*Aagiza Wakojani wawezeshwe

 mitumbwi Uchumi wa Buluu

*Ni Kisiwa chenye skuli ambayo

 wanafunzi wanasoma kompyuta

ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema atakitembelea Kisiwa cha Kojani, Pemba baada ya mfungo mtukufu wa Ramadhani.

Rais Mwinyi ametoa ahadi hiyo baada ya kuulizwa na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JAMHURI, Deodatus Balile, kuwa ni lini atakwenda Kojani baada ya awali wahariri kutembelea na kubaini fursa nyingi za uwekezaji zinazoweza kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi, ila ikawa kuna shida kidogo ya viongozi wa kitaifa kutotembelea eneo  hilo mara kwa mara.

“Nitakwenda Pemba baada ya mfungo wa Ramadhani,” alisema Dk. Mwinyi Machi 30, 2022 katika mkutano na vyombo vya habari, na alipoulizwa na Mwandishi Mwandamizi, Salim Said Salim, iwapo akienda Pemba atafika Kojani, akasema: “Nitakwenda Kojani.”

Awali, akijibu maswali mawili ya msingi, Rais Mwinyi amesema aliyoelezwa kuhusu Kojani na malalamiko kwamba hakuna gati au bandari ya uhakika kwa watu kusafiri na kusafirisha mizigo, amesema: “Lengo la msingi la mpango huu chini ya Uchumi wa Buluu ni kujenga miundombinu ikiwamo bandari. Kwa hiyo maeneo kama hayo (Kojani) tutajenga miundombinu itakayorahisisha biashara.”

Amesema kwa Zanzibar, eneo lote uvuvi ni biashara ya msingi, hivyo kujenga gati au bandari ya uhakika Kojani ni suala la msingi linalopaswa kufanywa. 

Alipoelezwa kuwa Kojani hakuna ushirika rasmi uliosajiliwa, hivyo wananchi yawezekana wasipatiwe mkopo usio na riba unaotolewa kutokana na fedha za Uviko – 19, Rais Mwinyi amesema wanaweza kupatiwa.

“Nimekwisha kuwaelekeza Wizara ya Uchumi wa Buluu na katika hili nitawaelekeza watu wangu, wahakikishe Kojani kama hawana ushirika au umoja rasmi wa vikundi, wawasaidie na kuhakikisha wanapata ushirika na wanakopesheka,” amesema.

Kisiwa hiki kwa kuingizwa katika mpango huu wa kupewa mikopo isiyo na riba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kitakuwa na nafasi za kumiliki boti za kisasa zinazotumia teknolojia ya kisasa ya GPS na Fish Finder na zitaongeza uwezo wa kuvua samaki wengi kuliko ilivyo sasa.

Mara kadhaa Rais Mwinyi amesema kuwa analenga kuongeza uwezo wa wavuvi kupata samaki kutoka wastani wa kilo mbili wanazovua sasa kwa kutumia mashua, ngarawa na mitumbwi isiyo na teknolojia hadi wastani wa kilo 1,000 kwa mvuvi mmoja kwa siku.

Hii inamaanisha kuwa uvuvi ukikua, Kojani inaweza kujenga kiwanda kikubwa cha samaki na kuanza kuwasindika kwa ubora wa kimataifa na wakaanza kuuzwa ndani na nje ya nchi. 

Hii itakuwa ni fursa muhimu kwa Wakojani wengi ambao wana utaalamu wa hali ya juu katika eneo la uvuvi na wakiongezewa teknolojia na vifaa vya kisasa, kisiwa hicho kitapiga hatua kubwa kiuchumi.

Kojani ipo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kisiwa hiki chenye ukubwa wa kilomita za mraba saba kina wakazi 13,000. Kisiwa hiki kilichojaa amani kinatia matumaini, kwa sababu katika miaka ya karibuni kimepata huduma za jamii za uhakika ikiwamo maji, umeme na shule.

Skuli ya Sekondari ya Kojani, Pemba, ni moja ya mfano, kwa sababu imejengwa kwa ghorofa na wanafunzi wake wanasoma somo la kompyuta kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. 

“Nilichoona hapa Kojani kimenitia matumaini. Wanafunzi wanajifunza masomo ya kompyuta ambayo sehemu nyingi za Tanzania wengi wanaziona wakifika chuo kikuu, lakini hapa Kojani wanazisoma katika ngazi ya sekondari, nadhani hili ni jambo muhimu,” amesema mmoja wa wahariri waliotembelea Kojani.

Kunradhi

Katika toleo Na. 547 la Machi 22-29, 2022, gazeti hili lilichapisha makala ambayo pamoja na mambo mengine ilieleza kuwa Rais wa mwisho kutembelea Kojani alikuwa Dk. Salmin Amour. 

Ukiacha hilo, mwandishi alikwenda mbali zaidi na kusema Kojani ni eneo ambalo dawa za kulevya zinauzwa bila kificho, maisha  ya wakazi wa kisiwa hiki hayaakisi karne ya 21, wasichana wengi wanaacha shule na kuolewa na wavulana wengi wanaacha shule na kukimbilia uvuvi.

Makala ilieleza kuwa kisiwa hiki ni kama kimetelekezwa au kutengwa na serikali kutokana na kutokuwa na miundombinu mizuri katika sekta ya afya, barabara, kutokuwapo pikipiki au gari kisiwani Kojani, na ilitaja kuwa kuna uchafu uliokithiri.

Wakaazi wa Kojani hawakufurahishwa na makala hiyo, ambapo walimwandikia barua Mhariri Mtendaji wa Gazeti hili la JAMHURI kuelezea masikitiko yao na wakataka makala hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘Ukifika Kojani utatokwa machozi’ irekebishwe.

Mhariri amezungumza na wananchi wa Kojani na kuwaelewa. Kwa mantiki hiyo, Gazeti la JAMHURI linaomba radhi kwa maeneo yaliyokuwa na ukakasi na yakawakwaza wananchi wa Kojani, kwa sababu nia haikuwa kubomoa, bali kujenga na kuhakikisha maisha ya watu wa Kojani yanazidi kuwa bora zaidi. Tunajenga nyumba moja, hatuna sababu ya kugombea fito. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri