Kikao cha Baraza la Ushauri la Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichokuwa kifanyike wiki iliyopita, kilishindikana baada ya kuchafuka kwa “hali ya hewa”.
Hali ya mambo ilibadilika baada ya mpango wa Rais Jakaya Kikwete wa kuwatumia kama njia ya yeye kukwepa lawama za “kuwakata wagombea, kujulikana.
Wazee wamelazimika kujipanga upya, na sasa taarifa zinasema kikao hicho kitafanyika Julai 4, mwaka huu.


Hayo yakiendelea, Idara ya Habari (MAELEZO) imeliandikia barua Gazeti la JAMHURI, hoja kuu ikiwa kutaka maelezo ya kwanini Wakurugenzi wa Usalama wa Taifa, na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), waalikwe kwenye kikao cha kujadili wagombea urais kupitia CCM.
Imekuwa ikijulikana kuwa Usalama wa Taifa umekuwa na dhima halali ya kuwachambua na kuwatambua wagombea wa nafasi nyeti katika taasisi zote na serikalini, lengo likiwa kuiepusha nchi kuongozwa na watu wasiokuwa na sifa za uraia na uzalendo.
Kadhalika, Takukuru kupitia kwa Mkurugenzi wake, mara zote imekuwa ikisema haina woga wa kupambana na rushwa kwenye uchaguzi ndani ya CCM na vyama vingine vya siasa kwa sababu kazi yake ya kukabiliana na rushwa haina mipaka. Kuahirishwa kwa kikao cha Wazee kunaelezwa kwamba kulitokana na kuvuja kwa mkakati wa kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea kutokana na shinikizo, huku mlengwa mkuu akiwa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.


Aidha, mwingine anayelengwa ni Mbunge wa Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Kuna madai kwamba kuachwa kwa mgombea mmoja na kumpitisha mmoja kunaweza kuwa na athari kubwa za kukigawa chama. Kumejengwa taswira ya kuuaminisha umma kuwa wanasiasa hao ndiyo wenye kambi zenye nguvu kuliko kambi nyingine.
Hata hivyo, Wazee wenyewe wanatajwa kutokuwa wamoja kutokana na tofauti za mitazamo hiyo, hasa linapokuja suala la sifa za mtu mwenye uwezo wa kukabiliana na upinzani nje ya CCM.
Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu, John Malecela, na Makamu Mwenyekiti mstaafu, Pius Msekwa, wanatajwa kuwa mwiba mchungu kwa Lowassa.
Wote, kwa nyakati tofauti wametajwa kuonja shubiri ya nguvu za Lowassa. Malecela ni mwaka 2005 kipindi ambacho Lowassa aliongoza kambi iliyompa ushindi Rais Jakaya Kikwete. Msekwa, anaumia kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuzidiwa na nguvu za Lowassa pale alipokengeuka ahadi yake na kurejea kwenye kinyang’anyiro cha uspika. Kwenye mchuano huo Lowassa alishiriki kwenye kampeni iliyomwezesha Samuel Sitta, kumwangusha vibaya Msekwa.


Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), Rajab Luhwavi, ameshapewa maelekezo ya kuitishwa kwa kikao cha Julai 4.
Katibu wa Baraza hilo la Wazee, Msekwa amethibitisha kuandaliwa kwa kikao hicho baada ya kukwama wiki iliyopita, lakini amekataa kutaja siku mahsusi na mahali kitakapofanyika.
Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM linaundwa na wajumbe sita ambao ni wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu Taifa wa chama hicho. Viongozi hao ni Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi (Mwenyekiti), Msekwa (Katibu). Mwenyekiti na Rais mstaafu Benjamin Mkapa (Mjumbe); Makamu Mwenyekiti na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume; Makamu na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour; na Mzee Malecela.


