Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imepokea zaidi ya bil 1.3/ kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuboresha upatikanaji huduma za afya kwa wananchi katika zahanati na vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

Hayo yamebainishwa jana na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Ramadhan Shaban Kapela alipokuwa akitoa taarifa kwa Watumishi na Madiwani wa halmashauri hiyo na waandishi wa habari.

Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujali maisha ya wakazi wa manispaa hiyo na kuwapatia kiasi hicho kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa ili kusambazwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na zahanati.

Amebainisha kuwa baadhi ya vituo vitakavyonufaika na vifaa tiba hivyo ni pamoja na Kituo cha Afya Tumbi, Misha na vinginevyo ikiwemo zahanati zilizoko pembezoni mwa manispaa hiyo.

‘Tunamshukuru sana mama yetu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kiasi hicho cha fedha, baadhi ya zahanati zetu na vituo vya afya vilikuwa na uhaba wa dawa na vifaa tiba, lakini sasa tatizo limekwisha’, ameeleza.

Mstahiki Meya amebainisha kuwa watasimamia ipasavyo vifaa hivyo ili kuhakikisha vinafikishwa katika maeneo yote yaliyokusudiwa na kuongeza kuwa watavilinda ili visitumike kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

Amesisitiza kuwa mkakati wa halmashauri hiyo ni kuendelea kuboresha miundombinu ya afya na kuongeza zahanati na vituo vya afya katika vijiji na kata zote ambazo hazina huduma hizo ikiwemo kujenga nyumba za watumishi.

Kapela alifafanua kuwa Manispaa hiyo pia inatarajia kunufaika na Mradi wa Benki ya Dunia (WB) unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu, hivyo wana matumaini makubwa ya kutatuliwa changamoto ya ukosefu wa nyumba za watumishi.

Aidha ameongeza kuwa ujio wa mradi huo na mikakati iliyowekwa na halmashauri hiyo vitasaidia kumaliza tatizo la mlundikano wa wagonjwa katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma hizo.

Mstahiki Meya amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Elias Kayandabila kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi zinazoletwa na Mheshimiwa Rais katika Manispaa hiyo.

Amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha mipango yote iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha inafanikishwa kwa kiwango kikubwa.

Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Rose Kilimba amempongeza Rais Samia na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwa kumaliza kero ya sukari kwa wakazi wa manispaa hiyo na sasa inapatikana nchi nzima kwa bei elekezi ya sh 3,000/- kwa kilo.