WHO:Afrika ina idadi kubwa ya watu wanaojiua

Shirika la Afya Duniani limesema Afrika ina kiwango kikubwa zaidi cha watu wanaojiua duniani.

Shirika hilo sasa limezindua kampeni ya mitandao ya kijamii ya kuzuia watu kujitoa uhai katika eneo hilo, ili kuongeza ufahamu juu ya suala hilo.

Katika taarifa WHO limesema nchi sita za Afrika ni miongoni mwa nchi kumi zilizo na idadi kubwa ya watu wanaojitoa uhai kote duniani.

Bara hilo linasemekana kuwa na daktari mmoja wa magonjwa ya akili kwa kila wakazi 500,000.Hii ni mara 100 chini ya pendekezo la WHO.

Shirika hilo limebainisha kuwa matatizo ya afya ya akili yanachangia hadi asilimia 11 ya mambo ya hatari yanayohusiana na kujiua.

Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti amesema kujiua ni tatizo kubwa la afya ya umma lakini ni nadra kupewa kipaumbele katika mipango ya kitaifa ya afya.