Hali ya mambo ndani ya CCM inazidi kuwa tete, huku mwenye kuonekana kuwa na wakati mgumu akiwa ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Ushauri mwingine unaotarajiwa kufikishwa na hata kufikiriwa na Wazee kwenye kikao chao ni kuangalia uwezekano wa kuondoa ‘automatically’ kwa majina sita kati ya 40 ya walioomba urais. Majina sita ni ya makada waliopewa adhabu ya kufungiwa. Hofu inayowapata ni kwamba kwenye fomu za kuomba ridhaa, kuna kipengere kinachomtaka anayeijaza aeleze kama alishaadhibiwa ndani ya Chama na sababu za kuadhibiwa kwake. Kama hilo litafanywa, basi watakaoumia ni Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Mbunge wa Sengerema na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Membe na mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira ambaye ni Mbunge wa Bunda na Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika.


Aidha, kwenye swali linalouliza kama mgombea aliwahi kukihama chama na sababu zilizomfanya akafikia uamuzi huo, wagombea wawili wanaweza kuumia moja kwa moja. Nao ni Wasira na Makongoro Nyerere ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wote walijiunga katika chama cha NCCR-Mageuzi na kuwa wabunge. Wasira (Bunda) na Makongoro Jimbo la Arusha.
Lakini kwenye kundi hilo, kama Wazee na vikao vya uamuzi vitaamua kuchimbua mambo, basi ni wazi kuwa Sitta, naye atatupwa katika hatua za awali kwani anahusishwa na kukianzisha Chama cha CCJ akiwa na aliyekuwa Mbunge wa Kishapu, Fredy Mpendazoe. Wengine wanaotajwa tajwa kwenye CCJ ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye. Naye hakutangaza nia ya kuwania urais.
Pia Wasira anaweza kujikuta akijikwaa kwenye kipengere hicho kwani kuna madai ya kuwa alipojitoa NCCR-Mageuzi, kabla ya kurejea CCM, alishiriki kuanzisha chama kingine cha siasa.
Kikwazo kingine ni kitendo chake cha kutiwa hatiani kwa makosa ya rushwa akiwa Mbunge wa Bunda, hali iliyoilazimu Mahakama Kuu kutengua ubunge wake.


 “Tutaangalia namna ambavyo wamejaza fomu zao. Maana mle ndani kuna masharti yanayompa mtu sifa za kugombea,” kinasema chanzo chetu kutoka Kamati ya Maadili.
“Kuna wanaowadanganya hawa…wakisema ooh wana ripoti nzuri, wengine wakiwatishia kwamba wana ripoti mbaya. Hayo yote yatafahamika Dodoma, watu wasubiri, lakini wajiandae kisaikolojia kwa wale wanaowapenda zaidi. Hofu kubwa ni kuwa wasije kuvuruga chama wakati huu wa uchaguzi,” anaongeza.
Moja ya kazi za Baraza la Wazee ni kuwapitia wagombea kulingana na maswali yaliyoko kwenye fomu.
Kuna sehemu mgombea anatakiwa kuelezea ukada wake katika chama kama vile kuwa mwanachama tangu kwa ‘wazazi’ wa CCM ambao ni TANU (Bara) na Afro Shiraz (ASP).
“Watajaza nini? Mimi sijui, lakini hapo ndipo Kamati ya Maadili na Kamati Kuu watakapopata nafasi ya kuwashughulikia,” kimesema chanzo chetu.
 
Stephen Wasira
Wasira ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya CCM 2015-2020 licha ya kuandamwa hivyo, anaelezwa kuwa ni kada mwenye nguvu za ushawishi.
Ana rekodi nzuri ya kiutendaji katika awamu zote alizopitia kuanzia ya Mwalimu Nyerere. Uchapakazi, ufuatiliaji na usimamizi ni moja ya sifa kubwa za Wasira kwa watu waliofanya naye kazi. Kwa sasa ni miongoni mwa mawaziri mahiri wa Rais Jakaya Kikwete.
Pamoja na hayo ana udhaifu katika kutoa kauli za vitisho na zinazoashiria udikteta, kudharau haki, hoja na hata madai ya watu wengine kwani alipata kushauri vyama vya siasa vinavyotumia haki ya kuandamana, kufutwa.
 
