Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Arusha

Vijiji 20 kati ya 49 Wilayani Longido, Mkoa wa Arusha, vimetenga eneo la hekta 186.794.2 kwa ajili ya nyanda za malisho ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Katika wilaya hii, asilimia 95 ya wakazi ni wafugaji ambao wanamiliki mifugo 918,248 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 hata hivyo hivi sasa wamekosa malisho ya mifugo na maji kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mwenyekiti Kijiji cha Kimokowa Kilel Olenyokie Mollel

Afisa mifugo na uvuvi wilaya ya Longido, Nestory Daqarro akizungumza na waandishi wa habari za mazingira kupitia mradi wa uhifadhi wa mazingira kwa maarifa asilia ambao unafadhiliwa na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) kupitia programu ya miradi midogo amesema wilaya hiyo, imeathirika sana na mabadiliko ya tabia nchi.

Daqarro amesema kutokana na uhaba wa malisho ya mifugo na maji katika wilaya hiyo, hivi sasa wafugaji wamehamia maeneo ya nje ya wilaya hiyo kusaka malisho hivyo ili kukabiliana na changamoto hiyo wameamua kutenga maeneo ya nyanda za malisho ambapo watapanda majani na kuweka maji.

“Serikali inatambua changamoto za wilaya kwani kwa mwaka wa pili sasa hakuna mvua za kutosha hivyo, vijiji vimetenga maeneo ya nyanda za malisho ambayo yataidhinishwa na serikali kuu ili kuokoa mifugo yao,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji Cha Kimokowa Wilaya ya Longido, Kilel Olenyokie Mollel amesema wameamua kutenga maeneo ya nyanda za malisho ili kuyatunza kwa ajili ya ufugaji.

“Tumekuwa tukikabiliwa na ukame katika wilaya yetu hivyo tumeona ni vizuri kutenga maeneo ya malisho ambayo hayatavamiwa,” amesema.

Mwenyekiti Kijiji Cha Olbomba Kashira Alais amesema wamekuwa wakitumia maarifa ya asili katika uhifadhi hata hivyo wanataka serikali kutambua maarifa hayo ili kupunguza migogoro.

Masono Ole Malendai amesema wanawake wamekuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi lakini wanaamini suluhu ni matumizi ya maarifa asilia.

Afisa Mifugo Longido Nestor Daqarra

Mradi wa uhifadhi mazingira kwa maarifa asilia unatekelezwa na shirika la wanahabari la kusaidia jamii za pembezoni la MAIPAC kwa kishirikiana na CILAO na unataratibiwa na Jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF).

By Jamhuri