Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amebainisha kuwa, Bima ya Afya kwa wote itatoa fursa kwa Mtanzania mwenye hali yoyote kwenda kupata matibabu katika hospitali yoyote zikiwemo hospitali za kitaifa kama Muhimbili na nyingine za kibingwa.

Prof. Makubi amesema hayo, alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Mkoa ya Amana, ambapo alipata fursa ya kuongea Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Amana, Mwananyamala, Temeke, Tumbi, Mbagala Rangitatu, Kigamboni walioongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume na pamoja na tkamati za usimamizi za afya za Halmashauri.

“Kumbukeni Bima ya Afya itakapopitishwa Mgonjwa atakuwa na haki ya kutibiwa hospitali yoyote anayoitaka, yaweza kuwa hospitali ya binafsi au ya Serikali, sasa niwakumbushe kujipanga vizuri katika kutoa huduma bora na kutatua kero za wananchi ikiwemo kukaa muda mrefu, matumizi ya lugha nzuri na misongamano isiyo ya lazima.” Amesema Prof. Makubi.

Amesema, wananchi wana haki yakupatiwa huduma bora, hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali imewekeza katika upatikanaji wa dawa, miundombinu bora, vifaa tiba pamoja na ongezeko la Watumishi katika maeneo ya kutolea huduma za afya nchini.

Serikali inaendelea kuelekeza kuweka kitengo cha huduma kwa mteja katika maeneo yote yakutolea huduma za afya kitachosaidia kupata mrejesho kutoka kwa wananchi juu ya huduma zinazotolewa, huku akisisitiza vitengo hivyo vitapunguzia usumbufu wananchi wanaofika kupata huduma. Amesisitiza Prof. Makubi.

Sambamba na hilo, ameelekeza uongozi wa Hospitali kutoa mafunzo ya huduma kwa mteja ikiwemo matumizi ya lugha nzuri na zenye staha kwa walinzi wa usalama wanaochaguliwa kwenda katika vituo vya kutolea huduma ili kuondoa malalamiko yanayoweza kuzuilika kutoka kwa wananchi.

Aidha, Prof. Makubi amewaagiza Wataalamu wa afya kuboresha uandikaji wa taarifa za mgonjwa ili kuimarisha ufuatiliaji mzuri wa mgonjwa hivyo kuongeza ufanisi katika kutoa huduma, lakini pia itasaidia Serikali katika kufanya tafiti.

Sambamba na hilo, amewaelekeza viongozi wa Hospitali kuimarisha mifumo ya ICT katika maeneo ya kutolea huduma, ikiwemo kuwa na hatua za mbadala endapo mifumo italeta changamoto ili kuondoa kero za kusubiri muda mrefu na misongamano inayoweza kuzuilika katika maeneo ya utoaji huduma.

Pia, amewaelekeza mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuboresha utendaji kazi katika taasisi hiyo, ikiwemo kufanya malipo ya fedha kwa haraka katika vituo vya kutolea huduma ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vituo na uboreshaji wa utoaji huduma kwa wananchi.

Hata hivyo, Prof. Makubi ameendelea kuwakumbusha juu ya kuboresha huduma za mama na mtoto ili kupunguza au kuondoa vifo, huku akisisitiza kuendelea kufanyia uchunguzi kwa karibu vifo vyote vinavyotokana na uzazi ili kujua namna bora ya kukabiliana dhidi ya changamoto hiyo katika vituo vya kutolea huduma.

Suala la magonjwa yasiyoambukiza bado ni janga katika taifa letu, niwaombe kama Wataalamu kulifanyia kazi eneo hili, Watanzania wengi wana changamoto za magonjwa ya moyo, kansa, magonjwa ya njia ya hewa, ajali, vyote vinasababisha mzigo mkubwa wa matibabu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla. Amesisitiza Prof. Makubi.

Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema, Mkoa wa Dar es Salaam umejipanga vizuri kuelekea kuanza kutekeleza matumizi ya Bima ya Afya kwa wote, kwani hali ya upatikanaji wa dawa zilizo katika mwongozo (STG) imefika zaidi ya asilimia 90, huku ujenzi na uboreshaji wa huduma ukiendelea kwa kasi.

“Mkoa wa Dar es Salaam umejipanga kwa kuhakikisha hali ya upatikanaji wa huduma bora, ikiwemo dawa ipo vizuri, tumekuwa tukitumia njia ya re-allocation ili maeneo ambayo kutaonesha dalili za upungufu wa dawa, kuhudumiwa kwa kupewa bidhaa hiyo ili wananchi wasipate hadha yoyote.” Amesema Dkt. Mfaume.