January Makamba
Makamba aliyezaliwa Januari 28, 1974 mkoani Singida. Ni mtoto mkubwa kati ya watoto wanne wa Mzee Yusuph Makamba. Kwa sasa January ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Hakuna ubishi kwamba nguvu ya January ni kwa vijana ambao kwa mwaka huu wamejitokeza kwa wingi wakiwa na ndoto kama sera za mwanasiasa huyo. Elimu ya January na uzoefu wa kufanya kazi serikalini na Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam alikopata fursa ya kuzunguka nchi hivyo kujifunza matatizo ya Watanzania.
Mbali ya hilo, January ana nguvu ya baba yake, ambaye ameshatangaza wazi kumuunga mkono. Mzee Yusuph Makamba ana mtandao mkubwa na anaweza kutumia mtandao huo kumsaidia mwanaye.
Pamoja na hayo, January anaelezwa kuwa ni kiongozi mwenye msimamo mkali wa kuijenga jamii mpya ya Tanzania kama alivyowahi kuunga mkono kuua kwa risasi wala rushwa hadharani.
Kadhalika, itakumbukwa kwamba katika Bunge Maalumu la Katiba (BMK), January aliwachukiza vijana wengi wanaomuunga mkono baada ya kuonekana akitetea hoja za Serikali yake hata kama hazikuwa na mashiko.
 
Makongoro Nyerere
Kwa upande wa Makongoro, tafiti zinaonyesha kwamba amekuwa akifanya mambo ambayo husaidia watu wengine na hata taifa lake. Yaani pamoja kwamba ni mtoto wa Rais Nyerere, lakini hupenda ‘kujichanganya’.
Mfano halisi ni pale alipoona maisha ya kubaki nyumbani si mali, badala yake alijiunga jeshini kama mmoja wa vijana waliohitaji kulinda taifa lao dhidi ya nduli Idd Amin katika Vita ya Kagera.
Makongoro haonekani kutaka kujitofautisha na jamii japo kwa mavazi hali iliyowashangaza hata watu wengi pale alipoamua kuhamia NCCR-Mageuzi, mwaka 1995 na kuacha CCM – chama kilichoasisiwa na baba yake, Mwalimu Julius Nyerere. Alipambana na kushinda ubunge Arusha bila kusaidiwa na baba yake. Makongoro Nyerere ni mtoto wa Nyerere anayefahamika, kutajwa na kuonekana kuliko watoto wengine wote hasa ushiriki wake katika masuala ya siasa na hata uongozi ndani ya CCM.
 
William Ngeleja
 Katika shughuli zake za ajira na siasa, William Ngeleja amewahi kuwa karibu sana na Lowassa, na hadi leo. Kwa hiyo, anaujua vizuri mtandao wa ushindi ndani ya CCM hasa kwa sababu alishiriki pia shughuli kama hiyo wakati wa kumpigania Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005.
Hakuna ubishi kwamba nguvu ya Ngeleja inatokana na umri wake, kwani anaonekana bado kijana na CCM itahitaji kupitisha mgombea mwenye umri unaolingana ambaye ana kariba inayoweza kuwavutia vijana na watu wengine.
Miaka 20 iliyopita, Ngeleja amekuwa mtumishi wa Serikali na katika mashirika binafsi na ya kimataifa kama mwanasheria. Uzoefu huo una maana kuwa anaifahamu vizuri nchi na mazingira ya kazi katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Nguvu nyingine ya Ngeleja inapatikana kwenye taaluma yake ya sheria kwani mara nyingi viongozi wanasheria wanatarajiwa kujiamini na kutenda masuala ambayo yanaweza kutohojiwa kirahisi.
Wizara ya Nishati na Madini kwa takribani miaka mitano na nusu, shida ya Ngeleja ni kuwa karibu na wanasiasa wanaotajwa vibaya na wenye taswira hasi katika jamii.
 
