Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkoa wa Pwani, umezindua mfumo wa usafirishaji wa dharura kwa wajawazito waliojifungua na watoto wachanga (M MAMA)katika kituo cha kuratibu mawasiliano ya rufaa hospital ya mkoa Tumbi, Pwani.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mgeni Rasmi Katibu Tawala mkoa wa Pwani,Savera Salvatory, alieleza mfumo huo ni moja ya mkakati wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutokana na changamoto ya ukosefu wa usafiri wa dharura kutoka kituo kimoja hadi kituo kingine cha viwango vya juu.

Alieleza, kwa mkoa wa Pwani kuna magari ya kubeba wagonjwa wa dharura 20 ambapo yanatoa huduma kwa vituo 431.

“Idadi hii haitoshelezi kabisa mahitaji yetu,na pia ukosefu wa usafiri wa dharura kutoka hata kwenye ngazi ya jamii mpaka kwenye vituo vya kutolea huduma”

Savera alifafanua, kutokana na sababu hizo mfumo huo ni muhimu na utakuwa msaada kwa jamii, hivyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuanzisha mpango huu tangu auzindue rasmi April 6 mwaka 2022.

“Kama tunavyofahamu mama zetu wameumbika kutunza mimba na kujifungua na ndiyo mwanzo wa maisha ya binadamu, Kwahiyo Hakuna huduma muhimu na yenye baraka duniani kama kumhudumia mama kwenye kipindi cha ujauzito na kuhakikisha anajifungua salama”

Nae mratibu wa M MAMA Mkoani Pwani, Alfred Ngowi alieleza waratibu 32 wa usafirishaji wa huduma za dharura wamepata mafunzo ya jinsi ya kuratibu mfumo huo ikiwa ni sanjali na timu ya uendeshaji huduma za afya mkoa, halmashauri, hospital na waratibu wa M MAMA.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Benedicto Ngaiza, anaeleza utambuzi wa madereva watakaosaidia katika usafirishaji wa dharura ulifanyika na madereva 140 wameweza kupatikana kutoka kwenye halmashauri zote na kusaini mkataba.

Awali Mkurugenzi Mkazi wa Vodafone Foundation Tanzania, Dolorosa Dancan aliishukuru Serikali kwa kuipa thamani na kushirikiana na Sekta Binafsi ,ili kuleta maendeleo nchini.

Mfumo huu ulitambulishwa mkoa wa Pwani 15 ,Juni 2023 , mpango huu unatekelezwa na Serikali kupitia uongozi wa Mkoa, halmashauri pamoja na wadau wa Pathfinder International,Touch Foundation na Vodacom Tanzania ambao wanasaidia kujenga uwezo namna ya kuendesha mpango huo.

By Jamhuri