Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, amesema viwanda vingi nchini vimekuwa vikijiendesha kwa kutumia malighafi zitokanazo na bidhaa za kilimo, mifugo, uvuvi na misitu kutokana urahisi wa upatikanaji wa malighafi hizo.

Aliyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba mitatu (3) iliyohusisha TIC (Kituo cha Uwekezaji Tanzania) na makampuni matatu tofauti, ikihusisha makabidhiano ya utekelezaji wa uendelezaji wa jiji la kilimo Mkulazi, Ngerengere, mkoani Morogoro.

Picha mbalimbali wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba mitatu (3) iliyohusisha TIC (Kituo cha Uwekezaji Tanzania) na makampuni matatu tofauti, ikihusisha makabidhiano ya utekelezaji wa uendelezaji wa jiji la kilimo Mkulazi, Ngerengere. Tukio hilo lilifanyika jana mkoani Dodoma

Katika hafla hiyo iliyofanyika leo, jana Ijumaa Dodoma City Hotel, Prof. Kitila alisema sekta ya kilimo imekuwa na mchango mkubwa kwa ustawi wa Tanzania kwa kuwa kilimo ndiyo sekta inayobeba pato la Taifa.

Alisema sekta ya kilimo imekuwa chanzo cha usalama kwa nchi kwa kuwa Tanzania inajitegemea kwa chakula kwa asilimia zote, na kwamba kutokana na hilo ndio maana sekta hiyo imekuwa ikiongoza kwa bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi

Katika hafla hiyo TIC kupitia Mkurugenzi mtendaji wake Gilead Teri alisaini mikataba hiyo sambamba na wawakilishi wa makampuni matatu (3) ya TFP (The Food Platform), Longping Agriscience na Eagle Hills.

Prof Mkumbo alitoa wito kwa wawekezaji wote waliokabidhiwa eneo hilo kuhakikisha wanatekeleza makubaliano ya mikataba yao kwa wakati kama ambavyo matarajio ya serikali yalivyo, na kwamba serikali itahakikisha inasimamia kikamilifu ili uwekezaji huo uoneshe tija kwa jamii.