Edward Lowassa
Kwa upande wa Lowassa nguvu zake ni umaarufu ikilinganishwa na wagombea wengine wote ndani na nje ya CCM mwenye uwezo wa kirasilimali watu na fedha. Lowassa na mtandao wake wana rasilimali za kutosha kuendesha harakati hizi. Kwa mujibu wa mchambuzi wa wanasiasa nchini, Julius Mtatiro anamwelezea Lowassa hivyo akirejea mfumo wa chama hicho kwa sasa akisema kuwa kwa siasa za CCM iliyowaweka kando wakulima na wafanyakazi, rasilimali ni kila kitu.
Lowassa ana nguvu kwa sababu ya kuwahi kuwa Waziri Mkuu na kuijua kwa undani mifumo ya uendeshaji wa nchi na hata kuisimamia. Ushawishi wake kwa mifumo hiyo umeendelea hadi sasa.
Taarifa kutoka ndani ya asasi mbalimbali za Serikali zinasema kwamba vyombo kadhaa vya dola vimegawanyika kwa sababu ya kumuunga mkono kutokana na kuonyesha misimamo ya kiuongozi na kuthubutu kwingi kunakotakiwa kufanywa na mkuu wa nchi.
Lowassa ni miongoni mwa vinara wanaojua njia zilizompa madaraka Rais Kikwete mwaka 2005. Mtu kama Ngeleja hamfikii Lowassa kwa kutambua njia hizo ingawa naye anajua ‘vichochoro’.
Tatizo la Lowassa ni kuwa karibu mno na watu wenye majina yenye taswira zinazotia shaka. Wale wanaotajwa kuingia kwenye kashfa za ufisadi au kuwa na marafiki wakubwa wenye pesa na matajiri kupindukia.
 
Bernard Membe
Kwa upande wa Membe, turufu zake muhimu zaidi ni tatu. Kwanza, nafasi yake kama Waziri wa Nje inamweka karibu sana na Rais Kikwete kwani wanasafiri pamoja takriban katika kila ziara ya Rais nje ya nchi. Huhitaji kuwa mdadisi kufahamu kuwa watu wanaosafiri pamoja kwa miaka 10 mfululizo wana ukaribu kiasi gani.
Pili, kuna taarifa zisizo rasmi kuwa Membe anaungwa mkono na familia ya Kikwete. Katika moja ya mahojiano, mmoja wa watoto wa Kikwete, Ridhiwani, alikiri bayana kuwa anadhani Membe anaweza na anafaa kuwa Rais. Siasa za kifamilia zinaweza kubadilika lakini kwa angalau kwa sasa hali ipo hivyo.
Tatu, Membe ni ‘shushushu mstaafu.’ Pengine ni vigumu kuelezea kwa undani umuhimu wa kigezo hiki, lakini kwa kifupi, ni vigumu sana kwa mwanasiasa kuingia Ikulu pasi kuungwa mkono na Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi husika (angalau katika ‘demokrasia changa’). Mashushushu, kama watumishi wengine wa vyombo vya dola, wana tabia moja ya kumuunga mkono ‘mwenzao.’
Kwa hiyo licha ya uwezo mkubwa wa kifedha wa Lowassa (tukiweka kando kukanusha kwake kuwa yeye si tajiri), Membe anaweza kumshinda kwa mbinu.
 
