Na Deodatus Balile, Istanbul, Uturuki

Aprili 18, 2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, alifika katika Jiji la Ankara, nchini Uturuki kwa Ziara Rasmi ya Kiserikali.

Nimepata fursa ya kuwa katika ziara hii. Niseme Rais Samia amepokewa kwa heshima ya hali ya juu na mwenyeji wake, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, lakini si kupokewa tu, ziara hii imeifungulia Tanzania mlango muhimu wa kiuchumi.

Napenda kuamini msomaji umeishasoma au kuona kupitia TV na mitandao ya kijamii kuhusu ukubwa wa mapokezi yake, likiwamo gari lililompokea kumpeleka Ikulu ya Uturuki kuongozwa na farasi 70, kupigiwa mizinga 21, kukagua gwaride la heshima, kuandaliwa chakula cha jioni, lakini kubwa likiwa kusaini mikataba yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 6.4 sawa na Sh trilioni 17.3.

Sitanii, nadhani Watanzania bado tunayo kumbukumbu ya matumizi ya fedha za Uviko-19 zipatazo Sh trilioni 1.3, ambazo Rais Samia amezitumia kutenda mambo makuu katika nchi yetu.

Kwa kukumbusha tu, fedha hizo zimetumika kujenga madarasa 15,000 ya sekondari, madarasa 3,000 ya shule shikizi (jumla ni madarasa 18,000), kutengeneza madawati 462,795 na kujenga vyuo vya Ufundi Veta 32 nchini.

Si hivyo tu, fedha hizo Sh trilioni 1.3 za Uviko-19 zimenunua magari 25 ya kuchimba visima virefu (kila mkoa gari moja), mitambo mitano ya kuchimba mabwawa, kwa kila kanda kupewa gari moja, mitambo ya kupima ubora wa maji kila kanda. Katika hospitali amejenga ICU mpya 72, zimenunua magari ya wagonjwa (ambulance) 395 na magari ya chanjo 214.

Hizo hizo Sh trilioni 1.3 zimetumika kujenga mifumo ya Oxygen katika hospitali 82 nchini, zimenunua vitanda vya wagonjwa 2,700, mashine za X-ray za kisasa 85 na CT Scan 29. Kila mkoa sasa una CT Scan moja, badala ya zamani ambapo zilikuwa Bugando, Muhimbili, Hospitali ya Rufaa Mbeya na KCMC Moshi.

Aidha, fedha hizo pia zimenunua mashine za MRI kwa kila hospitali ya kanda, zikajenga vituo vipya vya afya zaidi ya 400 na mengine mengi.

Sitanii, nimerejea fedha za Uviko-19 ambazo zilikuwa Sh trilioni 1.3, kukujengea taswira msomaji wangu juu ya ukubwa wa fedha za mikataba iliyosainiwa kati ya Tanzania na Uturuki hizo Sh trilioni 17.3. Ikiwa Sh trilioni 1.3 zilifanya hayo niliyoyataja na mengine, zikiwamo boti za faiba za uvuvi, ebu fikiria Sh trilioni 17.3 zinakwenda kufanya kitu gani katika uchumi wa Tanzania. Ni kutokana na uzito wa kiwango cha fedha kilichotiliwa saini, nimeamua kuandika kichwa cha makala hii kuwa “Rais Samia amechagua fungu bora Uturuki”.

Ninavyofahamu zaidi ya dola bilioni 5 zitatumika kujenga reli ya kisasa (Standard Gauge). Ikiwa kuna watu walikuwa wanajiuliza iwapo reli hii itajengwa kweli, majibu sasa yako wazi. Reli inajengwa. Lakini binafsi wala nisizungumzie zaidi fedha zilizosainiwa mikataba hii, nieleze japo kwa ufupi eneo la biashara kati ya Uturuki na Tanzania.

Mwaka 2021 biashara kati ya Tanzania na Uturuki ilikuwa dola milioni 11 (Sh bilioni 29.7), lakini kufikia mwaka 2023 biashara imekua na kufikia dola milioni 350 (Sh bilioni 945). Katika mkutano na waandishi wa habari, Rais Samia na Rais Erdogan wamekubaliana nchi hizi kukuza biashara na kufikia dola bilioni 1 ndani ya mwaka mmoja.

Hii ina maana ziara hii ya Rais Samia imefungua milango kwa wafanyabiashara Watanzania kuja hapa Uturuki na kufanya biashara. Itakumbukwa kuwa wakati Uturuki imesaini mkataba wa dola bilioni 6.4 ambazo zinakuja moja kwa moja Tanzania, taifa kubwa kama Marekani lilikutanisha marais zaidi ya 50 wa Afrika na kuahidi dola bilioni 5 kwa nchi zote za Afrika… lakini sikia, hizo dola bilioni 5 zinatolewa kwa kiwango cha dola bilioni 1 kila mwaka kama msaada kwa nchi zaidi ya 50. Uturuki sasa inatoa kwa Tanzania pekee dola bilioni 6.4!

Kwa sasa Tanzania inauza kwa wingi dhahabu, tumbaku ghafi na bidhaa za kilimo hapa Uturuki, ambapo Uturuki inauza Tanzania bidhaa za viwandani zikiwamo nguo, vifaa vya ujenzi, mbolea, vifaa vya kilimo na vingine vingi. Ushirkiano wa nchi hizi mbili kwa sasa umejikita katika elimu, sayansi na teknolojia, afya, usafirishaji, ujenzi na maeneo mengine.

Kampuni inayojenga reli ndefu na yenye kasi kuliko zote katika Afrika Mashariki ya SGR iitwayo Yapi Merkez inatokea nchini hapa. Serikali ya hapa imetamka bayana kuwa inajivunia mradi huo wa ujenzi wa reli ya kisasa. Kilichonivutia zaidi, Uturuki imesema iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kujenga viwanda na kuhakikisha kuwapo kwa ujuzi.

Sitanii, nafahamu msomaji unajiuliza kwa nini Uturuki? Wakati tumezoea kusikia mataifa mengine na Uturuki haitajwi sana, uhalisia hili ni taifa kubwa ambalo limejengwa na Rais Erdogan. Uturuki ni nchi ya 19 kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani. Uchumi wake kwa sasa katika GDP ni dola bilioni 906, wakati sisi Tanzania GDP yetu ni dola bilioni 84. Kwa pato hili inakuwa moja ya nchi tajiri sana duniani zilizomo katika kundi la G20.

Nchi hii pamoja na kilimo, uchumi wake mkubwa unatokana na viwanda na huduma. Sekta za viwanda na huduma za fedha na utalii zinakua kwa kasi ya kutisha. Wakati Tanzania tunapambana kufikisha watalii milioni 2 na lengo la watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025, kwa hapa Uturuki ni maajabu. Nchi hii yenye watu milioni 84.9, inafanya maajabu katika utalii.

Kabla ya Uviko-19 mwaka 2019, nchi hii ilikuwa inapokea watalii milioni 45. Watalii milioni 45 kila mtalii akitumia dola 200 tu, inakuwa nchi hiyo imeingiza dola bilioni 9 sawa na Sh trilioni 24.3, kiasi ambacho ni nusu ya bajeti ya Tanzania kwa mwaka mzima. Kwa Uturuki madhara ya Corona yamekwisha. Mwaka 2022 nchi hii imepata watalii milioni 44.6. Kwa mwaka 2023 nchi hii imepata watalii milioni 49.2. Jiji la Istanbul pekee, limepokea watalii milioni 17.4.

Sitanii, hili nimelishuhudia. Hoteli ya Hilton Istanbul Bomonti yenye vyumba 829, vikiwamo vyumba 84 vya watu mashuhuri, tulipofika kutoka Ankara kuja hapa Istanbul tulikosa vyumba, ilikuwa imejaa. Tulipelekwa kwenye hoteli inayotajwa kuwa ndogo iitwayo Cevahir Hotel Istanbul Asia yenye vyumba 198, tukabahatisha vyumba, ambako unalipa dola 100 (karibu Sh 280,000) kwa kubembeleza. Hatimaye tulipata vyumba Hilton Hotel siku iliyofuata kwa mbinde.

Ukiwa hotelini, utadhani kuna harusi muda wote. Kila wakati yanaingia makundi ya watu wakiwa na mabegi, watoto kwa wakubwa. Kikubwa zaidi, hupewi ufuguo wa chumba hadi uwe umelipia. Ukichelewa kulipa, chumba kinauzwa ukiwa umesimama kwenye msitari. Hao watalii milioni 49.2, hakika unawaona.

Rais Samia amefungua sekta ya utalii kupitia sinema aliyoshiriki ya Royal Tour. Kwa hakika nilichokiona hapa Uturuki, Rais wetu ameona mbali. Takwimu hazidanganyi. Vitabu vya hesabu za serikali vya hapa Uturuki, vinaonyesha kwa mwaka 2003 utalii umeliingizia taifa hili dola bilioni 12.27 (sawa na Sh trilioni 33.1). Uturuki tayari wana ndege ya kila siku inayokuja hapo Tanzania ya Turkish Airline. Wamesaini mkataba na ATCL katika mikataba iliyosainiwa. Hii ni fursa ya watalii kuja moja kwa moja Tanzania.

Sitanii, ndege ni biashara ya aina yake. Kumbe ukiangalia kutoka Dar es Salaam hadi Ankara au Istanbul, Uturuki ni mwendo wa saa 8 hewani. Kwa meli inatumia siku 54 hadi 90 kulingana na njia uliyopitia. Inawezekana, narudia, inawezekana nauli ya ndege isikulipe, lakini ndege ikisafirisha watalii wakaja Tanzania kwa wingi, wakilala katika hoteli, wakanunua vitu na kuingia kwenye mbuga, faida itakuwa kubwa kuliko nauli. Hili si somo la leo.

