Rais Dk. John Magufuli amezindua rasmi ujenzi wa mradi wa umeme wa maji Mto Rufiji.

Mradi huo utakapokamilika utazalisha megawatt 2,115 za umeme. Akizungumza katika uzinduzi huo uliohusisha uwekaji wa jiwe la msingi, Rais Magufuli amesema kufanikishwa  kwa mradi huo ni ukombozi wa Tanzania kiuchumi.

Ujenzi wa mradi huo utatekelezwa ndani ya miezi 36 na Sh trilioni 6.5 zote zikiwa ni fedha zinazotokana na makusanyo ya kodi nchini zitatumika kukamilisha mradi huo.

Rais Magufuli ameeleza kuwa mradi huo utalipeleka taifa kwenye uchumi wa viwanda huku akisisitiza kuwa sera ya viwanda haiwezi kutekelezwa kwa uhakika kama hakuna umeme wa kutosha.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, uzalishaji wa umeme kutoka katika mradi huo utashusha gharama za umeme.

 “Hapa palikuwa na ulaji wa watu, wewe unafikiri hao watu wanaweza kufurahia wakiona sisi tunataka kupaendeleza? Nashukuru Mungu, ndoto ya Mwalimu Nyerere ya tangu miaka ya ‘70 , leo inakwenda kukamilika,” amesema.

Mradi huo wamepewa makandarasi kutoka kampuni za ubia – Arab Contractors na Elsewedy Electric za Misri.

Ameeleza kuwa wanaodai mradi huo utaharibu mazingira si wakweli, kwa kuwa eneo la Selous lenye ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 ni asilimia tatu tu ya eneo lote ndilo litakalotumika kwa ajili ya mradi huo.

Amesema hekta 64,866 za kilimo cha umwagiliaji zinatarajiwa kulimwa kutokana na uwepo wa mradi huo.

Kwenye uzinduzi huo, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuligawa eneo hilo katika maeneo ya uwindaji na hifadhi ya taifa.

Ameeleza kuwa Selous ina zaidi ya kilometa za mraba 50,000, hivyo kuwa mbuga kubwa kuliko zote nchini ukilinganisha na Mbunga ya Ruaha yenye kilomita za mraba 20,000 ikifuatiwa na Serengeti yenye ukubwa wa kilomita za mraba 14,112 na Burigi – Chato yenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,702.

Pia, kwenye uzinduzi huo ameagiza dhahabu na fedha, vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 5 baada ya kurudishwa kutoka Kenya zitumike kujenga barabara kutoka Fuga ilipo Reli ya TAZARA kwenda eneo la mradi.

Amebainisha kuwa zaidi ya wafanyakazi 6,000 wanahitajika katika shughuli za ujenzi wa mradi huo na kuwataka wananchi walioko karibu na vyanzo vya maji katika mikoa ya Pwani na Morogoro kutunza vyanzo vinavyotengeneza Mto Rufiji unaomwaga maji yake Bahari ya Hindi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania kuiunga mkono serikali ili izidi kuwaletea maendeleo.

Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge katika uzinduzi huo, amesema Bunge linamwelewa Rais Magufuli na linaunga mkono juhudi za kuliletea maendeleo taifa.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema mradi huo utakamilika mwaka 2022 na utasimamiwa na Watanzania wenyewe.

Mhandisi wa Shirika la Umeme la Taifa (Tanesco), Steven Manda, amesema mradi huo umegawanywa katika maeneo manne na kwamba bwawa linachukua asilimia 45 ya mradi wote.

Maeneo hayo ni eneo la kuingiza maji, jengo la mitambo na mitambo yenyewe (power house) na eneo la transformer 27 zenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kilovolt 16.5 utakaosafirishwa kwenda kwenye transformer zenye uwezo wa kupokea umeme wenye nguvu kiasi cha megawatt 400.

Amesema bwawa litakuwa na sehemu ya barabara yenye ukubwa wa mita 10 na mita za ujazo bilioni 73.2, na kwamba litachukua upana wa kilomita 914 na kina cha urefu wa mita 131. Amebainisha kuwa shughulli zote za kujenga bwawa na maeneo mengine ni asilimia 1.922 ya eneo lote la pori la Selous.

Msemaji wa Kampuni ya Elswedy Electric, Mhandisi Mohamed Elswedy, ameahidi Kampuni yake ya Elswedy Electric kuutekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa.

Mhandisi mwingine mbia katika mradi huo, Mohammed Saleh wa Arab Contractors, amesema idadi ya wafanyakazi katika kampuni yake ni takriban 70,000 na imekwisha kufanya kazi za ujenzi ndani ya Misri na nje ya Misri.

Katika hatua nyingine, utafiti uliofanyika Machi mwaka huu ukiongozwa na Salehe Pamba, Dk. Abubakar Rajabu, Abdulkarimu Shah, Dk. Magnus Ngoile na Dk. Thomas Kashililah kuhusu mradi huu kuharibu mazingira umebaini kutokuwapo kwa athari dhidi ya mazingira kama ilivyopata kuelezwa awali.

Ripoti hiyo inaonyesha mradi kuwa wa manufaa makubwa kuliko athari zake – uchafuzi wa mazingira na kuharibika kwa bioanua zinazotajwa na mashirika ya kimataifa.

Utafiti huo umeainisha kuwa kigezo cha kelele ndani ya mbuga hakiwezi kuzuia mradi huo kutekelezwa, kwani katika Mbuga ya Selous kuna safari za ndege 38 huku safari 33 zikihusika ndani ya mbuga hiyo.

Uchunguzi huo unaonyesha kuna hoteli 11 na maeneo ya kupokea wageni 284 kwa siku na safari za magari katika pori hilo, lakini hakuna madhara kwa wanyama waliomo katika pori hilo.

Zaidi matokeo ya utafiti huo yanaonyesha mradi utaongeza na kuimarisha ulinzi ndani ya Mbuga ya Selous, ikiwa ni pamoja na kuongeza shughuli za utalii.

Vilevile utafiti unaonyesha utekelezaji wa mradi hautasababisha wanyama kutoweka kama inavyoelezwa wala shughuli za kitalii kuathirika katika eneo hilo.

1024 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!