Frederick Sumaye
Sumaye ni Waziri Mkuu mwenye rekodi ya aina yake kwani kati ya wote walioshika wadhifa huo kuanzia Mwalimu Julius Nyerere, ni pekee aliyeshika wadhifa huo kwa miaka 10 chini ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa.
Alipata nafasi hiyo kutokana na uwezo wake wa uongozi alionyesha tangu akiwa Naibu Waziri alionyesha utulivu wa hali ya juu katika majukumu yake. Hakupenda kufanya mambo mengi, kwa wakati mmoja. Sumaye ni mtu asiyependa umaarufu usio na tija. Ni kiongozi anayeamini kuwa kazi aliyokabidhiwa akiifanya vizuri inatosha kumpeleka ngazi ya juu zaidi kwa kutumia taratibu za haki.
Alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1995, wabunge wengi walishangazwa kwani hakuwa waziri maarufu katika kipindi cha Mwinyi na alionekana kama mtu wa kawaida. Nchi ambayo ina matatizo kama Tanzania inaweza kuhitaji Rais mwenye kariba ya namna ya Sumaye.
Wengi wanakumbuka hali ilivyokuwa katika sakata la mauaji ya wakulima Kilosa ambako Sumaye alipofika Kilosa aligundua kuna udhaifu mkubwa kwa Mkuu wa Wilaya. Baada ya kusikiliza mgogoro alitoa uamuzi papo hapo kumsimamisha kazi aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo, kwa kushindwa kushughulikia tatizo, kwa wakati.
Ila tatizo lake ni ulalamishi hasa akiilalamikia CCM kama chama kinachoendeshwa kwa rushwa lakini anasahau kuwa miaka 10 tu iliyopita yeye alikuwa mtu wa tatu kwa ukubwa katika nchi na alistaafu akikiacha chama chake na serikali vikiendeleza vitendo vya rushwa. Lakini pia hana alama aliyoiacha baada ya kuongoza miaka kumi.
 
Mizengo Pinda
Mizengo Kayanza Peter Pinda ana nguvu ya asili, ni kiongozi mtulivu na msikivu. Mawaziri wakuu wengi waliopita hapa nchini si watu wa kusikiliza watu kwa urahisi.
Bila shaka atafanya hivyo kama akipewa ridhaa kwani hata bungeni ameweka utaratibu wa kupokea na kujibu maswali ya moja kwa moja kutoka kwa kuanzia kiongozi wa kambi ya upinzani, wabunge wa upinzani na wengine wote wa CCM. Wengi wanaomfahamu watakubaliana na wachambuzi wa masuala ya siasa kwamba Pinda si mtu wa makuu wala mbwembwe, ni mtu asiyejikweza na kila mara anaishi maisha ya kawaida tofauti na mawaziri wakuu wengi duniani na hata baadhi ya waliopita hapa Tanzania.
Mwenyewe hujiita “mtoto wa mkulima”  mara nyingi hujichanganya na bado anasali kanisa lake la Hananasif anapokuwa Dar es Salaam.
Kashfa ya Escrow ni tukio pekee unaloweza kusema lingemtia doa katika wadhifa alionao hivi sasa. Kashfa zilimwendea kwa sababu ya nafasi yake ya Waziri Mkuu, lakini si kwa sababu alishiriki kukwapua fedha hizo.
Tatizo lake ni udhaifu mkubwa wa kuamua mara moja. Ameifanya Serikali ya Awamu ya Nne ionekane ina ombwe kubwa, ikizingatia kuwa mkuu wa nchi pia ana upungufu ambao ungeweza kuzibwa na waziri mkuu wake ambaye naye hatendi inavyopaswa.
Si hivyo tu, Pinda pia ana udhaifu mkubwa mambo yakimzidia, anakata tamaa na kuona hakuna suluhisho. Mwaka 2013, alipoulizwa bungeni kuhusu tabia ya vyombo vya dola kuzuia maandamano ya wananchi na kuwapiga wanaoandamana bila sababu, aliishia kusisitiza kuwa “watu hao lazima waendelee kupigwa”.
Hasira na pupa katika uamuzi na kukata tamaa kwake vilionekana pia wakati alipokuwa akitoa kauli ya Serikali juu ya mauaji ya albino. Pinda alijikuta ametamka kuwa wanaofanya hivyo nao “wauawe tu”.
Upole kupita kiasi ni udhaifu mwingine wa Waziri Mkuu anayemaliza muda wake. Pinda ni mpole mno kiasi kwamba duru za ndani ya Serikali zinasema kuna baadhi ya mawaziri wanatumia upole huo kumruka na kujifanyia mambo yao bila kibali chake.
 
