Rais Valdimir Putin ameonya jana Jumatano kwamba Urusi inaweza ikawapatia mataifa mengine makombora ya masafa marefu kwa ajili ya kushambulia maeneo lengwa kwenye mataifa ya magharibi.

Hatua hii amesema itakuwa ni jibu ya ruhusa iliyotolewa na washirika wa jumuiya ya NATO kwa Ukraine kutumia silaha inazopewa na magharibi kuishambulia Urusi.

Putin aidha amethibitisha kwa mara nyingine kuhusu utayari wa kutumia sialaha za nyuklia ikiwa kutakuwa na kitisho chochote kwenye eneo lake.

Amesema hatua hiyo ya magharibi itazidi kudhoofisha usalama wa kimataifa na kuchochea matatizo makubwa, na itaashiria wazi ushiriki wake wa moja kwa moja kwenye vita kati ya Urusi na Ukraine na kuongeza kuwa wana haki ya kuchukua hatua kama hiyo.

Putin alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo vya magharibi, jambo ambalo analifanya kwa nadra mno tangu alipoivamia Ukraine.