Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Mashimba Ndaki amesema kuwa Programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI) inakwenda kuleta mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Mifugo.

Waziri Ndaki ameyasema hayo juzi wakati anazungumza na vijana waliochaguliwa kujiunga kwenye vituo atamizi kwa ajili ya mafunzo ya unenepeshaji mifugo katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Kanda ya Mashariki na Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITA) – Buhuri.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea ofisi za CCM mkoa wa Tanga wakati alipofanya ziara ya kikazi mkoani hapo.

Programu ya SAUTI lengo lake ni kuanza kubadilisha fikra za vijana ili waweze kufuga kisasa na kibiashara na kuona kuwa ufugaji unaweza kuwaletea maendeleo makubwa kiuchumi. Aidha, Waziri Ndaki amemshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha Wizara kutekeleza Programu hiyo yenye kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Mifugo.

Akiwa katika kituo cha TALIRI Kanda ya Mashariki, Waziri Ndaki amewataka watafiti kuhakikisha matokeo ya tafiti wanazozifanya zinawafikia wafugaji ili kuweza kuwabadilisha na kuwafanya waanze kufuga kisasa na kibiashara.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba (katikati) na Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Mashariki (kulia), Dkt. Zabron Nziku mara baada ya kuwasili kwenye ofisi zao Mkoani Tanga.

Aidha, baada ya kutembelea vitalu vya majani ambayo tayari yameshafanyiwa utafiti, amewasihi wafugaji kutembelea vituo vya utafiti wa mifugo kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za ufugaji ikiwemo ya kilimo cha malisho. Lakini pia amewasihi wafugaji kuanza kulima malisho na kuyahifadhi ili yaweze kuwasaidia wakati wa kipindi cha ukame.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki, Dkt. Zabron Nziku amesema kuwa TALIRI imekuwa ikifanya tafiti nyingi kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Mifugo inakua na wafugaji wananufaika kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya vijana waliochaguliwa, Bi. Magesa ambaye ni mshiriki wa mafunzo kutoka wilayani Muheza mkoani Tanga ameishukuru serikali kwa kuanzisha vituo atamizi kwa kuwa vitawasaidia kupata elimu ya ufugaji kwa vitendo na hivyo kuwawezesha kufuga kisasa na kwa tija.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akizungumza na vijana waliochaguliwa kujiunga kwenye vituo atamizi wakati alipotembelea Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Buhuri mkoani Tanga ambapo amewataka vijana hao kuhakikisha wanaitumia fursa hiyo ili kujiletea Maendeleo kwa kuanza kufuga kibiashara.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Omary Mgumba (wa nne kutoka kushoto), Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga, Viongozi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Halmashauri ya Jiji la Tanga mara baada ya kumaliza kikao kifupi kilichojadili hali ya mgogoro wa eneo la TALIRI Kanda ya Mashariki lililovamiwa na wananchi

By Jamhuri