uwanja wa Chuo cha Teknolojia ya Reli mjini Tabora.

Alisema kuwa Rais wa Awamu ya Sita Dk Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya kuunganisha mtandao wa reli nchi nzima hivyo anatamani kuona usafiri huo unaanza haraka ili wananchi waanze kunufaika.

Amebainisha kuwa vipande hivyo viwili vipo katika hatua za mwisho kukamilika hivyo akalitaka Shirika hilo kuhakikisha vinakamilishwa haraka na treni hiyo ianze.

‘Wananchi wana hamu sana kuona treni hiyo ikiianza safari ili waanze kuipanda, imalizieni haraka,’ amesema.

Possi amesisitiza kuwa serikali imeendelea kuifanyia maboresho makubwa miundombinu ya reli ya kati na ile ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuleta tija kubwa kwa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa hiyo ni hatua muhimu sana kwa wafanyabiashara, wakulima na wadau mbalimbali kusafirisha bidhaa zao hivyo kuchochea uchumi wa Taifa.

Amefafanua kuwa usafiri wa reli ni kichocheo muhimu sana kwa uchumi wa jamii na taifa hivyo kwa kulitambua hilo serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu hiyo.

Naibu Katibu Mkuu alitoa wito kwa wananchi kutunza miundombinu hiyo ikiwemo kutoa taarifa za wanaoharibu miundombinu ili kuepusha ajali na wahusika kuchukuliwa stahiki.

Aidha ametaka jamii kuzingatia alama za reli kabla ya kuvuka na kuchukua tafadhari kwenye maeneo ya vivuko vya reli.