Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian kufuatia vifo vya watu 18 vilivyotokea katika ajali ya gari.
Ajali hiyo imetokea leo saa 5 asubuhi katika kata ya Uchama, tarafa ya Nyasa wilaya ya Nzega mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora CP Richard Abwao waliopoteza maisha ni wanaume 14 akiwemo mtoto mmoja na wanawake 4.
Majeruhi ni 60 ambapo majeruhi 51 wanatibiwa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, 19 wako Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, 1 anatibuwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando na 9 wametibiwa na kuruhusiwa.
CP Abwao amesema ajali hiyo imehusisha basi la kampuni ya Alfa lililokuwa likisafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam ambalo liligongana na Lori la mafuta lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza.
Rais Samia anawapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina.