Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Njombe

Mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Mgalo iliyopo mkoani Iringa Carister Haule(15),mkazi wa kijiji cha Lifua, wilayani Ludewa mkoa wa Njombe, amefariki dunia kwa kupigwa na radi wakati akifungulia mbuzi chini ya mti.

Mbali ya tukio hilo pia nyumba 16 zimeezuliwa paa na mvua iliyoambatana na upepo mkali katika tukio lililotokea Desemba 17,majira ya saa 11 jioni,katika kijiji cha Lifua kata ya Luilo.

Kaimu katibu tawala ya Wilaya ya Ludewa Daniel Ngalupela amesema kuwa marehemu amepigwa radi akiwa akifungulia mbuzi waliokua wamefungwa kwenye mti mkubwa wa mkorosho ambapo mbuzi nao walikufa.

Ngalupela amesema kuwa kati ya nyumba 16 zilizoezuliwa na upepo mkali,nyumba sita zimebomoka kabisa.

“Kitu cha kwanza kama wilaya tumefanya tathimini ya athari zilizojitokeza baada ya hapo kukutana na wadau kwa ajili ya kuwachangia ili kuwasaidia kupata vifaa kama mabati,mbao ili kuweza kuzirudisha hizo nyumba katika hali ya kawaida”amesema Ngalupela.

Amesema jitihada ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuwaomba baadhi ya wananchi kuwahifadhi watu ambao wamepata madhara.

By Jamhuri