-Asema kampeni hiyo ni ya siku 10 itaanza Juni 20-30,2024

-Abainisha kampeni hiyo inatarajia kuwafikia wananchi zaidi ya elfu kumi

-Atoa rai kwa wakazi wa DSM kujitokeza kwa wingi kupima afya zao

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Juni 14, 2024 ametangaza kampeni kabambe ya kupima afya bila malipo katika Mkoa huo ambayo inatarajiwa kuanza Juni 20-30,2024 katika wilaya zote za mkoa huo kwa siku mbilimbili kila wilaya ambapo amesema kampeni hiyo inaratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Afya Check.

RC Chalamila ameyasema hayo ofisini kwake Ilala Boma mbele ya waandishi wa habari ambapo amebainisha lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kupima afya vilevile kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambazo anazifanya katika sekta ya afya ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya afya, kusomesha wataalam wa Sekta ya Afya na hata kutoa kibali cha kuajiri wataalam wa afya.

Aidha RC Chalamila amesema kupitia kampeni hiyo magonjwa mbalimbali yatapimwa ikiwemo magonjwa yasiyoambuliza na wataalam wa afya wabobevu watapiga kambi kila wilaya kwa siku mbili mwaka huu uzinduzi wa Afya Check utafanyika Wilaya ya Ubungo katika uwanja wa barafu Juni 20,2024.

Sanjari na hilo RC Chalamila ametoa wito kwa wadau ikiwemo mabenki kujitokeza kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa masilahi mapana ya jamii, pia amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.

Ifahamike kuwa kila wilaya katika mkoa itakuwa na eneo maalum ambapo timu ya wataalam wa Afya Check kwa uratibu wa Mkoa itaweka kambi ya siku mbili kama ifuatavyo Wilaya ya Ubungo-Viwanja vya barafu, Kinondoni- VIwanja vya Biafra, Ilala-Viwanja vya Mnazi Mmoja, Temeke- VIwanja vya Zakhiem na Kigamboni viwanja vya Mjimwema