Safari ya kisiasa ya Rais Erdogan ilianza rasmi mwaka 1994 alipochaguliwa kuwa Meya wa Jiji la Istanbul. Kazi ya kwanza, alimaliza tatizo la maji kwa kujenga mfumo na mtandao wa maji katika Jiji la Istanbul kwa mamia ya mabomba ya maji. Suala la pili alilofanya ni kujenga mfumo wa kisasa wa kukusanya na kuteketeza taka, hali iliyoufanya Mji wa Istanbul kuwa msafi kuliko miji yote nchini hapa. Suala la tatu, aliondoa msongamano wa magari jijini Istanbul. Akiwa Meya kati ya mwaka 1994 na 1997 alijenga madaraja (flyovers) 50 katika jiji hili. Mameya wa miji mingine yote walikuja Istanbul kujifunza kuhusu mengi mazuri aliyoyafanya kwa ufanisi mkubwa.

Wakati anaingia kuwa Meya, alikuta Jiji la Istanbul lina madeni ya wastani wa dola bilioni 2 (Sh triliolini 5.4). Alianzisha miradi mikubwa yenye thamani ya dola bilioni 4 (Sh trilioni 10.8) hadi deni lote likalipwa, lakini Julai 12, 1997 akiwa katika mji wa Siirt, alisoma hadharani shairi lililokuwa limepigwa marufuku na serikali likipinga umaskini kwa Waturuki.

Kitendo cha kusoma shairi hilo kilihitimisha umeya wake, kwani alikamatwa akafunguliwa mashitaka na akafungwa jela, alikotumikia kifungo miezi minne. Agosti 14, 2001 alianzisha chama kilichojulikana kama Justice and Development Party (AK Party), yeye akawa Mwenyekiti. Mwaka mmoja baadaye katika uchaguzi mwaka 2002 chama hicho kilishinda theluthi mbili ya viti vya Bunge la Uturuki.

Rais Edogan hakuweza kushiriki uchaguzi wa Novemba 3, 2002 kutokana na hukumu aliyokuwa ametiwa hatiani mwaka 1997, lakini Machi 9, 2003 alishiriki uchaguzi mdogo baada ya kuwa ameondolewa jinai na mahakama, akashinda. Mwaka huo huo akawa Waziri Mkuu wa Uturuki. Uchumi wa Uturuki wakati huo ulikuwa na hali mbaya.

Akiwa Waziri Mkuu Mtendaji, alisukuma sera ya viwanda na sekta ya huduma ukiwamo utalii, ambapo uchumi ulianza kuimarika kwa nguvu kubwa. Alifuta sifuri sita nyuma ya fedha ya Uturuki (lira), yaani noti ya Sh 10,000,000, ilichapishwa upya na kuwa noti ya Sh 10. Hadi sasa dola moja ya Marekani ni sawa na Lira 32. Wengi wanamwona Rais Erdogan kuwa ni mkombozi wa kweli wa Taifa la Uturuki.

Nchi za Magharibi, miaka ya uongozi wa Rais Erdogan zimekuwa zikiitaja kama “Mapinduzi ya Kimyakimya ya Uchumi” kwani ameifanya nchi hii iliyokuwa haifahamiki kokote, ikiwa na migogoro ya kisiasa, mauaji, amani ikiwa bidhaa adimu, lakini sasa ni nchi inayotoa misaada kwa mataifa mengi duniani kutokana na uchumi wake mkubwa ambao ni wa 19 duniani.

Kutokana na historia ya Uturuki, mpango wa marais wetu wawili kukuza biashara kutoka dola milioni 350 hadi dola bilioni 1 ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa, naamini na narudia, napenda kuamini kuwa “Rais Samia amechagua fungu bora Uturuki”. Hawa angalau wanayo kumbukumbu ya matatizo ya uchumi na wanaweza kutusaidia kwani maisha yetu yanafanana.

Jambo moja niwatie moyo Watanzania, kumbe si lazima kufahamu Kiingereza ndipo ukuze uchumi. Katika hoteli nyingi tunapokwenda, madereva teksi, kwenye maduka ya nguo na kila sehemu, Waturuki hawajui Kiingereza, wanajua Kituruki.

Ukimuuliza jambo, anaingia kwenye Google anaandika inamtafsiria, mnaelewana. Yeye anaandika Kituruki, wewe unaandika Kiingereza, Google inatafsiri, mnaelewana. Kumbe KISWAHILI chetu kinatosha. Tujenge mifumo na tuwekeze kwenye viwanda, Tanzania kuwa tajiri inawezekana. Hongera Rais Samia kwa uchaguzi ulioufanya wa kushirikiana na Uturuki.

Mwandishi anapatikana kwa simu 0784404827

By Jamhuri