Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Asali ya Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa ubora Afrika, huku asilimia 96 ya sampuli ya asali ya inayozalishwa nchini zilizopelekwa maabala ya kimataifa nchini Ujerumani zilibainika kukidhi viwango vya ubora wa Kimataifa.

Hayo yamebainishwa jijini hapa Agosti 16,2023, na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Profesa Dos Santos Silayo wakati akizungumza na wandsishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa taasisi hiyo na mwelekeo katika mwaka huu wa fedha.

Amesema kupitia mashindano ya ubora wa asali zinazozalishwa barani Afrika, asali ya Tanzania ilinayozalishwa mkoani Tabora ilishika nafasi ya pili kwa ubora na kufanya kuendelea kuuzwa katika masoko ya nchi za Umoja wa Ulaya, Uarabuni na kwenye masoko mapya ya Poland na China.

“Wakala ulikusanya sampuli 70 za asali kutoka wilaya 34 na kuzipeleka kwenye maabara ya Kimataifa iliyopo nchini Ujerumani ambapo matokeo yalionesha kuwa asilimia 96 ya sampuli hizo zilikidhi viwango vya ubora wa Kimataifa.”

Ameongeza kuwa :”TFS imeanzisha mfumo unaoitwa “Honey Traceability System” ambao unafuatilia ubora wa asali kuanzia kwa mfugaji hadi pale inapoingia sokoni.”

Katika hatua nyingine Profesa. Silayo amebainisha kuwa TFS Inasimamia hifadhi za nyuki 20 zenye ukubwa wa hekta 39,444 ambapo Tanzania inakadiriwa kuwa na makundi ya nyuki milioni 9.2.

Amefafanua kuwa uzalishaji wa mazao ya nyuki umeongezeka kwa wastani wa tani elfu 33 kwa mwaka.

“Kama sehemu ya jitihada za kuongeza tija katika ufugaji nyuki nchini TFS ilianzisha mashamba matatu ya nyuki ambayo ni shamba la nyuki la Kipembawe katika Wilaya ya Chunya lenye ukubwa wa hekta 20,728, pia umeendeleza mashamba ya nyuki ya Mwambao (Handeni – Kilindi) na Kondoa-Manyoni lililopo katika Wilaya za Kondoa na Manyoni kwa kuanzisha manzuki mpya 14,”ameeleza

Kwa mujibu wa Profesa. Silayo amesema wakala umetoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki kwa wafugaji nyuki 1,998 kutoka katika vijiji 40.

ONGEZEKO LA WATALII

Kamishna huyo ameeleza kuwa kufuatia juhudi za serikali ikiwemo ubunifu wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuandaa filamu ya “Tanzania the Royal Tour” ambayo imeitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi kwa kiasi kikubwa, TFS imejipanga kutumia fursa hiyo kuongeza tija katika uhifadhi, utalii na ukusanyaji maduhuli.

Ameeleza kuwa juhudi hizo zimesaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea vivutio vya utalii ikolojia ambapo hadi kufikia Juni 2023 jumla ya watalii 242,824 walitembelea vivutio hivyo.

“Idadi hii ni ongezeko la asilimia 60.8 ukilinganisha na watalii 152,002 waliotembelea vivutio hivyo kwa kipindi hicho kwa mwaka 2021. Jumla ya sh.bilioni 1.3 zilikusanywa ikilinganishwa na sh.milioni 603.3 zilizokusanywa mwaka uliopita ikiwa ni ongezeko la Asilimia 126.9.”

Ameongeza kuwa :”Katika kipindi cha miaka miwili TFS tumeanzisha shamba jipya moja la Makere Kasulu-Kigoma, na kufanya upanuzi wa mashamba mawili.

Kuhusu utunzania wa miti profesa Silayo amesema katika mwaka wa fedha uliopita, TFS ilizalisha jumla ya tani 25.9 za mbegu za miti na kuotesha miche milioni 32.7 ya aina mbalimbali ambayo ilipandwa katika mashamba 24 ya serikali na mingine kugawiwa kwa watu binafsi, taasisi na mashirika mbalimbali kwa ajili ya kupandwa katika maeneo yao.

Ameeleza kuwa hadi sasa, TFS imepanda miti katika hekta 6,909 na kurudishia miti iliyokufa kwenye hekta 2,434 pamoja na kuendeleza mashamba ya miti kwa kupalilia hekta 31,197, kupogolea hekta 8,353 na kupunguzia miti kwenye hekta 2,785.

”Wakala umeandaa mkakati wa usimamizi na uendelezaji wa mashamba ya miti ya serikali wa miaka 30 kuanzia 2021 – 2050 ambao umelenga kupanua wigo wa aina ya miti ya ikiwemo ile ya madawa kama vile Prunus africana na mpira . Miti hii imeanza kupandwa katika mashamba ya Mbizi, Wino, Rongai, Saohill, Iyondo Mswima, Meru na Shume,”ameeleza

By Jamhuri