Profesa Mark Mwandosya
Nguvu ya Profesa Mwandosya ambaye ni mtaalum wa masuala ya uhandisi wa umeme aliyetumia utaalamu wake kuandika mambo mengi yanayohusu nishati na hata maendeleo yatokanayo na nishati.
Nguvu nyingine ni kufanya kazi Tanzania kwa muda mrefu kushinda wasomi wengine kama yeye wanaotafuta urais. Kwa miaka 40, amekuwa ama akifundisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, akiongoza wizara katika wadhifa wa Katibu Mkuu, akiwa mbunge na au waziri.
Profesa ana sifa ya utulivu na busara. Profesa Mwandosya si mtu wa kubeba mambo kwa pupa na kusimamia uamuzi wake huku ukiwa hauna tija. Ni mtu anayehitaji kila kitu kifanywe kwa utaratibu na kwa kuelewana.
Hataki kuishi maisha ya anasa, yasiyo na maana na ambayo haoni faida yake, lakini Profesa Mwandosya ni mmoja wa wanasiasa wapole sana. Utulivu na upole uliopitiliza ni vitu viwili tofauti.
Utulivu ni sifa kubwa ya kiongozi, lakini upole uliopitiliza ni udhaifu mkubwa kwa kiongozi. Mawaziri wengi waliofanya kazi na Profesa Mwandosya, wanasema ni mpole na anapoona mambo yamemzidia huwa na tabia ya kukaa kimya. Tatizo la afya yake linaweza kuwa sababu za kutompa nafasi kubwa.
 
Dk. John Magufuli
Kwa upande wa Dk. Magufuli ni mwanasiasa mwenye elimu ya kutosha akiwa na sifa nyingine za kushika wadhifa fulani, ana nafasi kubwa ya kufikiriwa kuliko yule ambaye hana elimu. Katika hili Dk. Magufuli amejizatiti na amebobea.
Hakuna ubishi kwamba elimu yake ikichanganywa na umri vinamfanya awe mgombea wa umri ambao unakubalika hasa kutokana na kukaa madarakani kwenye wizara kwa muda mrefu (miaka 20). Dk. Magufuli ana umakini na uwezo wa kusoma na kuchambua nyaraka, lakini Dk. Magufuli ana tabia ya kukurupuka kiasi kwamba kuna wakati inaonekana uamuzi wake hauna tija. Kwa mfano, kushiriki mpango haramu wa uuzaji wa nyumba za Serikali ambao ulilalamikiwa mno wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
 
Balozi Dk. Augustine Mahiga
 Dk. Mahiga naye ni msomi mwenye weledi na uwezo mkubwa hasa katika masuala ya diplomasia ya uchumi kutokana na kufanya vema katika masomo tangu darasa la 12 hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ni shushushu mahiri.
Inaelezwa kuwa ni miongoni mwa watu anayeona kwamba suala la Serikali tatu linajadilika. Alisisitiza kuwa Rasimu ile ya Kwanza imebeba majibu na kero zote za Muungano. Kiongozi huyu ana msimamo wa kipekee.
Dk Mahiga amepata kufanya kazi za kuteuliwa na kushika madaraka tangu Serikali ya Mwalimu Nyerere, Mwinyi, Mkapa na sasa Kikwete ambako pia alifanya kazi Umoja wa Mataifa (UN).
Udhaifu mkubwa wa Balozi Mahiga ni kutofahamika kwa wananchi wa kawaida. hivyo kuwa na nafasi ndogo ya kupata uungwaji mkono na makundi yaliyogawanyika ndani ya chama hicho.
 
