Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amedhamilia kufanya mageuzi katika kilimo cha Mkonge Kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kusambaza miche 6,991,200 ya mbegu za mkonge bure kwa wakulima wadogo katika Wilaya 16.

Mageuzi hayo yamefanya Tanzania kuwa Nchi ya pili Duniani kwa kuzalisha mkonge ikitanguliwa na Brazili.

Hayo yalibainishwa leo Agosti 16 Jijini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Saddy Kambona wakati akizugumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa odi hiyo a mwelekeo katika mwaka huu wa fedha.

Ametaja Wilaya zilizopatiwa mbegu hizo ni Korogwe, Muheza, Tanga, Mkinga, Handeni, Kilindi, Rorya, Bunda, Butiama, bariadi, Bagamoyo, Kisarawe, Mkuranga, Manyoni, Singida Vijijini na Mkalama.

Amesema Rais Dk.Samia ametoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo mipya ya kuchakata Mkonge na kufufua mitambo ya kuchakata mkonge ya mashamba ya Kibaranga Wilayani Muheza, Tanga na shamba la serikali la TPL lililopo Kata ya Bwawani Wilayani Arumeru, Arusha ambalo linasimamiwa na kuendeshwa na TSB.

“Mitambo hii itasaidia sana kuongeza uzalishaji wa Mkonge na hivyo kuwezesha kufikiwa kwa lengo la uzalishaji lililowekwa na serikali,”amesema.

Kambona amempongeza Rais Dk.Samia kwa hatua za kimageuzi alizochukua na anazoendelea kuchukua katika kuleta mageuzi ya kweli kwenye zao la mkonge na sekta ya kilimo kwa ujumla.

“Mwaka 2019 serikali ililiingiza zao la mkonge katika orodha ya mazao ya kimkakati na kufanya zao hilo kuwa zao la saba la kimkakati. Mazao mengine ya kimkakati ni Pamba, Tumbaku, Kahawa, Korosho, Chai, Michikichi.

”Zao la Mkonge likaingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025 ambamo limewekwa lengo la kuongeza uzalishaji kutoka tani 36,000 zilizokuwa zinazalishwa kwa Mwaka 2020 hadi kufikia tani 80,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025,”amesema

Kwa mujibu wa Kambona Serikali iliongeza lengo na kuiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka hadi kufikia tani 120,000 kwa Mwaka, ifikapo Mwaka 2025/2026.

Amefafaua kuwa hatua za serikali kuliingiza zao la mkonge kwenye orodha ya mazao ya kimkakati ilitokana na ukweli kwamba mahitaji na soko la mkonge limezidi kuimarika Duniani.

“Hii ni kutokana kugundulika kwa matumizi mapya ya mkonge na uzalishaji wa bidhaa mpya zitokanazo na mkonge kama vile vifaa vya ujenzi, Matofali,mbao, mabati, vigae), Sukari ya Mkonge, Pombe ya Mkonge, Karatasi maalum, Bio Gas, mbolea, Chakula cha mifugo , urembo, mabodi ya magari,”ameeleza