Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezionya taasisi za Serikali zinazokwepa matumizi ya mabadiliko ya mifumo ya kisasa kwenye utendaji wao.

Amesema, kuna baadhi ya taasisi zinakiuka matumizi na miongozo ya mifumo iliyowekwa kisheria kwa utekelezaji na utendaji wa kazi zao, jambo alilolikataza mara moja kwani linakwamisha mipango na malengo ya Serikali.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi kwenye uzinduzi wa Mkakati wa Kidijitali wa Serikali na Mfumo wa kitaifa wa Bajeti na Matumizi Serikalini (BAMAS).

Amewaagiza viongozi wa taasisi hizo wakiwemo Makatibu wakuu na wakuu wa taasisi wanazozisimamia kuhakikisha wanapokea na kutumia mifumo ipasavyo kwa lengo la kujenga na kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, sheria, miongozo, pamoja na taasisi zilizopewa majukumu ya kusimamia masuala hayo.

“Nawaagiza viongozi wote wa Wizara, Idara, Taasisi za Serikali zote ikiwemo Mashirika na Taasisi za Kodi, Serikali Kuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kulisimamia agizo hili mara moja.” ameagiza Rais Dk. Mwinyi.

Dk, Mwinyi amesema, Serikali itapunguza hujuma zinazofanywa na wachache kwa kutumia hati na nyaraka za kughushi na kuongeza mifumo imara, itatoa taarifa zilizotibitishwa kidijitali.

Amewaagiza Wakala wa Serikali Mtandao kupitia Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kushirikiana na Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango, kutoa elimu kwa taasisi zote za Serikali na wananchi juu ya mkakati wa pamoja na matumizi ya Mifumo mipya ya serikali inayoendelea kuzinduliwa.

Ameeleza kuwa, mfumo huo pia utaimarisha sekta muhimu za kiuchumi, uwekezaji na ukusanyaji wa mapato nchini kwa kuzingatia mbinu na mikakati ya kuimarisha na kuendeleza sekta za utalii, uchumi wa buluu, kuharakisha utoaji wa huduma bora za jamii, ikiwemo bima ya afya, kuimarisha biashara hasa kwa raia wageni hawatolazimika kufika Ofisi za Serikali kufanya miamala au usajili wa biashara na kampuni zao badala yake popote walipo watafanya hivyo kwa muda mfupi kupitia njia za kidijitali.

Pia Rais Dk. Mwinyi ameongeza mfumo utarahisisha shughuli za usajili wa wanafunzi kwenye Skuli na vyuo vikuu, usajili wa ndoa, vizazi na vifo.

Akieleza, Mfumo wa BAMAS pia umeondoa changamoto za mifumo inayoendelea kutumika sasa ya ukusanyaji mapato (Isidore) na Mfumo wa Matumizi (Epicor) na kueleza kwamba BAMAS umeleta uwazi kwenye Bajeti na Matumizi Serikalini kwa kuwezesha Mifumo yote ya Malipo na Matumizi ya Fedha za Serikali kusomana kwa haraka na kwa ufanisi.

Alieleza matarajio yake kwa Mfumo wa BAMAS kwamba utaongeza nguvu ya udhibiti wa mali za Serikali, uwajibikaji kwa Watumishi na watendaji wa Umma na kuhakikisha fedha za Umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, aliiomba Serikali kuiongezea uwezo taasisi badala ya kuwa wakala wa Serikali Mtandao iwe Mamlaka ili kuiongezea ufanisi na usimamizi mzuri wa matumizi mtandao kwa taasisi zote za Serikali.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, amesema Mfumo wa BAMAS utaongeza ufanisi na utoaji wa huduma bora za Serikali pia utaunganisha pamoja sehemu ya mapato na matumizi ya Serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala Serikali Mtandao Zanzibar, Saidi Seif Said ameeleza kwa kipindi cha miaka miwili na nusu sasa wametengeneza na kusimamia mifumo 28 ukiwemo mfumo wa BAMAS na kueleza kwelekeo wa taasisi hiyo ni kuongeza kasi ya kutengeneza mifumo yenye nguvu zaidi ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa taasisi za Serikali.

Uzinduzi wa Mkakati wa Kidijitali wa Serikali na Mfumo wa Bajeti na Matumizi Serikalini (BAMAS) ulikwenda sambamba na kaulimbiu “Hatma yetu ipo viganjani mwetu”

By Jamhuri