Jaji Augustine Ramadhani
Tangu Desemba, 2013, Augustino Ramadhani amekuwa akifanya kazi za kichungaji katika Kanisa la Anglikana, Zanzibar, mara baada ya kustaafu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania huku akiwa na sifa kuu tano za kuwania urais.
Ni Mzanzibari, ni Mkristo na vigumu kukutwa na doa lolote katika utendaji wake, hana makundi wala ukwasi mkubwa wa fedha. Akiwa Jaji Mkuu, hakuweza kuficha mapenzi yake kwa mchezo wa mpira wa kikapu na alikuwa mlezi wa chama cha mchezo huo ngazi ya Taifa.
Ni wakati huo pia ndipo alipoanza kufahamika kama mpiga piano wa kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Alban lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Ni askari aliyestaafu katika ngazi ya Brigedia Jenerali na pamoja na kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na Tanzania, amehukumu pia katika Mahakama ya Kijeshi (Court Marshall).
Jambo ambalo watu wengi hawalifahamu ni kwamba babu wa Jaji Ramadhani, Mzee Augustino Ramadhani, alikuwa mwasisi wa Chama cha African Association (AA) ambacho baadaye kilikuja kuwa sehemu ya muungano uliounda Chama cha ASP, ambacho sasa ni CCM.
 
Profesa Sospeter Muhongo
Kama kuna waziri ambaye amepata kushika Wizara ya Nishati na Madini kwa muda mfupi na kuonyesha mafanikio makubwa kabisa, hakuna wa kumpita Profesa Muhongo ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa miamba (jiolojia).
Hakuna ubishi kwamba Profesa Muhongo ni Mtanzania mwenye upeo wa hali juu hasa masuala ya miamba, nishati na madini katika ngazi ya kimataifa. Weledi wake hufananishwa na Profesa Ibrahim Lipumba.
Profesa Muhongo ni mchapakazi ambaye siku zote hutaka mabadiliko.
Ni msimamizi mzuri wa kazi na amesimamia ongezeko la usambazaji umeme vijijini na mijini na amesimamia punguzo la gharama za kuunganishiwa umeme kote huko. Japokuwa miradi mingi kati ya hii ilianzishwa chini ya mtangulizi wake, William Ngeleja, lakini Watanzania ni mashahidi kuwa utekelezaji wa hali ya juu ulisimamiwa na Profesa Muhongo. Amewezesha Watanzania wengi kupata udhamini wa masomo nje ya nchi katika fani za mafuta, madini na gesi.
Tatizo la Profesa Muhongo si mtu wa diplomasia pamoja na kuishi nje ya nchi muda mrefu ambako amekutana na watu wa kila namna. Hii ni kwa sababu ya kutoa majibu makali pindi anapolemewa na maswali.
Hadi mwishoni mwa wiki, wana-CCM 40 walikuwa wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania urais. Nao ni:-

1.Edward Lowassa
2.Frederick Sumaye
3.Bernard Membe
4.Stephen Wasira
5.January Makamba
6.William Ngeleja
7.Mizengo Pinda
8.Boniface Ndengo
9.Eldefonce Bilohe
10.Profesa Mark Mwandosya
11.Profesa Sospeter Muhongo
12.Lazaro Nyalandu
13.Dk. Titus Kamani
14.Dk. Harrison Mwakyembe
15.Dk. Asha-Rose Migiro
16.Dk. Mohamed Gharib Bilal
17.Dk. John Magufuli
18.Dk. Mzamini Kalokola
19.Dk. Hassy Kitine
20.Dk. Mwele Malecela
21.Dk. Hamis Kigwangalla
22.Balozi Amina Salum Ali
23.Balozi Agustino Mahiga
24.Balozi Ali Karume
25.Balozi Patrick Chokara
26.Mwigulu Nchemba
27.Mathias Chikawe
28.Luhaga Mpina
29.Amos Siyantemi
30.Samuel Sitta
31. Godwin Mwapango
32.Peter Nyalile
33.Leonce Mulenda
34.Makongoro Nyerere
35.Amos Robert
36.Monica Mbega
37.Jaji Augustino Ramadhani
38.Maliki Maruku
39.Ritha Peter
40. Helena Elinawinga
 
Habari hii imeandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vikiwamo vya Mchambuzi wa masuala ya Siasa, Julius Mtatiro.

 
7276 Total Views 4 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons