Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa kunako tarehe 19 Aprili 19, 1968 na Askofu mkuu Pierluigi Sartorelli akateuliwa kuwa ni Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania, utume alioutekeleza hadi tarehe 22 Desemba 1970. 

Uhusiano huu kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakati akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Ali Abeid Aman Karume wa Tanzania mjini Vatican unasimikwa katika tunu msingi za: Amani, haki, mshikamano na uhuru, kwani haya ni mambo yanayopata asili yake kutoka katika utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa msukumo wa pekee. Tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika nyanja za elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila kusahau huduma ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu nchini Tanzania na katika mchakato wa kudumisha amani ulimwenguni.

Ujumbe wa Tanzania na Baba Mtakatifu Francisko

Takwimu zinaonesha kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linamiliki na kuendesha shule za awali 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 244, vyuo vya ufundi, vyuo vikuu 5; taasisi za elimu ya 5 na vituo vya vyuo vikuu 2 ambavyo viko chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, SAUT. 

Vyuo vyote hivi vina jumla ya wanafunzi 31, 000 pamoja na taasisi za afya ni 473, lengo likiwa ni kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Kuna uhusiano mkubwa kati ya shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki pamoja na dhamana ya Uinjilishaji wa kina inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Uinjilishaji nchini Tanzania. 

Ili kutambua umuhimu huu, kuna haja kwanza kwa walimu, walezi na wanafunzi wenyewe kufahamu changamoto inayoletwa na Kanisa kwa wakati huu! Shule na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, vimekuwa ni vituo vya majiundo makini ya vijana: kiakili, kimaadili, kiroho na kiutu, kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa, ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho nchini Tanzania. 

Elimu bora inayotolewa na Kanisa inalenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiamini na kumudu ushindani wa kitaifa na Kimataifa kwa kuwapatia: elimu, ujuzi na uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Tanzania katika ujumla wake.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na Ujumbe wa Tanzania

Shule, vyuo, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vimekuwa ni vituo vya majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa kurithisha imani, maadili na utu wema. Kutokana na dhamana hii, vijana wanapaswa kuwa kweli ni wadau wa uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yao adili. 

Jambo msingi kwa walimu, wazazi na walezi ni kutambua dhamana na utume wa shule za kikatoliki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuwajengea watoto na vijana msingi wa imani, maadili na utu wema. 

Hapa ni mahali pa kujenga na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani, ili wanafunzi wanaohitimu kutoka katika shule za Kikristo waweze kuwa kweli ni wadau katika kuyatakatifuza malimwengu. Dunia inawahitaji vijana watakaotoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kwa kutambua kwamba, shule na taasisi hizi ni vyombo makini vya mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho!

Rais Samia akipokea zawadi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko

Imegota takribani miaka 17 tangu Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 19 Januari 2012. Katika mazungumzo ya dakika kumi na tano, viongozi hawa wawili waligusia kuhusu: Majadiliano ya kidini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, Afya, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Ni katika muktadha wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, tarehe 12 Februari 2024, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baadaye, Rais Samia amebahatika pia kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. 

Katika mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika ishirini na tano, wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta ya: elimu, afya na ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa. Baadaye, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii nchini Tanzania; masuala ya kikanda na Kimataifa na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa katika kujikita katika kudumisha amani ulimwenguni.

Rais Samia akimpatia zawadi Baba Mtakatifu Francisko

Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara hii ya kitaifa, alikuwa ameambatana na Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania. Prof. Deogratias Rutatora, Mwenyekiti Halmashauri ya walei, Taifa; Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA; Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar pamoja na Theresia Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam. 

 Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania kunako mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezeshe watanzania kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria: ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwaombea Watanzania paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu.

 Aliwaombea upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila, utaifa ili watanzania wote waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanzania na majirani zake; viongozi wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni milele na milele!

Watanzania wakiwa na Rais Samia Suluhu Hassana mjini Roma