Na Byarugaba Innocent, JamhuriMedia, Kibaha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewapunguzia mwendo wa Km.5 wananchi wa Kata ya Sofu kufuata huduma za afya kwenye maeneo mengine.
Takribani milioni 200 zimekamikisha jengo la Zahanati Kata ya Sofu itakayohudumia zaidi ya Wananchi 8,000 wa Mitaa ya mitatu ya Msufuni,Twendepamoja ,Sofu na mitaa mingine ya jirani ikinufaika na huduma hizo za kitabibu
Uzinduzi rasmi wa Zahanati hiyo umefanywa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Mussa Ndomba mapema wiki Jana ambapo aliwaongoza mamia ya wahudhuriaji kupata huduma za awali za kitabibu ikiwemo vipimo vya Shinikizo la damu,uzito,chanjo ya UVIKO-19,Upimaji wa saratani ya shingo ya Mlango wa Kizazi,ushauri wa ulaji mzuri na uchangiaji damu ambapo jumla ya watu 97 walipata huduma,amesema Mganga Mkuu wa Halmashauri Peter Nsanya
Ndomba ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sofu aliwapongeza wananchi kwa ushirikiano waliouonesha wakati wa ujenzi,majirani wa Zahanati hiyo kwa kutambua na kuthamini umuhimu wake na kuweza kujitolea kwa hali na Mali ili kufikia azma yao.
“Natumia fursa hii kuwapongeza Sana watangulizi wangu wa Kisiasa Mhe.Robert Machumbe na Mhe.Mbonde walionesha njia,wamelinda kiwanja nami nimekuja kukamilisha,nitoe rai kwa wananchi tuendelee kubuni miradi mingine yenye tija na tuendelee kuwa na ushirikiano na mshikamano kulinda rasilimali zetu kwa Maendeleo ya Taifa letu” ..amesema Ndomba
Kwa upande wake Mwanadiplomasia Balozi mstaafu Michael Seleki aliyewahi kuhuduma Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ameungana na Wananchi wengine kumshukuru na Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyomwaga fedha kwenye sekta zinazogusa maisha ya Mtanzania moja kwa moja ikiwemo Sekta ya afya, elimu, maji, barabara kwa uchache na kwamba ndani ya kipindi miaka miwili ya uongozi wake Maendeleo yametamaraki.
Aidha,Balozi Seleki amesifu uongozi na falsafa ya mafiga manne yanavyoshirikiana ili kumletea Maendeleo Mtanzania ikiwa ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa,Diwani wa Kata,Mbunge wa Jimbo na Rais wa nchi na Sasa wananchi wanafurahia uwakilishi wao kuanzia ngazi ya chini mpaka juu.
Mtendaji wa Kata ya Sofu Swaum Nkullo ametanabaisha kuwa ujenzi umegharimu takribani shilingi 200 milioni ambapo kati yake milioni 100 zikitoka Serikali kuu na zinazosalia zikiwa ni mapato ya Halmashauri na nguvu za wananchi na mchango wa Mbunge.